![]() |
| Meli ya Mv.Songea imetia nanga bandari ya Mbambabay Nyasa |
Na Albano
Midelo
MVUA kubwa ambayo
imenyesha kwa saa nne mfululizo kata ya
Mbambabay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imesababisha kifo cha mtu mmoja na
kuleta uharibifu mkubwa wa mali.
Mtu aliyefariki dunia
baada ya kusombwa na maji ametambulika
kwa jina la Albat Likeli(70) aliyekuwa mkazi wa kijiji cha Ndengele kata ya
Mbambabay wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Mkuu wa wilaya ya
Nyasa Erenest Kahindi ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama
amethibitisha mvua iliyonyesha hivi karibuni imeleta madhara makubwa yakiwemo
kifo na uharibifu mkubwa wa mali za watu.
Kulingana na mkuu
huyo wa wilaya mvua hiyo imeleta madhara makubwa ya uharibifu wa mali katika
vijiji vya Ndengele,Kilosa,Lundo na Mbambabay ambayo ni makao makuu ya wilaya
ya Nyasa.
“Mvua hii
ilisababisha kujaa maji katika ujazo wa
mita moja na nusu kutoka usawa wa ardhi katika mji wa Mbambabay hali
iliyosababisha nyumba katika vijiji vilivyoathirika kujaa maji, imeharibu ekari
zaidi ya 45 za zao la muhogo katika kijiji cha Kilosa pamoja na zao la
mpunga’’,alisisitiza.
Athari nyingine
ambazo zimeletwa na mvua hizo ni ng’ombe saba wamekufa maji,madarasa mawili ya
shule za msingi yamesombwa na maji na kwamba hivi sasa hakuna mawasiliano ya
barabara kati ya makao makuu ya wilaya Mbambabay na kata za Liuli hadi Lituhi
baada ya daraja la mto Mbawa kusombwa na maji.
Mkuu wa wilaya ya
Nyasa amelipongeza jeshi la polisi katika mji wa Mbambabay kufanikiwa kuwaokoa
watoto watatu wasiojiweza waliokolewa wakiwa wanaelea juu ya maji ya mafuriko
ya mvua,hata hivyo majina ya watoto hao hayakuweza kufahamika mara moja.
Wakati huo huo
mafuriko hayo katika mji wa Mbambabay yamesababisha mamba mmoja kutoka ziwa
Nyasa kusafiri hadi katikati ya mji wa Mbambabay akifuata maji ya mafuriko
ambapo baada ya maji kukauka amebakia katikati ya dimbwi la maji lililopo
katikati ya mji huo na kuzua wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa mji huo.
Hata hivyo mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Nyasa Erenest
Kahindi amesema taratibu za kumuua mamba
huyo zinafanyika hivyo amewaomba wananchi kuwa watulivu.
Victor Komba mkazi wa
kijiji cha Liuli ametoa lawama kwa wakala wa barabara mkoa wa Ruvuma kuwa
wanachangia kila mwaka kuleta usumbufu kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa kwa
kuwa msimu wa mvua barabara zinapomoka na madaraja yamekuwa yanasombwa na maji
ya mvua.
“Madaraja yanajengwa
chini ya viwango ndiyo maana yanasombwa na maji,hata barabara zinajengwa chini
ya viwango,nani anawasimamia makandarasi wanaojenga miundombinu hii kama ina
ubora unaotakiwa, je makandarasi
wanaopewa tenda wana sifa? lawama zote tunazipeleka kwa TANROADS sasa hatuna
mawasiliano na makao makuu ya wilaya’’,alisisitiza.
Hata hivyo meneja wa
wakala wa barabara mkoa wa Ruvuma TANROADS injinia Abrahamu Kisimbo hakuweza
kupatikana mara moja kuzungumzia tuhuma dhidi ya TANROADS na lini ujenzi wa daraja la Mbawa linalounganisha
Mbambabay na miji midogo ya Liuli na Lituhi utaanza ili kumaliza kero ambayo
wakazi wa maeneo hayo wanaipata hivi sasa.
Miongoni mwa kero
ambazo wanazipata wakazi wa maeneo hayo ni gharama za usafirishaji kuongezeka
kwa kuwa mabasi na magari yanaishia katika daraja la mto Mbawa lililobomoka
hivyo inawalazimu kulipa gharama nyingine ili waweze kuendelea na safari hadi
kufika kwenye makazi yao.
Mabasi ya abiria na
magari mengine yanaishia katika eneo la daraja la Mbawa na kuanzia hapa ili
kumaliza safari hadi Liuli inakulazimu kuingia gharama nyingine zikiwemo kukodi
pikipiki na magari hali ambayo inaleta
usumbufu mkubwa kwa wananchi wasiokuwa na uwezo kutembea kwa mguu karibu
kilometa 25 hadi Liuli.
Mary Challe mkazi wa
Liuli anasema kutoka Songea hadi Liuli kabla ya kusombwa kwa daraja hilo nauli
ya mabasi ilikuwa ni sh.12,000 ambapo hivi sasa inawalazimu kutumia hadi
sh.20,000 na kwamba endapo unakuwa na mizigo mingi inakulazimu kutumia gharama
kubwa zaidi kukodi vyombo vya usafiri.
albano.Midelo@gmail.com,simu
0766463129

Asante kwa taarifa hii ya kina na natoa pole kwa waathirika. Endapo utafanyika utaratibu wa kuwapelekea michango, itakuwa vema ukituwekea hizo taarifa.
ReplyDelete