Wednesday, January 26, 2011

Hospitali ya serikali ya mkoa wa Ruvuma lawamani

 
Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela
 Na Albano Midelo

LAWAMA zinaandama hospitali ya serikali ya mkoa wa Ruvuma. Kuna wanaosema wauguzi, hasa wa usiku hawana lugha nzuri. Kuna wanaodai kuwa madaktari na manesi hawapatikani usiku, hasa baada ya saa sita.

Hii ni hospitali ambayo ni tegemeo la wakazi wa wilaya za Songea, Natumbo, Tunduru pamoja na wagonjwa ambao  wanapata rufaa kutoka hospitali, vituo vya afya na zahanati nyingine mkoani.

Mwandishi wa habari hizi alibeba malalamiko haya kutoka midomoni mwa wananchi na kuyabwaga kwa Mganga Mkuu wa  mkoa wa Ruvuma , Dk. Daniel Malecela.

Dk. Malecela haraka anakiri kusikia malalamiko hayo kuwa yapo bali anasema miaka ya nyuma ndipo yalikuwa mengi lakini uongozi wa hospitali ulichukua hatua za kukabiliana na watumishi walokuwa wakikiuka maadili ya kazi.

“Huko nyuma tulikuwa na tatizo kubwa kwa baadhi ya watumishi kukiuka maadili ya kazi; hivyo tulichokifanya ni  wauguzi kupiga kura na kutambua nani wanafanya mchezo huo mchafu unaowapaka matope watumishi wote,” Dk. Malecela anaeleza.

Anasema walichofanya ni kuwawabadilisha wauguzi wote watuhumiwa kutoka zamu zamu za usiku na kuwapangia zamu za mchana. Anasema, “… hali hiyo ilileta ufanisi na malalamiko ya wananchi yalipungua.”

“Sasa nadhani tabia hiyo inajirudia kwa kiasi kikubwa. Itakuwa inachangiwa na  baadhi ya watumishi hawa wapya. Unajua kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi katika idara ya afya, serikali imepeleka vijana wengi kusomea fani hii na wengine wameingia ‘bora kupata ajira’ kwa kuwa katika sekta ya afya na elimu ni rahisi kupata ajira,” anafafanua.

Dk. Malecela, huku akimwangalia machoni mwandishi na kutoa macho kama anayekazia akisemacho anasema, “…tutafanya uchunguzi na kuwatoa zamu za usikuwale wote wanaosababisha malalamiko; tutawapanga mchana ili iwe rahisi kuwasimamia,”amesisitiza.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya wauguzi na madaktari wanaofanya kazi katika hopsitali hiyo wanakiuka maadili ya kazi yao kwa makusudi kwa kutohudumia wagonjwa, hasa wanaofika kutibiwa majira ya usiku; na kwamba wale ambao wanatibiwa inadaiwa huwa inawalazimu kutoa “kitu kidogo.”

Wanaoathirika zaidi katika mazingira haya ni waliopata ajali, wajawazito pamoja na watoto. Kusubiri daktari asiyepatikana ndani ya hospitali au aliyepo lakini hatoi huduma, kunaweza kugharimu maisha ya watu, hasa waliopata ajali, wajawazito na watoto wenye magonjwa ya ghafla.

“Ukifika usiku hospitali ya mkoa utakuta mlango wa daktari umefungwa; daktari wa kuwapokea hayupo; na hata akifika atachukua muda mrefu kabla ya kukuhudumia. Hapa kama mgonjwa atakuwa amezidiwa, basi aweza kupoteza maisha,” ameeleza John Tembo, mkazi wa Mfaranyaki, mjini Songea.

Jacob Komba, mkazi mwingine wa mjini Songea, anasema ukifika kutibiwa wakati wa usiku, “utagundua jinsi baadhi ya lugha za wauguzi zisizo nzuri.” Amedai kuwa wauguzi wanawakemea wagonjwa huku baadhi yao wakidai kuwa wanafanya kazi hiyo “kwa kujitolea zaidi kwa kuwa kazi ya uuguzi ni ya kujitolea; haina masalahi hivyo wasiwafundishe kazi; kama hawaridhiki waende kutibiwa kokote kule.”

