Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dr.Christine Ishengoma akizungumza kwenye ukumbi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma
Na Albano Midelo
ROSE Chale mkazi wa Songea ambaye amejifungua mtoto njiti katika hospitali ya mkoa Ruvuma iliyoko mjini Songea, anawapongeza madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa huduma nzuri.
Maria Ponela mkazi wa wilaya ya Namtumbo, mzazi mwingine, anasema mapokezi katika hospitali hiyo yalikuwa mazuri. Anasema wauguzi walimpokea vizuri katika huduma ya upasuaji na kwamba ameridhika na huduma inayotolewa katika wodi ya wazazi.
Asha Abdalah mkazi wa Namtumbo, anasema alipokewa vizuri na alijifungua salama mtoto wa kiume.
Mwangasa Kaisi, mkazi wa Masuguru wilayani Namtumbo, aliyejifungua mtoto wa sita kwa operesheni katika hospitali ya mkoa, anasema anawapongeza madaktari na wauguzi wa hospitali ya mkoa kwa kumfanyia upasuaji mara mbili na hivi sasa hali yake inaendelea vizuri.
Anasema angekuwa Namtumbo, pengine angepoteza maisha kwa kuwa walishindwa kutambua iwapo mtoto amekaa vibaya na kwamba hospitali ya mkoa ndio walitambua kuwa mtoto ametanguliza mgongo.
Kila mmoja ana kauli yake. Wakati hawa wanasema hawapati huduma nzuri, wengine wanasema wamehudumiwa vizuri. Hizi ndizo changamoto za hospitali ya serikali ya mkoa mjini Songea, mkoa wa Ruvuma.
Amina Athumani mkazi wa Majengo, Songea mjini anasema alipokwenda kujifungua katika hospitali ya mkoa, aliposhikwa uchungu akiwa kitandani, alimwita muuguzi na kuomba msaada, lakini muuguzi alimwambia muda bado. Hivyo alijifungua peke yake na mtoto wake kuanguka sakafuni.
“Nilimwambia muuguzi njoo unisaidie lakini alikataa akidai kuwa amenipima muda wa kujifungua bado; mtoto akatoka na kuanguka chini ingawa mtoto wangu hakufa,” anaeleza Amina.
Mohamedi Kudeka, mkazi wa Msamala Songea mjini anasema wodi ya wazazi katika hospitali ya mkoa haina vitanda vya kutosha. Hili ndilo linasababisha akinamama zaidi ya mmoja kulala katika kitanda kimoja tena wakiwa na watoto wao waliojifungua.
“Nimeshuhudia wakati fulani akinamama wajawazito wanalala chini. Walio katika matazamio ya kujifungua nao wanahangaika kupata sehemu za kulala; inafikia mahali wanalala sakafuni. Hali hii haileti picha nzuri hasa kwa hospitali ya serikali ambayo inatumia fedha za walipakodi,” anaeleza.
Kudeka anasema mke wake alipokuwa mjamzito alimpeleka pale hospitali ya mkoa majira ya saa tano usiku. Alijifungua kwa kufanyiwa upasuaji. Aliandikiwa dripu za na dawa lakini aliambiwa dawa hakuna hivyo aende kununua duka la jirani na hospitali.
“Katika mazingira haya, tena saa sita usiku, unaweza kupoteza maisha,” analalama Kudeka.
Pamoja na furaha ya wachache waliobahatika kujifungua vizuri, bado vifo vya akina mama nchini na mkoani Ruvuma, ni changamoto kubwa kwa serikali.
Katika mkoa wa Ruvuma kasi ya kupunguza vifo hivyo ni ndogo na hairidhishi. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 1999 vifo vya wajawazito vilikuwa 260 na mwaka 2007vilipungua hadi kufikia 182 kwa wazazi 100,000.
Uchunguzi umebaini kuwa kasi ya kupunguza vifo hivyo ni ndogo hali ambayo inaufanya mkoa wa Ruvuma kuchangia ongezeko la vifo vya wazazi kitaifa.
Ongezeko hilo la vifo vya wajawazito katika mkoa wa Ruvuma linatajwa kutokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha ya uzazi, hali ambayo inaleta ugumu katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa zipo sababu nyingine nyingi zinazoleta vifo vya wajawazito katika mkoa wa Ruvuma zikiwemo, upungufu wa vituo vya kutolea huduma za afya, ukosefu wa dawa, wataalamu, vifaa vingine hospitalini; na kuwepo miundombinu hafifu ya barabara.
Ofisa muuguzi anayeshughulikia afya ya mama na mtoto kutoka katika hospitali ya mkoa, Bi Irmunda Komba anazitaja sababu zinazoleta vifo vya akina mama wajawazito kuwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua.
