MTANDAO wa Wanawake na Katiba
umeainisha mambo mbalimbali ambayo ni muhimu yazingatiwe katika Katiba Mpya.
Maeneo hayo yameainishwa na kutolewa ufafanuzi kama ifuatavyo;
Haki za wanawake kwenye Katiba Mpya zipewe kipaumbele stahiki: Mtandao wa Wanawake unasisitiza
haki za msingi za wanawake ziendelee kubainishwa zaidi
katika Tamko la Msingi wa Haki za Binadamu (Bill of Rights), ili wanawake
waendelee kupata haki sawa za uraia, siasa, uchumi na ustawi wa jamii
zinazolindwa kikatiba.Haki za wanawake kwenye Katiba Mpya zipewe kipaumbele stahiki: Mtandao wa Wanawake unasisitiza
Katiba Mpya iendelee kubatilisha sheria zote za ubaguzi wa jinsia, ikiwa ni pamoja na kubagua na kudhalilisha wanawake na watoto wa kike chini ya mfumo dume unaotawala jamii zetu. Hiki ni kilio cha wanawake kwa miaka nenda rudi hivyo kifikie ukomo sasa.
Aidha, Katiba Mpya iendeleze misingi inayolinda utu wa mwanamke ikiwa ni pamoja na kulinda wanawake dhidi ya vitendo vya kikatili wa kijinsia ukiwamo ubakaji ndani na nje ya ndoa, unyanyasaji wa kisaikolojia, ukeketaji wa watoto wa kike, ndoa za utotoni, na vitendo vingine vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Serikali iwajibishwe na Katiba Mpya katika kutekeleza mikataba yote ya kimataifa iliyoridhia kuhusu haki za wanawake. Kadhalika, sheria za nchi zitambue mikataba hii ili kuepusha ucheleweshaji wa kutafsiri au kuruhusu tafsiri zenye kukinzana na misingi ya mikataba husika.
Haki sawa katika nafasi za uongozi zizingatiwe: Katiba mpya ibainishe misingi itakayozuia kuhodhiwa kwa madaraka katika mihimili mikuu ya utawala kwa jinsi moja, kwa mfano; Taasisi ya Urais, Makamu, Waziri Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Spika na Naibu Spika.
Pia wakuu wa mikoa, Manispaa, Halmashauri na wilaya vyama vya kisiasa, bodi za mashirika ya umma na viongozi mpaka ngazi za chini kabisa. Kwa mantiki hiyo, uwepo uwiano wa kijinsi (50/50%) na ujengwe katika ngazi zote za uongozi na maamuzi na sio kwenye nyanja ya siasa tu.
Haki ya kufikia, kutumia, kunufaika na kumiliki rasilimali ya nchi: Kwa kuzingatia kwamba rasilimali ya nchi yetu ni ya kila Mtanzania (Me na Ke), Katiba Mpya iweke bayana kwamba wanawake wa Kitanzania wana haki sawa za kufikia, kutumia, kumiliki na kufaidika na rasilimali za nchi yetu ikiwa ni pamoja na ardhi, madini na vitu vyote vilivyoko nchi kavu na majini.
Haki ya Uzazi Salama ni eneo lingine muhimu: Katiba mpya ihakikishe kuwa afya ya uzazi salama kwa kila mwanamke inalindwa kikatiba. Serikali iwajibishwe kuwekeza katika afya ya uzazi kwa ujumla, pamoja na uzazi wa mpango ili kumpunguzia mwanamke mzigo mkubwa anaobeba katika kuendeleza kizazi cha Tanzania. Katika kutimiza jukumu la uzazi katika jamii, wanawake hukumbana na changamoto nyingi zinazotishia haki yao ya msingi ya kuishi.
Katiba ibainishe haki sawa kwa wanawake za kufikiana kufaidi huduma za msingi ikiwa ni pamoja na afya, elimu, maji na huduma za hifadhi ya jamii.
Haki za wanawake wenye ulemavu ziwekwe bayana. Katiba Mpya iainishe vile vile haki za wanawake wenye ulemavu kwa kutambua kwamba kundi hili huathirika maradufu na mfumo dume.
Katiba mpya iiwajibishe serikali kuchukua hatua za kisera na kisheria ili kulinda wanawake wenye ulemavu dhidi ya vitendo vya ukatili, na kufikia huduma za msingi za kukimu maisha kama vile huduma za afya, elimu, hifadhi ya jamii, na fursa sawa katika ajira.
