Na Albano Midelo
UZINDUZI wa mchakato wa kumtangaza Sista Bernadeta Mbawala kuwa Mwenyeheri umezinduliwa rasmi leo na Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega katika kanisa kuu la kiaskofu la mjini Songea.
Uzinduzi huo umefanyika mbele ya maaskofu wote saba wa kanda ya kusini pamoja na waumini mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambako mchakato ulianza kwa kuchimba masalia ya mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta kwenye makaburi ya watawa yaliopo Abasia ya Peramiho .
Maaskofu walioshiriki kwenye uzinduzi huo ni Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega,askofu wa jimbo la Mbinga mhashamu John Ndimbo,jimbo la Tunduru Masasi mashamu Castrol Msemwa,askofu wa jimbo la Njombe mhashamu Maruma,Askofu wa jimbo la Mbeya Evaristo Chengula,Askofu wa jimbo la Lindi Bruno Ngonyani na Askofu wa jimbo la Iringa mhashamu Ngalalekumtwa.Akihubiri katika kanisa la kiaskofu la mtakatifu Mathias Kalemba mjini Songea kwenye adhimisho la misa takatifu ya uzinduzi wa mchakato wa kutangazwa kuwa mwenyeri mtumishi wa Mungu Sr.Benadeta Mbawala OSB Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Njombe mhashamu Alfred Maluma alisema kanisa limeamua kufanya mchakato huo wa kufukua masalia ya mtumishi wa Mungu ili kuimarisha maisha ya kiimani tangu Januari 24 mwaka huu kwa kufua masalia ya mwili wake.
Alisema utafiti wa kumtangaza mtumishi wa Mungu Sr.Benadeta kuwa mwenyeri unafanywa chini ya usimamizi wa wajumbe maalum wawakilishi wa Baba mtakatifu kutoka Roma na kwamba unaweza kuchukua zaidi ya miaka miwili.
“Utafiti huo ukikamilika hatimaye utamfanya Sr.Benadeta kuwa mwenyeri na hatimaye kupata wokovu na kuwa mtakatifu,nawaomba waumini katika kipindi hiki cha mchakato kuanza kutoa shida na maombi mbalimbali kupitia mtumishi wa Mungu na yeyote ambaye atakuwa amefanikiwa atoe ushuhuda wake’’,alisisitiza.
Mhashamu Maluma alisisitiza kuwa katika kipindi chote cha uhai wake mtumishi wa Mungu Sr.Benadeta alifanya jitihada za kuishi maisha ambayo yanampendeza mwenyezi Mungu na kueleza kuwa mchakato huo huwawezeshe waumini hasa wa jimbo kuu la Songea kumarika kiimani kwa ajili ya kupata wokovu.
Kwa upande wake Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea akizungumzia mchakato huo alisema kuwa hivi sasa kanisa limeanza safari ya imani na kwamba waumini wanapoyaona masalia hayo yanachochea imani.Kulingana na mhashamu Mtega kanisa katoliki limeamua kushirikisha waumini kwenye tukio hilo ili kujifunza maisha ambayo aliishi mtumishi wa Mungu na kwamba masalia hayo yatasambazwa katika maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kueneza imani ya kanisa katoliki.
Masalia ya yaliopatikana kwenye kaburi la mtumishi wangu Benadeta ni pamoja na masalia ya ya mifupa ya miguuni,kwenye vidole na fuvu la kichwa,msalaba wake ambao umeonekana kama ulivyo pamoja na msalaba na vipande saba vya rozari.
“Hili ni tukio la kwanza kutokea hapa Tanzania ,mchakato unafanyika kwa kufuata sheria,kanuni na taratibu za kanisa katoliki hivyo watanzania wote tunatakiwa kuheshimu utaratibu huu na kuchangia gharama za mchakato ambao utachukua muda mrefu’’,alisisitiza.
Sista Bernadeta aliyezaliwa Oktoba 27,1911 katika kijiji cha Likuyufusi wilayani Songea mkoani Ruvuma alifariki Novemba 29,1950 na kuzikwa katika makaburi ya Abasia ya Peramiho yaliopo kilometa 24 kutoka mjini Songea.Makao makuu ya kanisa katoliki Vatican hivi karibuni yametoa ruhusa kwa jimbo kuu katoliki la Songea kuanza mchakato wa utafiti kuhusu maisha,fadhila za uhodari,sifa ya utakatifu na nguvu za kimaombezi za Sista Bernadeta Mbawala ili aweze kutangazwa kuwa mwenyeheri na hatimaye mtakatifu.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment