Bodi ya utalii Tanzania ilivyopania kuvitangaza vivutio vya utalii kupitia ligi kuu ya Uingereza
Na Albano Midelo.
Wizara ya maliasili na utalii inafanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa vivutio hivyo vinatangazwa ndani na nje ya nchi ili vifahamike na kusababisha wageni wengi kuvitembelea na nchi kupata pato kubwa kutokana na ada ambazo wanalipia wageni hao wanapotembelea vivutio hivyo.
Ni ukweli usiopingika kuwa bado vivutio vingi vilivyopo nchini havijatangazwa ipasavyo hasa na vyombo vya habari vya kimataifa kutokana na gharama kubwa za matangazo na kusababisha vivutio hivyo visifahamike kimataifa.
Kutokana na hali hiyo Bodi ya utalii Tanzania yaani TTB imeanza kutumia mbinu mbalimbali za kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi kadiri ya ya uwezo wa kifedha unapopatikana ili kuhakikisha kuwa vivutio vyote vinafahamika vizuri ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya utalii Tanzania Dk.Aloyce Nzuki anasema TTB imeamua kutumia michezo ya ligi kuu ya mpira wa miguu ya Uingereza yaani English Premier League kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kutokana na ligi hiyo kutazamwa na mamilioni ya watu ulimwenguni kote.
“Wizara ya maliasili na utalii kupitia baadhi ya mashirika yake hususan TANAPA na NGORONGORO kwa uratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania TTB tumenunua nafasi ya kutangaza kwenye viwanja vya nyumbani vya timu sita zilizopo kwenye ligi kuu ya Uingereza iliyoanza Agosti 14 2010 na itakamilika Mei 22,2011”,anasema.
Anabainisha kuwa jumla ya shilingi milioni 800 zitatumika kutangaza matangazo ya vivutio vya utalii vya Tanzania katika ligi kuu ya Uingereza kwa miezi tisa na kwamba Tanzania inakuwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kuweka matangazo yake kwenye viwanja vya mpira katika ligi kuu ya Uingereza.
Kwa mujibu wa Nzuki viwanja ambavyo Tanzania imeweka matangazo yake ya vivutio vya utalii katika ligi hiyo ya Uingereza ni pamoja na na Ewood wa timu ya Blackburn Rovers wenye uwezo wa kuchukua watu 31,367, uwanja wa St James park wa timu ya Newcastle united wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 52,387.
Viwanja vingine ni cha Britania cha timu ya Stoke city chenye uwezo wa kuchukua watazamaji 28,383,uwanja wa timu ya Sunderland unaitwa stadium of Light wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 49,000,uwanja wa timu ya West Bromwich Albion wenye uwezo wa kuchukua watu 28,008 na uwanja wa timu ya Wolverhamton Wanderer unaoitwa Molineux stadium wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 29,303.
“Kama ambavyo wengine mnafahamu zipo timu 20 zinazocheza ligi hii kuu ya Uingereza na kila timu katika ligi hiyo inacheza na nyingine yaani nyumbani na ugenini,sisi tumeweka matangazo yetu kwenye viwanja hivyo sita vya nyumbani kwa maana hiyo tutakuwa na jumla ya mechi 114 tangu ligi hiyo ilipoanza Agosti 14 mwaka huu hadi Mei 22 mwaka 2011 ligi hiyo itakapomalizika”,anasema.
Hata hivyo Dk.Nzuki anabainisha kuwa matangazo hayo ni ya teknolojia ya digital video yaani (LED Perimeter Advertising) ambayo yatakuwa yanaonekana kwenye kuta za matangazo kwa sekunde 30 kila yanaporushwa ambapo katika kila mechi tangazo hilo litarushwa sio chini ya mara sita.
Kulingana na mkurugenzi huyo wa TTB kwa sekunde 30 yameandaliwa matangazo mafupi yenye kuonesha vivutio maarufu vya utalii vilivyopo hapa nchini na kwamba kila mwisho wa tangazo kuna tovuti ambayo ni rahisi kuikumbuka kwa mtu yeyote ambaye ataona tangazo hilo ndani ya uwanja au kuona kupitia luninga.
“Vivutio maarufu ambavyo vitaendelea kuoneshwa katika matangazo hayo ni kampeni za kupanda mlima Kilimanjaro,utalii katika mbuga za wanyama ambapo tukio maarufu la the greatest animal migration ambalo hutokea ndani ya hifadhi ya Serengeti litaonekana,pia tutaonesha utalii wa fukwe ambapo fukwe za Zanzibar zitaonekana”,anasisitiza.
Anasisitiza kuwa ndani ya sekunde 30 watazamaji wataweza kuona vitu vyenye mvuto wa haraka ambapo mwisho wa kila tangazo kuna tovuti ambayo ni http://www.visit-tanzania.go.tz/ ambapo kuna taarifa mbalimbali kuhusu utalii wa Tanzania kwa ujumla.
TTB pamoja na wadau wa utalii nchini wameamua kutangaza vivutio vya utalii katika ligi kuu ya Uingereza, kutokana na mpira wa miguu kuwa ndiyo mchezo unaopendwa kupita michezo mingine yote duniani na ligi kuu ya Uingereza ni miongoni mwa ligi bora duniani.
Takwimu za utafiti zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni mbili duniani wanatazama ligi kuu ya Uingereza kutokana na hali hiyo TTB inategemea watu zaidi ya milioni mbili wataona matangazo ya vivutio vya utalii wa Tanzania katika viwanja hivyo kwa miezi tisa ijayo na watu wengine zaidi ya milioni 100 watayaona kupitia kwenye luninga na mtandao kote duniani.
Hata hiyo anasema katika kipindi cha wiki mbili toka ligi kuu ya Uingereza ianze ,jumla ya watazamaji 186,522 wameweza kuhudhuria mechi sita zilizochezwa nyumbani na kufanikiwa kuyaona matangazo hayo ya vivutio vya utalii vya Tanzania na kwamba TTB inafuatilia kwa karibu kuweza kupata taarifa ya matangazo hayo(impact).
Moja ya njia ambazo TTB inatarajia kufuatilia ili kupata taarifa za matangazo hayo ni pamoja na kupita kwenye tovuti ya TTB ili kujua idadi ya watu wanagapi wanatembelea tovuti hiyo kabla ya ligi kuanza na baada ya ligi hiyo kumalizika hapo mwezi Mei mwakani.
“Pia tutashirikiana na wadau mahsusi kufuatilia na kutathimini idadi ya wageni au watalii walikuja nchini Tanzania kutoka nje ya nchi baada ya kuona matangazo yetu kwenye ligi kuu ya Uingereza,TTB itaendelea na mikakati mingine ya kutangaza utalii nchini Uingereza.
Baruapepe amidelo@yahoo.com,simu
http://www.maendeleo/ ni vita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment