Na Albano Midelo,Mbinga.
ASKOFU wa jimbo la Mbinga mhashamu John Ndimbo pichani kulia ameanza kazi yake ya uaskofu kwa nguvu,kasi na ari baada ya kutoa sakramenti ya kipaimara kwa wanafunzi 201 katika parokia za Liparamba na Mpepo .
Kati ya wanafunzi hao wanafunzi 82 ni kutoka katika shule za msingi parokia ya Mpepo kata ya Tingi na wanafunzi 119 wanatoka katika parokia ya Liparamba kata ya Liparamba.
Akihubiri katika kanisa la mtakatifu Joseph la parokia ya Mpepo mara baada ya kutoa sakramenti hiyo ya kipaimara mhashamu Ndimbo aliwapongeza makatesta kwa kazi nzuri walioifanya ya kuwandaa wanafunzi hao baada ya kujibu maswali yote ya kiimani aliowauliza wanafunzi hao.
“Jambo jema haliwezi kufanywa bila ya uwepo wa roho mtakatifu hawezekani kuuishi ukristo wetu kwa kuwa bila nguvu yake binadamu hana kitu kabisa ‘’,alisisitiza mhashamu Ndimbo.
Askofu Ndimbo amewaagiza wanafunzi waliopata kipaimara kueneza na kutetea imani sahihi ya Yesu kristo kwa maneno na matendo yao kama mashahidi wa mwokozi,kukiri kwa ujasiri jina la kristo na kamwe wasiuonee aibu msalaba wake ambao ni siraha katika imani.
Askofu huyo wa jimbo la Mbinga ametoa agizo kwa wazazi , walezi na wasimamizi wa wanafunzi hao kuendelea kuwasaidia kwa mifano na katika matendo mema pamoja na kuwashauri katika maadili ili siku za usoni wawe wazazi bora pamoja na viongozi wa kanisa.
Awali siku ya Jumamosi waumini wa parokia ya Mpepo walifanya mapokezi ya aina yake baada ya kutumia pikipiki zaidi ya 50 katika maandamano ya kumpokea askofu John Ndimbo ambaye ni mara yake ya kwanza kufika katika parokia hiyo akiwa Askofu.
Pichani Paroko wa parokia ya Mpepo padre Lukas Kanyamballa amewapongeza waumini wa parokia hiyo kwa kujitokeza kwa wingi katika mapokezi umbali wa kilometa mbili na nusu kutoka makao
makuu ya parokia hiyo wakiwa katika pikipiki 50 huku wamevaa sare maalum.
Sherehe hizo za mapokezi ziliambana na kwaya,ngoma mbalimbali,huku wakina mama wakiwa wametandika vitenge karibu 40 ambapo wakinamama hao walimtaka Askofu huyo kupita juu ya vitenge hivyo hadi ndani ya kanisa hilo ambapo hatimaye Askofu aliwashukuru waumini hao pamoja na kuzibariki pikipiki 50 zilizotumika katika mapokezi yake.
Halmashauri ya walei ya parokia ya Mpepo pamoja na kikundi cha wazee katika parokia hiyo kwa namna ya pekee walimpongeza Askofu John Ndimbo kwa kuteuliwa kuwa Askofu mpya wa jimbo la Mbinga ambapo walimpa zawadi maalum pamoja na kumuahidi kumpatia ushirikiano wa kutosha katika kazi yake ya kichungaji.
albano.midelo@gmail.com simu o766463129


No comments:
Post a Comment