Na Albano Midelo.
IDARA ya mambo ya kale kwa kushirikiana na idara ya makumbusho ya Taifa chini ya wizara ya maliasili na utalii zina jukumu kubwa la la kuhakikisha kuwa malikale zilizopo nchini zinahifadhi,kulindwa na kuendelezwa.
Idara hizo pia zinatakiwa kuendeleza vivutio vyote ambavyo ni vya kihistoria na kiutamaduni ambavyo vimetambuliwa kwa kuwa ni urithi wa Taifa katika kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii katika mambo ya kale vingi vikiwa katika maeneo ya vijijini,mfano wa vivutio hivyo ni nyayo za binadamu wa kale ambazo zimegundulika sehemu mbalimbali nchini,nyota au vimondo kutoka anga za mbali ambavyo vimeanguka katika sehemu mbalimbali nchini,magofu ya kale,mawe ya ajabu,nyumba za makumbusho pamoja na vivutio vingine.
Uchunguzi umebaini kuwa vivutio vya utalii wa mambo ya kale ambavyo vimetambuliwa,vimetelekezwa kwa kutoendelezwa jambo ambalo linahatarisha uwepo wa vivutio hivyo adimu na ambavyo endapo vingeendelezwa vingeweza kuliingizia taifa fedha za kigeni na kuwaendeleza kiuchumi wananchi wa eneo husika.
Moja ya vivutio vya utalii vya mambo ya kale ambavyo vimesahaulika ni nyota kubwa ambayo imeanguka mwaka 1840 katika kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi mkoani Mbeya yenye uzito wa tani 12 ikiwa ni ya nane kwa ukubwa duniani kati ya nyota au vimondo zaidi ya 600 zilizoanguka toka angani.
Uchunguzi umebaini kuwa kivutio hicho licha ya kuwa ni adimu na cha kipekee hakuna jitihada za makusudi ambazo zimefanywa kukihifadhi,kukitangaza na kukiendeleza ili kuvutia idadi kubwa ya watalii wa ndani na nje hali ambayo ingeweza kuinua kipato kutokana na viingilio ambavyo wangelipia watalii pamoja na kutoa ajira endapo maeneo hayo yangendelezwa kwa kujenga hoteli,usafiri kwa watalii na nyumba za kulala wageni.
Keneth Mwazembe ni mwanaharakati wa utalii katika wilaya ya Mbozi anasema licha ya nyota au kimondo kuanguka kwa miaka mingi katika kijiji cha Ndolezi wilayani humo idara ya mambo ya kale imeshindwa kukiendeleza kimondo hicho ambacho kinaongoza kwa ukubwa kuliko vimondo vyote hapa nchini hivyo kuwa kivutio adimu ulimwenguni.
Mtu anapopita barabarani jirani na eneo la kimondo hicho anakiona moja kwa moja na kwa kweli hakuna sababu ya kulipia ambapo utaratibu wa kulipia ambao umewekwa na wahifadhi wa kimondo hicho hauna tija kwa sababu endapo mmetembelea watu watatu ambaye anataka maelezo ya ya historia ya kimondo ndiye anayelipia wengine wanakiona kimondo hicho bila kulipia.
“Kwa kweli nyota hii licha ya kuwa na sifa nyingi ,mahali kilipo ni pa wazi kabisa,hakijaendelezwa kwa kujengewa uzio,mtu akipita barabarani anakiona hivyo hata haja ya kutoa ada ya kiingilio inaonekana haina sababu,lakini iwapo nyota hiyo ingeendelezwa pamoja na eneo lenyewe kuboreshwa,kujenga hoteli na vivutio vingine serikali ingepata pesa nyingi na wananchi wangepata maendeleo makubwa kiuchumi”,anasisitiza Mwazembe.
Mwazembe anabainisha zaidi kuwa kutokana na uhifadhi na uendelezaji wa eneo la kimondo hicho kutofanyika katika kiwango kikubwa inaonesha wazi kuwa idara ya mambo ya kale katika Halmashauri ya wilaya ya Mbozi imeshindwa kuwajibika ipasavyo licha ya kuwa na kivutio ambacho kingeleta watalii wengi wa ndani na nje ya nchi.
