Thursday, January 27, 2011

Askofu Dr.Maternus Kapinga atahadharisha serikali kuhusu amani na upendo kwa watanzania

 
Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma Dk.Maternus Kapinga katika moja ya huduma za kiroho kwa waumini wa kanisa hilo picha na Albano Midelo.
Na Albano Midelo
ASKOFU wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma mhashamu Dr.Maternus Kapinga  ameikumbusha serikali kuendelea kusisitiza amani,upendo na umoja kwa watanzania ili Taifa liendelee  kuwa kisiwa cha utulivu.

Dr.Kapinga ameyasema hayo  wakati anahubiri katika adhimisho la  misa  takatifu ya kumtolea mwenyezi Mungu sadaka ya shukrani kwa kutimiza miaka 11 ya uaskofu,miaka 25 ya ukasisi na miaka 15 ya ndoa yake.

Mhashamu Dr.Kapinga ametoa rai kwa serikali kuanzia ngazi ya kijiji,kata,tarafa,wilaya,mkoa hadi Taifa  kuendeleza mitazamo aliyoiacha Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere siku zote kuhubiri amani,upendo na utulivu hali ambayo alisema imeifanya nchi kuendelea kuwa kisiwa cha amani.

Hata hivyo kwa namna ya pekee Askofu Dr.Kapinga ameipongeza serikali ya mkoa wa Ruvuma kuanzia ngazi ya kijiji,kata,tarafa,wilaya na mkoa kwa  ushirikiano mkubwa ambao wameutoa katika kanisa la Anglikana hali ambayo imeleta amani kubwa miongoni mwa waumini wa kanisa hilo na kusisitiza kuwa serikali  imefanya kazi ya kuleta amani alioagiza Mungu moja kwa moja.

Dr.Kapinga alibainisha kuwa katika kipindi chake cha uongozi katika Dayosisi hiyo amekumbana na mafanikio makubwa ya kimwili na kiroho kwa waumini licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zilitokana na waumini wachache  ambao walipania kuuangusha uongozi halali  wa kanisa hilo.

“Mwaka 2010 ulikuwa na matukio ya ajabu kwa kanisa likiwepo tukio la Machi,30,2010 ambapo maadui wa kanisa la Anglikana kwa kufadhiliwa  walipanga kuuangusha uaskofu wangu kutokana na nguvu ya fedha walifanikiwa kuteka kila kitu,lakini walisahau kuwa uaskofu wangu nimewekwa na Mungu,mpango wao ukashindikana na ngome ya mwisho ya maadui wa kanisa  imeanguka huko Chiulu Nyasa na hivi sasa kanisa katika Dayosisi nzima ya Ruvuma ni jeupe,lenye upendo na amani”,anasisitiza.

Askofu Kapinga amewashukuru waumini wa kanisa kuu la mtakatifu Nicholous ambalo anasema siku zote limesimama imara katika kutetea haki za kanisa hilo dhidi ya maadui wachache ambao kwa makusudi walitaka kuliingiza kanisa hilo katika migogoro na kuhatarisha amani ya kanisa la Mungu.

Tovuti;www.maendeleonivita.blogspot.com



No comments:

Post a Comment