Na Albano Midelo,Songea
CHUO kikuu kishiriki cha SAUT cha Songea ambacho kimepewa jina la St.James University kinatarajia kuanza rasmi Oktoba 15 mwaka huu kikianza na wanachuo 500.
Mkuu wa chuo hicho ambaye tayari yupo Songea mwadhili mwandamizi mawasiliano wa SAUT Dk.Jeremere Araka aliwaeleza waumini wa kanisa kuu katoliki la kiaskofu la Songea kuwa maandalizi ya uanzishwaji wa chuo hicho yamekamilika ambapo hivi sasa wanasubiriwa wanachuo kuanzia masomo.
Hata hivyo alisema wanachuo watakaoishi katika mabweni ya chuo hicho ni 150 tu hivyo alitoa rai kwa wakazi wa mji wa Songea wale ambao wana nyumba za kupangisha zenye maji na umeme wafike katika ofisi ya parokia ya Songea ili kujiandikisha kwa ajili ya nyumba hizo kupangishwa na chuo kikuu hicho.
Awali chuo kikuu hicho kilitarajia kuanza kuchukua wanachuo mwezi Desemba mwaka huu.Jimbo kuu katoliki la Songea limetoa majengo matano ambayo yameazimwa na SAUT kwa ajili ya chuo kikuu hicho kitivo cha elimu.
Kwa mujibu wa Dk.Araka chuo kikuu cha St.James Songea kitaanza na kitivo cha elimu pamoja na kitivo cha tiba ambapo kanisa limetoa majengo yaliyotumika kwa ajili ya wagonjwa wa ukoma katikia kijiji cha Morogoro Peramiho.
Akizungumzia historia ya chuo kikuu cha SAUT hapa nchini,mwadhili mwandamizi mawasiliano wa SAUT Dk.Araka alibainisha kuwa SAUT ilianzishwa miaka 12 iliyopita hapa nchini ambapo hivi sasa ina matawi katika mikoa ya Dar es salaam,Iringa,Morogoro,Bukoba,Mtwara na sasa Songea.
“Kanisa katoliki barani Afrika lina vyuo vikuu 27,chuo kikuu cha SAUT ndiyo chuo kikuu kinachoongoza kwa ukubwa ,wakati kinaanza miaka 12 iliyopita kilikuwa na wanachuo 250,hivi sasa SAUT kina wanachuo zaidi ya 20,000’’,alisema.
Hata hivyo alitoa changamoto kwa wahadhili wa chuo kikuu cha SAUT kujitokeza kufundisha somo la Kiswahili katika chuo kikuu hicho kwa kuwa idadi kubwa ya wahadhili kutoka nje ya nchi ndiyo wanafundisha lugha ya Kiswahili ingawa lugha hiyo ilianzia Tanzania.
Takwimu zilizopo hivi sasa katika chuo kikuu cha SAUT, zinaonyesha kuwa kati ya wahadhili 11 wanaofundisha somo hilo katika chuo kikuu hicho,tisa wanatoka nchini Kenya na watanzania ni wawili tu na kwamba kati ya wahadhili 17 wanaofundisha somo la kiingereza 15 ni watanzania na wawili wanatoka nje ya nchi.
Kwa mawasiliano andika albano.midelo@gmail.com
No comments:
Post a Comment