Anataja nyingine kuwa ni upungufu wa damu, shambulio la malaria, ukimwi, kifafa cha mimba na kuchelewa kufika katika vituo vya kutolea huduma kutokana na shida ya usafiri.
Muuguzi katika wodi ya wazazi ya hospitali hiyo, Modestuta Mwageni anasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya idadi kubwa ya akinamama wajawazito.
Anasema wakati mwingine wanafika kati ya 25 hadi 40 kwa siku na kuzidi uwezo wa wodi; hali inayosababisha kitanda kimoja kutumiwa na wajawazito kati ya wawili na watatu.
“Hospitali hii ni ya mkoa. Inategemewa na wananchi kutoka wilaya za Songea, Namtumbo pamoja na wilaya zote na hata nje ya mkoa. Wagonjwa wengi wanaoshindwa kujifungua wanafika hapa kwa ajili ya upasuaji; hivyo idadi ya wagonjwa katika hospitali ya mkoa ni kubwa ukilinganisha na idadi ya wauuguzi na madaktari waliopo,” anasema Dk. Modestuta Mwageni.
Anakiri kupata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, ukiwemo upungufu wa dawa na ukosefu wa huduma kama inavyotakiwa. Anasisitiza kuwa hospitali haina uwezo wa kumudu ipasavyo wagonjwa wote wanaofika katika hospitali hiyo; hivyo ametoa mwito kwa wananchi kuwa na subira.
Kuhusu vifaa vya awali kwa ajili ya mjamzito kujifungulia, muuguzi Dk.Mwageni anasema mjamzito anatakiwa kuviandaa mwenyewe kwa kuwa anaweza kujifungulia njiani. Anasema mpira, nguo na dishi vitamsaidia mama pale akipata dharura ya kijifungua na kwamba wanaelekezwa kila kitu wakati wakienda kliniki.
Akizungumzia tatizo la upungufu wa dawa katika hospitali ya mkoa, mganga mkuu wa mkoa Dk. Daniel Malecela amekiri kuwa tangu mwezi Mei mwaka jana, hospitali imekuwa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kununulia dawa ambapo nguvu kubwa imekuwa inawekwa katika ununuzi wa dawa kwa ajili wajawazito na watoto.
Taarifa ya hospitali hiyo inaonesha kuwa kuna uhaba wa watumishi wakiwemo madakatari na wauuguzi na kwamba madaktari waliopo katika hospitali hiyo hivi sasa ni asilimia 32 tu; hivyo kuna uhaba wa madaktari wa asilimia 68.
Madaktari bingwa katika mkoa mzima wa Ruvuma ni changamoto kubwa inayosababisha wananchi, hasa wanawake kukosa huduma bora ya afya ambapo uwiano unaonesha kuwa daktari mmoja katika mkoa anahudumia watu 36,624 wakati uwiano wa kitaifa ni daktari mmoja kwa watu 25,000.
Kutokana na uhaba huo, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba katika hospitali hiyo kumekuwa utoaji wa huduma zisizoridhisha zinazoendana na mazingira ya rushwa ili kupata huduma bora.
"Taaluma ya muuguzi au daktari ni kuokoa uhai wa mgonjwa wake na sio kuua. Pale panapotokea kasoro tutaendelea kutoa elimu na katika hospitali ya mkoa kuna utaratibu kila wakati viongozi wa hospitali kukutana na wafanyakazi wake na kupeana mikakati ya kufanya kazi vizuri ili kuepusha vifo au lawama kutoka kwa wananchi," anasisitiza Dk. Malecela.
Wanawake wengi wajawazito wanafariki duniani kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kujifungulia majumbani au kwa wakunga wa jadi wenye ujuzi haba.
Akinamama wengi hasa katika maeneo ya vijijini hawana uwezo wa kupata fedha kwa ajili ya matibabu na wanashindwa kuzifikia huduma za afya kutokana na vituo vya huduma kuwa mbali.
Takwimu za kitaifa zilizotolewa na shirika la UTU MWANAMKE zinaonesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa wauguzi, wakunga na madaktari. Kulingana na takwimu hizo wakunga zaidi ya 3000 na wauguzi zaidi ya 8000 wanahitajika.
Kila saa moja mwanamke mmoja hufariki dunia kutokana na matatizo ya ujauzito au matatizo mengine ya uzazi; ambapo kwa mwaka zaidi ya wanawake 8000 hufariki dunia kutokana na matatizo ya uzazi.
Maelfu ya wanawake wanaonusurika na kifo wakati wa kujifungua hupata matatizo mengine makubwa kiafya ukiwemo ulemavu wa kudumu na tatizo la kuvuja mkojo au kinyesi mfululizo; yaani fistula.
0766463129
No comments:
Post a Comment