Monday, February 4, 2013

Uongozi mbovu unazimaliza SACCOS nchini



Baadhi ya wanachama wa SACCOS ya walimu Songea mjini
Na Albano Midelo

MKUU wa wilaya ya Songea Joseph Joseph Mkirikiti ametahadharisha kuwa  vyama vingi vya kuweka na kukopa (SACCOS) vinavunjika kutokana na uongozi mbovu ambao unashindwa kuwahudumia wanachama wake kulingana na katiba yake.

Mkirikiti alitoa tahadhari hiyo wakati anafungua mkutano mkuu wa 15 wa chama cha ushirika wa akiba na mikopo cha walimu wa manispaa ya Songea ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Songea klabu.

‘‘Uongozi mbovu ambao unashindwa kuwahudumia wanachama wake unasababisha wanachama wake kukosa raha na kupooza hali ambayo inaweza kusababisha saccos kutoweka, baadhi ya viongozi  katika saccos wanakosa maono hivyo wanafanyakazi kwa upendeleo na ubaguzi jambo ambalo ni hatari katika ushirika’’,alisisitiza.

Mwenyekiti mstaafu Saccos ya walimu wa Songea mjini Martin Challe
Mkirikiti ambaye kabla ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete  kuwa mkuu wa wilaya ya Songea alikuwa ni meneja wa saccos jijini Dar es salaam ametoa wito kwa viongozi wote wa saccos  kujipanga upya ili saccos wanazoziongoza ziwe na nguvu kubwa  kiuchumi ili kumudu ushindani dhidi ya vyombo vingine vya fedha.

‘‘Hivi sasa kuna wimbi kubwa la wanachama ambao wanajitoa uanachama katika saccos ,viongozi wa saccos hakikisheni  wanachama wote ambao wanajitoa uanachama wanaelimishwa ili wasiendelee kujitoa vinginevyo  siku moja saccos inaweza kutoweka na mimi kama mtu mwenye taaluma ya ushirika siwezi kukubali  hili liendelee kutokea ni aibu kwangu’’,alisema.


Kwa upande wake mwenyekiti wa saccos hiyo Martin Challe alizitaja changamoto ambazo zinakikabili chama hicho kuwa ni pamoja na  ushirikiano mdogo toka kwa baadhi ya wanachama, hazina kuingiza makato pungufu ya mikopo kutokana na uwezo mdogo wa mishahara ya wakopaji na wanachama 20 walijitoa katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2012 kutokana na sababu mbalimbali.

Mwenyekiti huyo ambaye ameiongoza saccos ya walimu kwa miaka 15 katika mkutano mkuu huo alijitoa kwenye  kamati ya wajumbe wa Bodi ya saccos hiyo hivyo kupoteza nafasi yake ambayo sasa imechukuliwa na mwenyekiti mpya wa saccos ya walimu Gosbert Nchimbi.

Risala iliyosomwa na makamu mwenyekiti wa saccos hiyo Julia Luoga inaonyesha kuwa saccos ina akiba za wanachama zaidi ya sh.milioni 490,mikopo iliyotolewa na wanachama ni zaidi ya  sh.milioni 357,Hisa zaidi ya milioni 36 na Amana ni zaidi ya milioni moja.

Baadhi ya wanachama wa saccos hiyo wakiwemo Ajaba Chitete,Stefano Haule na Thomas Kongo wameelezea athari za wanachama kujitoa katika saccos  kunasababisha riba na akiba  nyingi za wanachama waliojitoa kupotea na kwamba nguvu ya vyama vya akiba na mikopo ni uwingi wa wanachama.

 Wamedai kuwa Kasi ya wanachama kujitoe katika saccos ya walimu kila mwaka inakiweka chama hicho mashakani,na kwamba saccos hiyo hivi sasa  ni dhaifu sana ukilinganisha na saccos nyingine wilayani Songea ambazo zimeanzishwa karibuni ,hivyo wamewaomba viongozi waliopo wabadilike kifkra na kimtazamo ili kuikoa saccos hiyo ambayo ilikuwa mfano wa kuigwa.

‘‘Saccos hii ni yetu ni lazima tujiulize kwanini idadi kubwa ya wanachama wanajitoa ,hapa kuna tatizo kubwa,mwanachama anahitaji mkopo wa shilingi  milioni nne chama kinampa shilingi laki mbili hali ambayo inamfanya mwanachama kushindwa kutumiza malengo yake’’,alisema Chitete.

Wanachama hao pia wamedai uongozi uliopo madarakani umeshindwa kusimamia ujenzi wa  mradi wa jengo lao ambao walidai unatia mashaka kutokana na mradi huo kutumia muda mrefu na fedha nyingi  za wanachama zinaendelea kutumika bila mradi wa kitega uchumi kukamilika.

“Tunamwomba mwenyekiti wetu atoe taarifa ya ujenzi wa jengo hili kwa sababu hadi sasa hatujui fedha kiasi gani zimetumika kwenye mradi huo na bado shilingi ngapi kukamilisha ujenzi,kwanini uongozi uliamua kumtumia mkandarasi ambaye anatupa mashaka kwa kuwa ujenzi wake haukamiliki licha ya kutumia fedha nyingi na muda mrefu’’,alihoji mwanachama Ajaba Chitete.

 Mwenyekiti wa saccos hiyo aliyejitoa kwenye Bodi Martin Challe  katika mkutano mkuu wa 13 alisema  hadi  kufikia mwaka 2009  zaidi ya sh.milioni 138 zilitumika katika ujenzi wa kitega uchumi cha walimu  na kwamba kitega uchumi hicho kinatarajia kugharimu   sh. milioni 198 hadi kitakapokamilika.

Chama cha  ushirika wa akiba na mikopo cha walimu wa manispaa ya Songea chenye wanachama 375 kati yao wanaume 107 wanawake 266 na Taasisi mbili kilianzishwa rasmi Septemba 1998.

CHAMA kimoja cha ushirika wa akiba na mikopo  wilayani  Mbinga mkoani Ruvuma mwaka 2009 kilidaiwa kusambaratika kufuatia  upotevu wa shilingi milioni 400 ambazo  hazikufahamika nani wa kumkata hali iliyowasababisha wanachama kuwataka viongozi wake kuwajibika na sheria kuchukua mkondo wake.





No comments:

Post a Comment