Mwazembe anasema kimondo cha Mbozi ni cha nane kwa ukubwa kati ya vimondo karibu 600 vilivyoanguka sehemu mbalimbali duniani kina uzito wa tani 12,ni kimondo cha pekee chenye madini aina tano huku madini ya chuma yakishika asilimia zaidi ya 90 ya kimondo hicho hali ambayo inavutia watalii wengi kumiminika ili kukiona kwa sifa zake hazilingani na kimondo kingine chochote ulimwenguni.
“Wizara ya maliasili na utalii,Bodi ya utalii Tanzania inajua sifa za kimondo hicho lakini mimi nasema bado hatua za kukitangaza na kukiendeleza hazijafanyika ipasavyo kwa mfano hata watalii ambao wanafika hapa kwenye kimondo wanafikia kwanza Iringa kwa kupewa waongoza watalii wa Iringa ili kuwaleta hapa Mbozi kwa kweli hili ni kosa walitakiwa waje moja kwa moja Mbeya ndiyo waongozwe kuletwa hapa Mbozi”anasema.
Hata hivyo Mwazembe anasisitiza kuwa utalii katika mkoa wa Mbeya bado upo nyuma na kwamba kimondo cha Mbozi bado hakijatangazwa kiasi cha kutosha hali ambayo imesababisha mataifa mbalimbali kutokitambua kimondo hicho na kusisitiza kuwa mkoa wa Mbeya unatakiwa kuwajibika moja kwa moja kuvitangaza vivutio hivyo kwa kutumia vyombo vya habari vya kitaifa pamoja na vilivyopo ndani ya mkoa.
Mhifadhi msaidizi wa idara ya mambo ya kale katika Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Filmerick Bassange ambaye anahusika na uhifadhi wa kimondo cha Mbozi anasema licha ya kimondo hicho kukabiliwa na changamoto mbalimbali,serikali imeweza kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo za kukiingiza kimondo kwenye sheria ya mambo ya kale mara baada ya uhuru mwaka 1964 hivyo kukitambua na kutoa ulinzi ili kisiendelee kuhujumiwa.
“ Uboreshaji wa eneo la kimondo unaenda hatua kwa hatua,historia ya vivutio vya utalii vya kiutamaduni na mambo ya kale vilivyotambuliwa vipo sehemu mbalimbali hapa nchini,ukivitembelea vivutio hivyo bado havitaendelezwa hata kufikia nusu ya uendelezaji wa kimondo,katika mkoa wa Mbeya vivutio vipo vingi mfano nyayo wa binadamu wa kale,michoro ya kale,ziwa la Mungu,maji moto hebu nenda ukaangalie hakuna kitu chochote ambacho kimeendelezwa”,anasisitiza.
Gilbert Twente ni mmoja wa wahifadhi wa kimondo cha Mbozi anasema idadi kubwa ya watalii wanaongoza kwa kutembelea kimondo hicho ni wanafunzi wa shule za msingi,sekondari na vyuo ambao wanafika hapo kujifunza kwa vitendo wanapofikia mada ya sayansi inayohusiana na kimondo.
Anasema watalii kutoka nje ya nchi wanaofika kutembelea kimondo hicho idadi yao bado ni ndogo ukilinganisha na sifa za kimondo hicho na kwamba hali hiyo inatokana eneo hilo kutoendelezwa,kutoboreshwa na kutotangazwa kiasi cha kutosha katika vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa.
Philipo Maligisu ni mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa anasema kimondo cha Mbozi ni kivutio adimu ukilinganisha na vimondo vingine vilivyoanguka sehemu mbalimbali ulimwenguni kikiwemo cha nchini ambacho kilionekana wakati kinaanguka kina asilimia ndogo sana ya madini ya chuma ukilinganisha na kimondo cha Mbozi chenye madini ya chuma kwa zaidi ya asilimia 90.
“Kimondo cha Mbozi katika historia ya vimondo vyote duniani hakikubahatika kushuhudiwa na mtu yeyote wakati kinashuka toka kwenye obiti yake angani kuja duniani mwaka 1840,lakini kitu kingine kinachowavutia wengi ni kwamba kimondo hiki kimekuja kuonekana tayari kikiwa chini wakati wa utawala wa Mjerumani mwaka 1930 ambapo watalaamu wa kijerumani mwaka 1931 walikata kipande cha kimondo na kupima baada ya kufanya utafiti na kupata data zote kama ubora,ukubwa,upana na urefu”,anasema.