Haki za watoto wa kike: Katiba iunde chombo maalumu kitakachowajibisha serikali na taasisi mbalimbali nchini katika kutekeleza haki za wanawake katika maeneo yote ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini.
Aidha, uundwaji wa Mahakama ya Kifamilia uainishwe bayana ndani ya Katiba mpya, jukumu lake likiwa ni kuendesha na kuratibu kesi zote zenye mashauri ya msingi wa kifamilia. Mahakama hii itasaidia kuleta ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa haki za mwanafamilia, hasa wale wanyonge wakiwamo wanawake.
ANGALIZO: Takwimu kuhusu Ukatili wa kijinsia nchini zinaonyesha kuwa; Ukatili wa kingono/kupigwa kwa wanawake waliowahi kuolewa kati ya umri wa miaka 15- 49 ambao wamepitia ukatili mbalimbali uliofanywa na wanaume/wapenzi ni kama ifuatavyo; ukatili wa kihisia asilimia kwenye mabano (36), kupigwa (39), kingono (17), kupigwa na kingono (44).
Takwimu hizo zinaainisha kuwa asilimia 44 ya wanawake waliowahi kuolewa wamepitia ukatili wa kingono kutoka kwa waume/wapenzi wao na asilimia 37 ya walioolewa wamepitia ukatili wa aina hiyo kwa miezi 12 iliyopita.
Ukatili wa kingono ndani ya ndoa, asilimia ya wanawake wote kati ya miaka 15-49, wamepitia ukatili huo pamoja na wale waliolazimishwa bila matakwa yao. Kwa ambao hawajawahi kuolewa ni asilimia 11, walioolewa na kuishi pamoja asilimia 22 na walioachana au kutengana, wajane ni asilimia 34.
Asilimia 20 ya wanawake waliowahi kupitia ukatili wa kingono mara kwa mara hufanyiwa na wapenzi wao au waliowahi kuwa wapenzi wao. Mmoja kati ya wanawake 10 Tanzania waliopitia katika uhusiano wa kimapenzi, penzi la kwanza lilikuwa la kulazimishwa.
Kiwango cha ndoa kinachodhibitiwa na wanaume, asilimia ya wanawake waliowahi kuolewa kati ya umri wa miaka 15 hadi 49 ambao waume/ wapenzi wanavyodhibiti na aina ya udhibiti huu ni kama ifuatavyo;
Wivu au hasira pale mwanamke anapoongea na mwanaume mwingine (asilimia 32), kutoruhusiwa kukutana na wanawake wenzake (asilimia 2), kujaribu kumzuia kukutana na familia yake asilimia 18, mwanaume anataka kujua wakati wote mkewe yuko wapi asilimia 49, mume hamuamini kwa pesa yoyote (asilimia 16), tabia tatu au zaidi ya zilizotajwa ni asilimia 35 huku asilimia 23 haonyeshi tabia yoyote kati ya zilizotajwa asilimia 35. Hata hivyo, asilimia 35 ya wanawake waliowahi kuolewa wameeleza kuwa wanaume zao/wapenzi wana tabia tatu au zaidi ya hizo zilizotajwa hapo juu.
*Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania unahusisha mashirika yanayotetea haki za Wanawake na Binadamu yafuatayo:
Equality for Growth( EFG), Haki za Wanawake (HAWA), Kilimanjaro Women Information Exchange Consultancy Organization (KWIECO), Chama cha wanasheria Wanawake (TAWLA), Shirikisho la Vyama vya Walemavu (SHIVYAWATA), Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Tanzania Women Crass Party ((TWCP-ULINGO), Trade Union Congress of Tanzania (TUCTA), Tumaini Women Development Association (TUWODEA), Women Fund Tanzania (WFT), Women Legal Act Centre (WILAC), Zanzibar Gender Coalition (ZGC), KIVULINI, Wote Sawa, Jitolee Kishapu, ADC Foundation, Saidia Wazee Tanzania (SAWATA), Women in Law and Development in Africa (wildaf), Zanzibar Female Lawyers Assocition (FAFELA). Tanzania Women Miners Association (TAWOMA), Jukwaa la Katiba na wanawake Wanaharakati binafsi.
CHANZO;GAZETI LA NIPASHE

No comments:
Post a Comment