SERIKALI imetangaza matokeo ya
kidato cha pili kwa mwaka 2012, takwimu zikionesha kuwa nusu ya watahiniwa
wameshindwa kupata alama 30, huku shule kumi za mikoa ya Lindi na Mtwara zikishika
mkia.
Licha ya watahiniwa hao
kushindwa kupata alama hizo, zile za ufaulu zimeongezeka kutoka asilimia
45.40 mwaka 2011 hadi kufikia 64.55 kwa mwaka 2012.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa watahiniwa 136,946 walioshindwa kupata
alama 30 na wengine 23 walioonekana kudanganya watalazimika kukariri kidato
cha pili mwaka huu.Mulugo alisema kuwa watahiniwa
249,325 wataendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Ni vema ikaeleweka kuwa
kukariri kidato sio adhabu bali ni kutoa fursa nyingine kwa wanafunzi hao
kuweza kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu ya sekondari kidato cha
kwanza na pili kwa kiwango kizuri,” alisema.
Ufaulu wa watahiniwa
Kwa ipande wa ufaulu wa
watahiniwa Mulugo alisema kuwa watahiniwa 249,325 sawa na asilimia 64.55
walifaulu huku wasichana wakiwa 113,213 na wavulana 136,112 kiwango
kikipanda kwa asilimia 19.15.
“Watahiniwa waliofaulu kwa
kiwango cha A, B na C walikuwa 127,981 sawa na asilimia 33.13 na waliofaulu
kwa kiwango cha D ni 121,344 na alama ya juu ya ufaulu ilikuwa ni asilimia
92,” alisema.
Shule zilizofanya vizuri
Mulugo alizitaja shule za
serikali kumi zilizoongoza ni Mzumbe, Tabora wavulana, Ilboru, Kibaha,
Iyunga, Msalato, Malangali, Ifunda Ufundi, Samora Machel na Kilakala.
Kwa upande wa shule zisizo za
serikali, Mulugo alizitaja kuwa ni Kaizerege, Marian wavulana, St Francis,
Don Bosco, Bethel SABS, Marian wasichana, Don Bosco Moshi, Cannosa, St
Joseph Iterambogo na Carmel.
Shule zilizofanya vibaya
Kwa upande wa shule za serikali
zilizofanya vibaya ni Mihambwe, Dinduma, Kiromba, Marambo, Mbembaleo,
Kinjumbi, Litipu, Luagala, Miguruwe na Napacho ambazo zote ni kutoka mikoa
ya kusini – Mtwara na Lindi.
Kwa upande wa shule zisizo za
serikali ni Mfuru, Pwani, Doreta, Kigurunyembe, Ruruma, At-taaun, Jabal
hira, Mkono wa Mara, Kilepile na Kiuma.
Wanafunzi waliofanya vizuri
Mulugo aliwataja wanafunzi
walioongoza katika mtihani huo na shule wanazotoka katika mabano kuwa ni
Magreth Kakoko (St Francis) Queen Masiko (St Francis), Lukundo Manase
(Kaizerege), Frank Nyamtarila (Kaizerege), Grace Msovella (St Francis),
Harieth Makireye (St Francis) Robinnancy Mtitu (St Francis), Humrath
Lusheke (St Francis), Mukhsin Hamza (Kaizerege) na Anastazia Kabelinde
(Kaizerege).
Walimu shule za mijini
Katika hatua nyingine, Mulugo
alisema kuwa kuanzia mwaka huu hakuna mwalimu atakayepangwa shule za mjini.
Hatua hiyo imetokana na ukosefu
wa walimu ulioko vijijini na tabia ya walimu wengi kupenda kuishi mijini.
Akizungumza na viongozi wa kanda
mbalimbali kutoka Jumuia ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso), Mulugo
alisema kuwa mwalimu yeyote ambaye hataripoti katika kituo chake cha kazi
ndani ya wiki mbili atakuwa amejipotezea ajira yake mwenyewe.
Akitoa nasaha kwa viongozi hao
wa Tahliso, Mulugo aliwataka kuachana na tabia ya kuingiza siasa katika
mambo ya elimu kwani husababisha migogoro.
Mulugo alisema kuwa zinapotokea
changamoto zozote vyuoni, ni vyema wanafunzi kukubali kukaa meza moja ya
mazungumzo badala ya kusisitiza migomo na maandamano ya yasiyoleta tija
ambayo huaribu mfumo.
Naye mwenyekiti wa Tahliso, Amn
Chakushemeire, aliwataka wanafunzi wa vyuo vyote kuacha kutumika na
wanasiasa ikiwemo kuondoa chuki za itikadi za vyama vya siasa ndani ya vyuo
vyao
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment