![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu |
Na Albano
Midelo
KATIKA hali isiyokuwa
ya kawaida karibu nusu tu ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza mkoani Ruvuma mwaka huu hawajaripoti katika shule za sekondari ambazo zimefikia
179.
Mkuu wa mkoa wa
Ruvuma Said Thabiti Mwambungu amesema jumla ya wanafunzi waliochaguliwa katika
mkoa mzima kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu walikuwa ni zaidi ya 16,000
lakini hadi sasa walioripoti ni wanafunzi zaidi ya 9000 idadi ambayo ni karibu
nusu tu ya wanafunzi.
Uchunguzi ambao
umefanywa katika Halmashauri zote tano za mkoa wa Ruvuma kwa wanafunzi walioripoti shuleni baada
ya kuchaguliwa kidato cha kwanza hadi
kufikia Februari 13,2013 unaonyesha kuwa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga
ilipangiwa wanafunzi 5988 walioripoti 3606,wasioripoti 2382 sawa na asilimia
60.2.
Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo waliopangwa ni wanafunzi 2410,walioripoti 1432,wasioripoti 978 sawa
na asilimia 59.4,Songea manispaa waliopangwa 3274,walioripoti 1983 wasioripoti
1291 sawa na asilimia 61,Songea vijijini waliopangiwa 2118,waliripoti
1308,wasioripoti 810 sawa na asilimia 61.76 na Tunduru waliopangiwa ni
2788,walioripoti 1059,wasioripoti 1729 sawa na asilimia 38.
Uchunguzi huo
umebaini katika shule nyingi wanafunzi walioripoti wameshindwa hata kufikia
nusu ya wanafunzi waliopangiwa kwa mfano katika sekondari ya Chandarua iliyopo manispaa ya Songea
wanafunzi walioripoti ni 62 kati ya wanafunzi 132 waliopangiwa,shule ya
sekondari ya Barabarani iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea
wanafunzi wawili tu ndiyo wameripoti kati ya wanafunzi 23 waliopangiwa.
Kulingana na
uchunguzi huo katika shule ya sekondari Gumbiro iliyopo Halmashauri ya wilaya
ya Songea wanafunzi walioripoti ni 31 kati ya wanafunzi 101 waliopangiwa katika
shule hiyo na sekondari ya Nguluma wanafunzi walioripoti ni 54 kati ya
wanafunzi 144 waliopangiwa.
Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo katika sekondari ya Magazini
wanafunzi walioripoti ni 62 kati ya wanafunzi 145 waliopangiwa,sekondari ya
Sasawala wanafunzi walioripoti ni 62 kati ya wanafunzi 145
waliopangiwa,sekondari ya Mpunga wanafunzi waliopangiwa ni 148 lakini
walioripoti ni 48 na sendari ya Nasuli wanafunzi walioripoti ni 131 kati ya
wanafunzi 204 waliopangiwa.
Uchunguzi uliofanywa
katika Halmashauri ya wilaya ya Tunduru umebaini kuwa katika sekondari ya
Marumba wanafunzi walioripoti ni 10 tu kati ya wanafunzi 148
waliopangiwa,sekondari ya Mtutura walioripoti ni 22 kati ya wanafunzi 159
waliopangiwa,sekondari ya Namwinyu walioripoti ni 14 kati ya wanafunzi 109
waliopangiwa na sekondari ya Semeni walioripoti ni 20 kati ya 135 waliopangiwa.
“Idadi hii wanafunzi
walioripoti ndogo sana na imenishitua mimi na wenzangu hivyo inatakiwa kuchukuliwa hatua za
haraka kwa nafasi hii naagiza wazazi na
walezi ambao bado watoto wao hawajaripoti hadi kufikia Machi mosi mwaka
huu wahakikishe kuwa wanawapeleka watoto
wao shuleni hawana sababu za msingi za kutowapeleka shuleni’’,alisema mkuu wa
mkoa wa Ruvuma.
Mwambungu amewaagiza
wakuu wa wilaya zote mkoani Ruvuma,wakurugenzi,watendaji wa
vijiji,vitongoji,kata,mitaa na watendaji wengine kuanza kuwachukulia hatua
wazazi na walezi wote ambao watashindwa kuwapeleka watoto wao waliochaguliwa
katika sekondari walizopangiwa.
Baadhi ya wazazi na
walezi wakiwemo Adamu Nindi, AshuraRajabu, Stella Komba na John Hyera wamedai
kuwa moja ya sababu kubwa ambayo inachangia wazazi kushindwa kuwapeleka
wanafunzi shuleni ni michango iliyokidhiri katika shule za sekondari za kata
ambayo baadhi ya shule inafikia zaidi ya 300,000 .
“Wazazi na walezi
walio wengi ni masikini wanashindwa kumudu michango hiyo,ni kweli ada kwa mwaka
katika sekondari za kata ni shilingi 20,000 lakini michango ndiyo kikwazo kwa
wazazi wengi ambao baadhi yao wanasomesha watoto hadi watatu hivyo wanashindwa
kumudu kulipa hivyo wanafunzi wanashindwa kupelekwa shuleni’’,alisema Adamu
Nindi mzazi anayesomesha watoto wawili.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment