Saturday, June 30, 2012

Vifo vya mapadre vyaitikisa Songea


Na Albano Midelo
KANISA  katoliki jimbo kuu la Songea limepata pigo kubwa baada ya kufariki mfululizo mapadre watatu na mabruda wawili  katika kipindi kisichozidi siku 10 .
Vifo hivyo ambavyo vimezua maswali kwa waumini vimewakuta mapadri watatu kutoka parokia za  Matogoro,Njombe na Mbinga  na mabruda wawili wote kutoka Abasia ya Hanga.
Mwezi Juni mwaka 2012 hautasahaulika na waumini wa jimbo kuu la Songea kutokana na matukio hayo ya vifo ambavyo vilianza Juni 16 ambapo Abasia ya Hanga ilimpoteza bruda Markusi Nchimbi OSB  ambaye alifia Kurasini jijini Dar es salaam kutokana na maradhi na kuzikwa Juni 20 katika Abasia ya Hanga.

Siku moja baada ya kifo cha Bruda huyo yaani Juni 17 jimbo kuu la Songea lilipata pigo jingine baada ya kifo cha padre Alfonsi Mapunda ambaye alikuwa paroko msaidizi wa parokia ya Matogoro  ambacho kilitokea katika hospitali ya KCMC mjini Moshi  na kufuatiwa na misa takatifu ya mazishi iliyofanyika  Juni 21 kwenye makaburi ya mapadre parokia ya Matogoro mjini hapa.
Vifo vya watawa viliendelea na  kuwaweka waumini katika wakati mgumu ambapo Juni 20  padre Gabriel Mwilongo aliyekuwa mkurugenzi katika ofisi ya Caritas jimbo la Njombe alifariki baada ya kusumbuliwa na shida kubwa ya shinikizo la damu ya kushuka na kuzikwa Juni 22 mwaka huu  jimboni humo.
Juni 20 ilikuwa ni siku mbaya katika jimbo kuu la Songea kwa kuwa baada ya kifo cha padre Mwilongo,siku hiyo Bruda Paschal Mkalawa OSB alifariki dunia katika hospitali ya misheni Peramiho kutokana na maradhi na kuzikwa katika makaburi ya Abasia ya Hanga Juni 22 mwaka huu.
Katika hali ya kukatisha tamaa waumini wa jimbo kuu la Songea walipata msiba mwingine wa padre John Nchimbi ambaye alikuwa ni mkuu wa chuo cha ufundi Mbinga  ambaye alipoteza maisha Juni 22 katika ajali ya gari iliyotokea katika kijiji cha Likalangilo wilayani Songea.
Marehemu padre Nchimbi alikuwa na watawa wenzake katika gari dogo wakitokea Njombe kwenye mazishi ya padre Gabriel Mwilongo hivyo majira ya saa mbili usiku walipata ajali ya gari lao kugongana na gari kubwa la mizigo na kusababisha kifo cha padre huyo ambaye amezikwa parokia ya Kigonsera.
Historia ya maisha ya marehemu padre Alfonsi Mapunda iliyotolewa na Askofu mkuu Norbert Mtega siku ya mazishi yake katika parokia ya Matogoro inaonesha kuwa alizaliwa katika kijiji cha Ndumbi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma mwaka 1944,alipokea sacramenti ya ubatizo mwaka 1945,komunyo ya kwanza 1952 na kipaimara mwaka 1954 katika kanisa la Lituhi.
Padre Mapunda alimaliza elimu ya msingi mwaka 1956 ,alijiunga na seminari ndogo ya Kigonsera mwaka 1957 kisha kumaliza kidato cha nne katika seminari ndogo ya Likonde na mwaka 1966 alijiunga na seminari kuu Peramiho kwa masomo ya falsafa na teolojia.
Historia hiyo inaonesha kuwa marehemu padre Mapunda alipata ushemasi mdogo mwaka 1971 ,alipokea daraja takatifu la upadre mwaka 1972 ambapo tangu wakati huo ametumwa sehemu mbalimbali kuwa paroko msaidizi na paroko,mlezi wa sekondari ya Kigonsera na mwaka 1979 alitumwa nchini Ujerumani kujifunza malezi ya vijana .
Tangu Novemba mwaka 1993 hadi kifo chake marehemu padre Alfonsi Mapunda alikuwa  paroko msaidizi wa parokia ya Matogoro  ambapo alijishughulisha kikamilifu kuwasaidia waumini  wa dini zote kimwili na kiroho hali iliyosababisha waumini wa dini zote kumtumia kikamilifu.
Padre Mapunda kwa takriban miaka zaidi ya 20 alikuwa na  tatizo la ugonjwa wa mifupa ya uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ambayo ametiwa hospitali ya Muhimbili,Ulaya na hatimaye KCMC .
Kwa upande wake Askofu Alfred Maluma wa jimbo katoliki la Njombe akitoa historia ya marehemu padre Gabriel Mwilongo alieleza kuwa Padre Gabriel  Mwilongo alizaliwa Igwachanya, Oktoba 19, 1962, Alipata Sakramenti ya Ubatizo Oktoba 28, 1962, alipewa Sakramenti za Komunyo ya Kwanza mwaka 1972 na Kipaimara 1972.
 Alipata elimu ya Msingi  ya kuhitimu darasa la saba mwaka 1980 katika shule ya msingi Igwachanya, Kuanzia 1981 hadi 1987 alipata elimu ya Sekondari Kidato cha kwanza hadi cha sita katika Seminari ya Mt. Kizito, Mafinga.
 Baadaye alijiunga na Seminari Kuu ya Mt. Augustino, Peramiho kwa masomo ya Falsafa (1987 - 1989) na Teolojia (1989-1993). Siku ya Juni 14, 1992, Padre Gabriel alipewa Daraja Takatifu ya Ushemasi na Mhashamu Baba Askofu Mkuu Norbert Mtega katika Kanisa Kuu la Kiaskofu Njombe.
 Julai 4, 1993  alipewa Daraja Takatifu ya Upadre na Mhashamu Baba Askofu Raymond Mwanyika katika Kanisa la Watakatifu Malaika Wakuu.
Marehemu padre Mwilongo katika uhai wake alitumwa kuwa paroko msaidizi katika parokia za Luilo, Mundindi  na kwamba  1999 hadi mwaka huu 2012 alikuwa Mkurugenzi katika Ofisi ya Caritas Jimbo la Njombe na Mwenyekiti wa Caritas Kanda ya Kusini (SHICANET – Southern Highlands Caritas Network).
Tangu mwaka 2003 Padre Gabriel aliwahi kupata shida ya shinikizo la damu ambapo Jimbo lilimsaidia kupata matibabu katika hospitali za hapa nchini na baadaye alipelekwa nchini Italia kwa uchunguzi zaidi. Baadaye alipata nafuu  na kuendelea na kazi kama kawaida.
Hata hivyo Juni 19 mwaka huu aligundulika kuwa na shida kubwa ya shinikizo la damu la kushuka na kumsababishia mauti yake Juni 20. 
albano.midelo@gmail.com















No comments:

Post a Comment