Pichani ni baadhi ya wanafunzi viziwi katika shule ya St.Vinsent Songea wakifurahia mazingira mazuri ya kusomea pamoja vifaa muhimu wakiwemo walimu wa kutosha wa walemavu
Halmashauri nzima ya Mtwara hakuna shule wala mwalimu wa walemavu
Na Albano Midelo
Ni ukweli usiopingika kuwa elimu ni haki ya kila mtanzania pasipo kubagua,uwezo,jinsia ama namna mtu anavyooneka.Hata hivyo haki hii ya kupata elimu inaweza isitolewe kikamilifu kwa baadhi ya makundi kama la watu wenye ulemavu pale ambapo mazingira ya upatikanaji wa haki hiyo yanakuwa magumu.
Mwaka 2002 takwimu za shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto(UNICEF) zilionesha kuwa asilimia 98 ya watoto wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hawapatiwi kabisa elimu jambo ambalo ni hatari kwa walemavu.
Imeelezwa kuwa asilimia hii ndogo inasababishwa na kuwepo kwa shule chache maalum hapa nchini kwa ajili ya watu wenye ulemavu,ukosefu wa wataalamu,sera na sheria nyingi za nchi hizo zinazosimamia sekta ya elimu hazitaji moja kwa moja au kutoa utaratibu mzuri wa kutoa elimu kuhusu wenye ulemavu,ukosefu wa vifaa maalum na muhimu vya kuwawezesha kusoma pamoja na miundo mbinu duni katika shule zilizopo na vyuo isiyotosheleza na kukidhi mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu.
Hali ya walemavu wengi kukosa elimu inachangiwa na mtazamo hasi wa jamii kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kumnyanyapaa na kutomwendeleza mlemavu ikiwemo kumtenga na kutompeleka mtoto mwenye ulemavu shule,ukosefu wa utashi wa kisiasa hapa nchini na serikali kutozingatia mikataba ya kimtaifa iliyosiniwa na kuridhiwa inayotambua haki sawa kwa watu wenye ulemavu.
Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo wakazi wake wengi wanatajwa kuwa hawana mwamko kabisa wa kielimu jambo linalosababisha watoto wengi ambao wanatakiwa kuwa shule kutoandikishwa shule au kuacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro na mimba kwa watoto wa kike.
Takwimu za watoto wa kike kuacha shule kwa kupata mimba na utoro sugu zinatisha katika mikoa ya kusini hususani Mtwara na Lindi jambo ambalo linarudisha nyumba harakati za serikali ya awamu ya nne ya kujenga shule za sekondari katika kila kata ambapo katika mikoa hiyo shule zinakabiliwa na upungufu wa wanafunzi kutokana na wengi kuacha shule pamoja na utoro.
Uchunguzi umebaini kuwa hali ni mbaya zaidi kwa watoto wenye ulemavu ambapo takwimu za mwaka 2009 kutoka Halmashauri ya wilaya ya Mtwara zinaonesha kuwa watoto wenye ulemavu ambao wanasoma shule za msingi katika wilaya hiyo wenye umri kati ya miaka sifuri hadi 13 ni 300 tu kati ya walemavu 600 wanaostahili kuwepo shule za msingi.
Daniel Mbena ni mratibu wa elimu maalum katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara anasema wanafunzi hao wenye ulemavu ambao wanasoma katika Halmashauri hiyo wanasoma katika shule za kawaida na kufundishwa na walimu wa kawaida kwa njia za kawaida kutokana na wilaya hiyo kukosa shule,kitengo na walimu wa walemavu..
Kwa mujibu wa Mbena katika Halmashauri nzima ya Mtwara hakuna shule, kitengo wala mwalimu hata mmoja aliyesomea kufundisha watoto wenye ulemavu jambo ambalo linaleta ugumu kwa watoto hao kupata elimu maalum ambayo inatolewa kwa watoto wenye ulemavu.
“Mimi kama mratibu wa walemavu baada ya kufika Mtwara Oktoba 2009 kitu cha kwanza niliamua kuzunguka katika Halmashauri nzima ili kutambua takwimu sahihi za walemavu ambazo tayari nimezipata ,ninachofanya sasa ni kuhamasisha wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu kuwaandikisha shule watoto wao pamoja na kutoa elimu kwa jamii nzima ili kuwatambua walemavu”,anasema.
“Mwamko wa kuwatambua wenye ulemavu hivi sasa umeanza kwa taratibu sana kwenye Halmashauri yetu kwa kuwa wilayani Mtwara mwamko wa elimu kwa ujumla kwa makundi yote haupo hivyo tunatakiwa kufanyakazi ya ziada ili wananchi watambue umuhimu wa elimu kwa walemavu tunatarajia kuanzisha shule ya bweni kwa ajili ya walemavu ambapo tutawakusanya walemavu wote vijijini ili wasome katika shule hiyo”,anasisitiza.
Kulingana na Mbena takwimu za wanafunzi wenye ulemavu waliomo katika shule za msingi,sekondari na vyuo katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu zinaonesha kuwa shule za msingi ni wanafunzi 28 kati ya hao wavulana 13 na wasichana 15,sekondari wanafunzi wawili tu ambao ni mvulana mmoja na msichana mmoja.
Mchanganuo unabainisha kuwa wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma shule za msingi wasioona ni 13 kati yao wavulana watano na wasichana 13,albino 21 kati yao wavulana 15 na wasichana sita,wenye ulemavu wa akili 55 kati yao wavulana 38 na wasichana 17,walemavu wa viungo 151 kati yao wavulana 92 na wasichana 59,viziwi wasioona 12 na wenye ulemavu mwingine ni 43.
Uchunguzi umebaini kuwa hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wenye ulemavu shule za sekondari na vyuo ambapo walemavu wasioona sekondari yupo mmoja tu ,hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye ni albino, mwenye ulemavu wa akili,viziwi wasioona na kwamba hakuna mwanafunzi mwenye ulemavu hata mmoja ambaye amepata nafasi ya chuo.
Mratibu wa elimu maalum katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara anaelezea masikitiko yake kutokana na wilaya hiyo kutokuwa na shule wala mwalimu kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu hali ambayo inasababisha wanafunzi wengi wenye ulemavu ambao walistahili kuwepo shuleni kutoandikishwa na walemavu wanasoma kuwa watoro.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watoto wenye ulemavu wasiohudhuria masomo katika shule za msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara ni zaidi ya 250 wakiwemo viziwi 49,wasioona tisa,albino sita,walemavu wa akili 110,viziwi wasioona tisa,walemavu wa viungo 54,na ulemavu mwingine 15.
Changamoto nyingine ni Halmashauri hiyo kutokuwa na mwalimu hata mmoja kwa ajili ya wenye ulemavu kuanzia shule za msingi,sekondari na vyuo,kutokuwepo shule hata moja ya msingi na sekondari kwa ajili ya wenye ulemavu,kutokuwa na vifaa vya kisayansi vya elimu ikiwemo Audiometers,speech trainers na parking Braillers.
Kutokana na hali hiyo Mbena anapendekeza wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kuwezesha ujenzi wa angalau shule moja maalum ya walemavu pamoja na kusaidia kufungua vitengo vya elimu maalum pamoja na kutoa ombi maalum kwa wizara kutoa nafasi za upendeleo kwa walimu wa wilaya hiyo ili kujiunga katika chuo cha elimu maalum cha Arusha ngazi ya cheti kwa ajili ya walemavu.
Uchunguzi umebaini madhara ambayo wanayapata walemavu wilayani Mtwara kutokana na kukosa elimu ya msingi,sekondari na vyuo ni pamoja na idadi kubwa ya ombaomba,kukosa ajira,kuwa mzigo katika jamii,kuwa tegemezi,umaskini unaongezeka kwa kasi,wanashindwa kupata taarifa na habari mbalimbali kwa kukosa njia muafaka ya mawasiliano hivyo kukosa mambo mengi ya kitaifa ikiwemo elimu ya dhidi ya UKIMWI.
Deodata Mnunduma ni mwalimu katika shule ya msingi Rahaleo wilayani Mtwara anasema mwamko wa kuwasaidia walemavu kupata elimu katika wilaya hiyo ni hafifu sana kwa kuwa hadi sasa jamii bado haitambui umuhimu wa watu wenye ulemavu kupata haki zao za msingi kama elimu wanaamini kuwa walemavu ni watu tegemezi na hawana umuhimu katika Taifa.
Abdalah Ally mfanyabiashara wa mjini Mtwara, anadai kuwa jamii kwa ujumla katika wilaya ya Mtwara bado ina mtazamo hafifu kuhusu walemavu ndiyo maana wanaachwa bila kupatiwa hata elimu ambayo ndiyo ukombozi na kwamba hata Baraza la madiwani katika Halmashauri ya Mtwara halijaweka mikakati kabambe ya kuwakomboa walemavu kielimu.
“Mwandishi hebu fikiria katika Halmashauri nzima hakuna shule hata moja ya msingi wala sekondari kwa ajili ya walemavu,wakati hivi sasa kuna utitiri wa shule za msingi na sekondari karibu kila kata nchini,hapa tunahitaji wanasiasa wenye utashi ambao wanatambua kuwa walemavu ni sawa na watu wengine wanahitaji kupata fursa sawa katika nchi yetu”,anasisitiza.
Uchunguzi uliofanywa katika viunga mbalimbali vya mji wa Mtwara umebaini kuwa idadi ya omba omba wanaoongoza katika manispaa ya Mtwara ni watu wenye ulemavu kutokana na kutowezeshwa na kupewa fursa ya elimu hali ambayo inawafanya waone hakuna njia nyingine ya kujipatia riziki zaidi ya kuomba .
Kutokana na hali hiyo Ally Hamisi na Hawa Abdalah wanashauri kuwa jamii ya Mtwara inatakiwa kubadilika kifikra na kimtazamo kwa kuwasaidia wenye ulemavu kwanza kuwapatia elimu na wale ambao wamekosa elimu kuwezeshwa kiuchumi na kuwapatia japo elimu ya ufundi ili waweze kujikomboa kimaisha hivyo kutokuwa tegemezi tena katika jamii inayowazunguka.
Baruapepe amidelo@yahoo.com,simu 0766463129.
No comments:
Post a Comment