Thursday, January 27, 2011

Mnara wa mashujaa 67 wa vita vya Majmaji wakamilika Songea

 


Mnara wa kisasa wa mashujaa wa vita vya Majimaji uliopo mjini Songea
Na Albano Midelo.

MAKUMBUSHO ya Taifa chini ya wizara ya maliasili na utalii imeamua kujenga mnara wa kumbukumbu ya mashujaa 67 walionyongwa kikatili katika eneo la Songea klabu utakaogharimu zaidi ya shilingi milioni 16.

Mkurungezi na mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa ya Majimaji ya Songea Philipo Maligisu alisema jana kuwa ujenzi wa mnara huo unatarajia kumalizika mwanzoni mwa mwezi ujao na kwamba unatarajia kufunguliwa rasmi na waziri mkuu Mizengo Pinda siku ya mashujaa wa vita vya Majimaji Februari 27 kama sehemu muhimu ya kumbukumbu ya  mashujaa hao muhimu katika historia ya ukombozi wan chi yetu.

Mnara huo ambao jiwe lake la msingi liliwekwa mwaka jana na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma unatarajiwa kufunguliwa rasmi Februari 27 mwaka huu na waziri mkuu Mizengo Pinda siku ambayo ni siku ya mashujaa wa vita vya Majimaji.

“Baadhi ya vitu ambavyo vitajengwa na kuwekwa kwenye mnara huo ni  silaha za jadi za kabila ya wangoni pamoja na kuonyesha majina 67 ya watu walionyongwa kinyama katika vita vya Majimaji,Tunataka kulibadili eneo hili ambalo mashujaa walinyongwa kuwa  kuwa eneo maalum ambalo watu mbalimbali wakitembelea watajifunza historia pamoja na kumbukumbu muhimu ambayo walinyongwa mashujaa wa Majimaji,eneo hili litakuwa la kuvutia,watu wanaweza kukaa na kubadilishana mawazo”,alisisitiza Maligisu.


Alibainisha kuwa baada ya vita vya Majimaji viongozi na askari walioshiriki katika vita hivyo walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa ambapo Februari 27,mwaka 1907 ilikuwa ni siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa mkoa wa Ruvuma baada ya watu zaidi ya 60 kunyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita vya majimaji.

Mashujaa hao walinyongewa nyuma ya eneo ambalo hivi sasa linajulikana kwa jina la Songea Club,baada ya kunyongwa miili ya mashujaa hao ilizikwa katika kaburi la halaiki,lililoandaliwa na wafungwa kwa muda wa miezi miwili,siku ya tatu baadaye chifu wa kabila la wangoni  Songea Mbano alinyongwa na kuzikwa katika kaburi  la pekee yake ambapo inaaminika alizikwa kiwiliwili baada ya kichwa chake kukatwa na wajerumani na kukipeleka.

Hata hivyo mhifadhi kiongozi huyo wa makumbussho ya Taifa alisisitiza kuwa eneo la Mahenge walilozikwa mashujaa hao ni muhimu katika historia ya mtanzania ndiyo maana mara baada ya uhuru mwaka 1961 baadhi ya wazee walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hao pamoja na kuanza kufanya maombi ya kimila katika eneo hilo walilonyongewa mashujaa hao.

 Kwa mujibu wa Maligisu,Makumbusho ya vita vya majimaji kama yalivyo makumbusho mengine ya kihistoria ni chombo cha kuelimisha jamii kuhusu mambo muhimu ya kujivunia ya Taifa,makumbusho ya majimaji ni historia nzuri na kiburudisho pamoja na kuwa chombo cha kujenga hamasa ya kujiamini kama Taifa na kuimarisha umoja,kuheshimiana na kuishi kwa amani.
 Baruapepe amidelo@yahoo.com
Tovuti;www.maendeleonivita.blogspot.com

No comments:

Post a Comment