Hata hivyo, katika mahojiano na baadhi ya wananchi waliotibiwa katika hospitali hii, imegundulika kuwa siyo wote wanaopataka karaha. Uchunguzi umebaini kuwa baadhi wamepata matibabu vizuri, jambo ambalo linafanya wengine kuamini kuwa inawezekana kuna mazingira ya Kutoa chochoe.”

Aidha, baadhi ya wananchi wanaendelea kulalamika kuwa kila wanapoandikiwa dawa na daktari, huambiwa kuwa hazipo hospitalini bali zinapatikana katika maduka nje ya hospitali. Hutajiwa hata majina ya maduka husika.

Hili limezua shaka kwamba wenye maduka ni madaktari wenyewe ingawa hakika hakuna sheria inayowazuia kuwa na miradi ya aina hiyo. Madai ni kwamba madaktari huenda wanapeleka huko dawa ambazo zilipangwa kwenda hospitalini.

Muhidin Amri mwandishi wa habari wa gazeti la Majira mkoa wa Ruvuma ambaye hivi karibuni mtoto wake wa mwaka mmoja aliungua  vibaya sehemu ya tumbo na kumpeleka mtoto wake hospitali ya mkoa,amekiri huduma ni mbovu kwani licha ya mtoto huyo kuhudumiwa katika daraja la kwanza kwa gharama kubwa hali ya mtoto iliendelea kuwa mbaya ilimlazimu kununua madawa toka jijini Dar es salaam.

“ Wauguzi walikuwa wakifika asubuhi wanamtibu kwa dawa ambazo hazifai kidonda kilikuwa kinaendelea,dawa nilizonunua Dar es salaam ndizo ambazo zimemsadia mtoto wangu wauguzi katika hospitali ya mkoa huduma zao haziridhishi,hebu fikiria mimi ni mwandishi ambaye angalau nafahamika je mwananchi anayetoka kijijini hali ya huduma inakuwaje ni hatari sana,serikali inatakiwa kufuatilia utendaji kazi wa baadhi ya wauguzi na madaktari katika hospitali hii”,anasisitiza.

Hata hivyo mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela  anasema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uhaba mkubwa wa madawa kutokana na  kukosa fedha za kununulia madawa hayo hali ambayo inasababisha wananchi kuambiwa wakanunue madawa kwenye maduka ya dawa muhimu.

Catherene Komba  mkazi wa  kata ya Ruvuma mjini hapa analalamikia  uangalizi wa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali ya mkoa kwamba umetofautiana sana.

Analalamika kuwa wagonjwa waliolazwa wodi daraja la kwanza na la pili wanapewa uangalizi na huduma bora zaidi ikilinganishwa na wagonjwa wanaolazwa katika wodi daraja la tatu.

Alipoelezwa kuwa kuwa huo ni mfumo wa miaka mingi na wale wa daraja la juu hulipa zaidi, aling’ang’ania kuwa hospitali ya serikali haipaswi kuangalia kipato cha mtu bali uhai wake.

Komba amelaani kitendo cha akinamama wajawazito kuamriwa kununua mipira ya kujifungulia badala ya mipira hiyo pamoja na vifaa vingine kupatikana katika hospitali ya mkoa; kutokana na ukweli kuwa sera ya afya inasema huduma ya afya kwa mama mjamzito itatolewa bure.

“Serikali inanunua magari ya kifahari, inagharamia fedha nyingi kwa mambo mbalimbali; hivi kweli serikali inashindwa kununua vifaa vya kujifungulia mama mjamzito ambaye anamzaa rais wa kesho” Mbona vitu vingine ni vya aibu kufanywa na serikali yetu?” anauliza.

Baadhi ya wanafunzi wanasoma katika shule ya sekondari ya wasichana Songea ambao wanaitegemea hospitali ya mkoa kwa matibabu wanadai kuwa huduma za hospitali hiyo wakati wa usiku sio nzuri ukilinganisha na mchana.

Wanadai kuwa baadhi ya wauguzi wanadharau wanafunzi kwa madai kuwa “wanasingizia kuugua ili wakutane na  wanaume wapenzi wao.”

Baadhi ya wauguzi wa wodi ya wazazi katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma wanasema wanafanyakazi zao kwa mujibu wa maadili ya kazi zao ingawa wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo idadi kubwa ya wanaofika kujifungua. Wanasema hali hii inasababisha washindwe  kutoa huduma bora kutokana na uchache wa watumishi.

0766463129
www.maendeleonivita.blogspot.com



No comments:

Post a Comment