Kimondo cha Mbozi kina urefu wa mita tatu,unene wa mita 1.12,upana mita moja na uzito wa tani 12,hapa nchini hadi sasa kuna vimondo vinane vilivyoanguka katika sehemu mbalimbali nchini lakini kati ya vyote kinachoongoza kwa ukubwa hapa nchini ni kimondo cha Mbozi,kina sifa ya kipekee ya kuongoza kwa ubora duniani ni cha nane kwa ukubwa kati ya vimondo karibu 600 vilivyoanguka duniani kote.
Mhifadhi kiongozi kutoka makumbusho ya Taifa anavitaja vimondo vingine ambavyo vimeanguka katika sehemu mbalimbali nchini ambavyo uzito wake hauzidi hata kilo moja kuwa ni cha Lichinga mkoani Mtwara kilionekana kwa macho wakati kinaanguka mwaka 1949,kimondo kingine ni cha Mbulu mkoani Manyara ambacho hakikuonekana wakati kinaanguka toka angani.
Kulingana na mtaalamu huyo vimondo vingine vidogo vimeanguka mkoani Mbeya kikiwemo cha Ivuna Mbozi ambacho kilionekana kwa macho wakati kinachomoka toka angani mwaka 1938 na kufanya wilaya hiyo kuwa na vimondo viwili ambapo kimondo kingine kipo katika eneo la Malampaka mkoa wa Shinyanga ambacho kilionekana kwa macho wakati kinashuka mwaka 1930.
Kimondo kingine kidogo kipo Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma ambacho katika historia ya nchi yetu ndiyo cha kwanza kuonekana kwa macho mwaka 1899 ambapo mji huo mkongwe wa kihistoria wakati huo ulikuwa chini ya wamisionari ambao walikijua na ni watalaamu ambao walizoea kuona kwao wakati vimondo vinashuka hivyo waliwafahamisha wenyeji ambao walikishuhudia wakati kinashuka toka angani .
“Kimondo ni kivutio adimu cha utalii kwa kuwa watalii wengi wanasafiri na kuja hapa nchini ili kuona maajabu ya vitu ambavyo vimemeguka kutoka sayari nyingine katika anga za mbali na kushuka kama nyota hadi katika dunia tunayoishi wanapenda kujifunza vitu vingine ambavyo havipatikani katika dunia tunayoishi”,anasema Maligisu.
Hata hivyo mtaalamu huyo wa mambo ya kale amesema jamii inatakiwa kufahamu kuwa kimondo cha Mbozi ni hazina kubwa ya kipekee ambayo inatakiwa kulindwa na kuendelezwa kwa kuwa watu wengi wanapenda kufika kujifunza kielimu na kisayansi kwa kuwa watu wanapenda kufanya utafiti kwanini nyota hiyo iliangukia eneo hilo.
Maligisu anasema eneo la kimondo likiendelezwa linaweza kuwa chanzo cha kupunguza umaskini wa kipato kwa kuwa watalii wanapotembelea wanalipa kiingilio,watalipia chakula ambacho kitauzwa kwa watalii na watalipia usafiri pamoja na vifaa mbalimbali vya kiutamaduni kama vinyago na vifaa vingine vya asili ambavyo wanaweza kuviuza kwa watalii hao.
“Kazi kubwa inayotukabili sisi watumishi wa wizara ya maliasili na utalii hasa katika idara ya mambo ya kale na makumbusho kwa ujumla katika nchi nzima kuongeza nguvu za ufahamu na elimu ya utalii kwa wananchi kuweza kutambua malikale zilizopo katika maeneo yao kama kimondo,pamoja na kuvitangaza ili vifahamike ndani na nje ya nchi,watalii wengi watamiminika na serikali itaongeza pato lake mara dufu”,anasema.
Baruapepe amidelo@yahoo.com,simu
Simu 0766463129
http://www.maendeleo/nivita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment