Na Albano Midelo
UNAPOSAFIRI
kutoka Songea makao makuu ya mkoa wa Ruvuma hadi kulifikia jiwe
la Pomonda lenye taswira ya binadamu lipo meta takribani 300 ndani ya
ziwa Nyasa kutoka bandari ya Liuli inakulazimu kusafiri umbali wa zaidi ya
kilometa 200.
Wajerumani
walilipa jiwe la Pomonda jina la sphinxhaven
kutokana na kuwa na vivutio vya utalii lukuki vilivyopo katika jiwe hilo
lenye taswira ya binadamu.Utalii wa
kihistoria ni aina ya kwanza ya utalii ambayo inapatikana katika jiwe hilo
ambapo tangu vita vya kwanza vya dunia mwaka 1914 hadi 1918 pamoja na vita vya
pili vya dunia mwaka 1939 hadi 1945 wakoloni wa kijerumani na wakiingereza
walitumia pango kubwa lililopo katika jiwe hilo kama sehemu ya kujificha wakati
wa mapambano.
Jiwe la Pomonda linaweza kuhifadhi watu kati
ya 200 hadi 250 kwenye kilele cha jiwe
hilo ipo taa maalum kubwa yenye rangi nyekundu ambayo ilikuwa
itatumiwa na nchi tatu za
Tanzania,Malawi na Msumbiji wakati wa wakoloni wa kijerumani,kireno na
waingereza kwa ajili ya alama ya kuongozea meli katika ziwa Nyasa ili wasiweze
kupotea wanapotaka kutia nanga kwenye bandari
ya Liuli,taa hiyo iliwawezesha kuiona bandari ya Liuli hata wakiwa katika nchi za Malawi na Msumbiji.
Kivutio
kingine cha utalii ambacho kinapatikana katika eneo la jiwe hilo ni mawe matatu
makubwa ambayo wakazi wa eneo hilo wanaamini yamepangwa na mwenyezi Mungu ,huku
mpangilio wake ukiwa ni kivutio cha ajabu utadhani yamejengwa na mafundi ujenzi
huku yakiwa yameacha njia maalum ambayo unaweza kupita kutokea upande wa pili
hali ambayo inawashangaza na kuwavutia wengi.
Jiwe la kihistoria la Pomonda pia ni sehemu
muhimu ambayo inafaa kufanya utalii wa kupiga mbizi pamoja kuwepo utalii wa kuruka toka juu ya jiwe la Pomonda hadi ziwani
umbali wa karibu mita 40 hali ambayo
inawavutia watalii wengi wa ndani na wa kutoka nje ya nchi kwenda mara kwa mara
katika jiwe hilo na kujisikie kana kwamba wapo katika nchi zao ambazo zina maeneo ambayo wameyatengeneza tofauti na eneo hilo
la jiwe la Pomonda ambalo ni la asili.
Aina 120 wa
samaki wa mapambo wanapatikana
Katika
eneo lote linalozunguka jiwe la Pomonda kuna aina zaidi ya 120 wa samaki wa mapambo
hivyo mtalii akifika katika jiwe hilo kuna eneo maalumu ambalo anaweza kufanya
utalii wa kuvua samaki hao yeye mwenyewe
pia anaweza kupika au kupikiwa ugali wa asili wa muhogo ambao ni chakula maalum kwa wakazi wa mwambao
mwa ziwa Nyasa.
Hata
hivyo uchunguzi umebaini kuwa kuna makampuni ambayo yanaendelea kuwavua samaki
hao wa mapambo katika eneo hilo kama shamba la bibi na kwenda kuwauza Ulaya na Marekani kwa bei
kubwa huku wenyeji wa kata ya Liuli na
maeneo mengine ambako samaki hao wanavuliwa wakibakia mikono mitupu pia
serikali inapoteza ushuru halali wa kodi ya samaki hao ambao inakadiriwa
wanauzwa ulaya kwa bei ya kati ya shilingi za kitanzania 150,000 hadi 200,000
kwa samaki mmoja.
Jiwe
la Pomonda ni eneo ambalo linafaa kwa
ajili ya kufanyia picnic kwa kuwa lina ukumbi mkubwa ambao umefunikwa vizuri
kwa mawe na mwenyezi Mungu tangu kuumbwa kwa dunia hata wakati wa mvua mtalii
anaweza kukaa na kuwa salama,pia kuna eneo maalum ambalo linafaa kwa kupigia
picha huku mtalii akipata upepo mwananana wa ziwa Nyasa pamoja na kufanya utalii
wa kuzunguka maeneo yote ya jiwe hilo kwa kutumia boti maalum.
Martin
Ndomba kutoka kikundi cha Ntembo Tours
Liuli anashauri watalaamu kutoka wizara ya utalii na maliasili
kutembelea katika jiwe la kihistoria la Pomonda ili kufanya utafiti zaidi na
kubaini vivutio vingine zaidi na hata umri wa jiwe hilo ambalo linafanana na
lile lililopo ziwa Viktoria.
Tamko la serikali
kuhusu vivutio vilivyoibuliwa
Serikali
mkoani Ruvuma imesema vivutio vya utalii
ambavyo vimetambuliwa katika mwambao mwa ziwa Nyasa vitaingizwa kuwa miongoni
mwa vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Ruvuma pamoja na kuviendeleza
ili hatimaye wananchi na serikali waanze kunufaika na vivutio hivyo ambavyo
vitafungua milango ya utalii katika ukanda wa kusini.
Mjumbe
katika Bodi ya utalii katika mkoa wa Ruvuma na mkuu wa mkoa wa Rukwa Injinia
Stella Manyanya anasema matangazo ya vivutio mbalimbali vya utalii katika vyombo mbalimbali vikiwemo vya ndani
ya nchi na vyombo vya kimataifa yatawezesha vivutio hivyo kufahamika kitaifa na
kimataifa hivyo idadi ya watalii kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na kuliingizia taifa mapato
makubwa.
Injinia Manyanya anasema tafiti zinaonesha
kuwa ni watanzania wachache ambao
wanaonekana kuwa na tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo
nchini,mbali ya wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo bado watu wengi
hawajaonesha kipaumbele katika sekta ya utalii.
Hata hivyo anasisitiza elimu sahihi kuhusu
utalii itawezesha kujenga mazoea ya
kutembelea vivutio hivyo na hatimaye kuifanya sekta ya utalii katika mikoa ya kusini kusimama kwa miguu
miwili huku ikipata uwezo wa kutimiza malengo yake hata bila ya kutumia nguvu
kubwa ya kujitangaza.
Ngwatura Ndunguru ni mbunge mstaafu wa jimbo
la Mbinga magharibi na afisa maliasili na utalii mstaafu anabainisha kuwa Moja
ya mambo ambayo yanaweza kuwa ni matunda ya sekta ya utalii katika ukanda wa
kusini ni uboreshaji wa miundombinu hususani ya mawasiliano ya
barabara,usafiri, hoteli za kisasa ili kukidhi matakwa ya wageni wanaofika
kusini kwa shughuli za kitalii.
Mataifa
mengi duniani hivi sasa yanatoka kwenye utalii wa kutegemea mbuga za
wanyamapori na kuingia kwenye utalii wa mambo ya kale,ngoma,hadithi na simulizi
za kale hivyo fursa za utalii katika mkoa wa Ruvuma na ukanda wa kusini ni
nyingi na zikiibuliwa,zikiendelezwa na kutangazwa ukanda wa kusini unaweza
kupiga hatua kubwa katika utalii.
Utalii ni sekta au eneo la kiuchumi
linalokua kwa haraka duniani. Nchi
nyingi duniani zinaipa umuhimu mkubwa sana sekta ya utalii kwa kuzingatia
kwamba ni eneo jingine muhimu la kukuza uchumi wa taifa na watu wake.
Hivyo sekta ya utalii na shughuli zake
zikiwa zimewekewa mipango mizuri na inayotekelezeka,na kushirikisha wadau
husika, inatarajiwa kuchochea ukuaji wa kiuchumi kwenye nchi na eneo husika
kama ilivyo kwa mikoa ya kanda ya kaskazini hapa nchini.
albano.midelo@gmail.com,simu
0784765917 au 0766463129

No comments:
Post a Comment