Wednesday, January 26, 2011

Milango ya utalii mwambao mwa ziwa Nyasa sasa imefunguka

Fukwe nzuri za kuvutia katika eneo la Tumbi kata ya Kihagara ndani ya ziwa Nyasa mkoani Ruvuma
 
Na Albano Midelo.

MILANGO ya utalii katika ukanda wa kusini imeanza kufunguka baada ya kugundulika samaki  katika ziwa Nyasa mwenye umbo dogo anayeitwa ngoko mwenye maajabu mengi ikiwemo uwezo wa kukausha mti  mkubwa kwa siku saba hadi 14 kwa kutumia mwiba wake mgumu na wenye sumu na ncha kali.

 Wakizungumza na  mwandishi wa habari hizi  wavuvi wa samaki katika ziwa Nyasa pamoja na wananchi wa kawaida ambao wanamfahamu samaki walisema kuwa  samaki huyo ana maajabu mengi endapo yatatangazwa yanaweza kuvutia watalii wengi kumtazama samaki huyo pamoja na kumfanyia utafiti zaidi.

Martin Ndomba mkazi wa kijiji cha Kihagara alisema katika kijiji hicho kuna vivutio lukuki na vya kipekee vya utalii kikiwemo cha aina ya samaki wa pekee mwenye umbo dogo anayeitwa ngogo lakini ni mfalme  katika ziwa Nyasa kutokana na kuwa na uwezo wa kuuwa samaki wakubwa kama bogobogo ambaye ana mwili mkubwa sawa na binadamu mtu mzima.

“Sisi wavuvi tunamwita samaki huyu mfalme katika ziwa Nyasa kwa kuwa hakuna samaki anayeweza kupambana naye wote wanamkimbia,samaki huyu ana maajabu kwa kuwa samaki mkubwa akifika jirani na samaki huyo kwa lengo la kummeza,samaki ngogo anaficha miba zake ambazo zipo pande zote baada ya kumezwa akiwa tumboni samaki huyo hukunjua miba zake ambazo zina sumu kali  na kumsababishia samaki mkubwa kuanza kudhooofika na hatimaye  kufa hivyo yeye baada ya samaki huyo kuoza anatoka ingawa anakuwa amekonda na kuendelea na maisha kama kawaida na kuendelea kupambana na samaki wengine”,alisisitiza  Ndomba mvuvi mzoefu ziwa Nyasa.

Maajabu mengine ya samaki ngogo kwa mujibu  mvuvi Felician Komba, endapo samaki huyo atashikwa vibaya wakati anavuliwa na kumchoma mvuvi kwenye mguu au mkono wake anaweza kusababisha mguu au mkono uliochomwa kwa mwiba wake wenye sumu kali kukatwa  hali ambayo inawafanya wavuvi kuwa waangalifu wanapokuwa ziwani endapo wanakutana na samaki huyo.

Uchunguzi mwingine ambao umethibitishwa na baadhi ya wavuvi na wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa umebaini kuwa samaki huyo anatumiwa kwa ajili ya kukausha miti mikubwa kwa ajili ya kupata kuni kama anavyoeleza Martini Ndomba “Tangu enzi za zamani wazee wetu walikuwa wanamchukua samaki ngogo akiwa hai na kwenda kuchomeka mwiba wake kwenye mti mkubwa mbichi ,wakati samaki huyo anachomekwa mwimba wake uliochongoka,mnene na mgumu kwenye mti mbichi anatoa sauti ambayo ni ishara kuwa sumu yake imeingia kwenye mti ambao baada ya siku saba hadi 14 unakauka kabisa”

Samaki aina ya ngogo mwenye maajabu lukuki ziwa Nyasa
 Hata hivyo inadaiwa kuwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa katika mila zao tangu zamani wanakataza mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano kula samaki aina ngogo kwa madai kuwa analeta ugonjwa wa degedege  yaani malaria kali,hata hivyo samaki huyo mwenye radha ya kipekee wakazi wa mwambao wanamtumia zaidi kula wakati wanakunywa pombe za kienyeji badala ya kutumika kama kitoweo kwa ajili ua ugali au wali,pia samaki huyo ni moja kati  ya aina 120 wa  samaki wa mapambo wanaopatikana ziwa Nyasa.
Baruapepe amidelo@yahoo.com
tovuti;www.maendeleonivita.blogspot.com

No comments:

Post a Comment