Tuesday, February 1, 2011

Hii ni hatari darasa la kwanza hadi la tano wanasomea kwenye chumba kimoja?

 
Baadhi ya wanafunzi  viziwi wa shule ya msingi Rahaleo manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wakisomea katika chumba kimoja cha darasa kuanzia darasa la kwanza hadi la tano,hali hiyo inachangia wanafunzi kuwa watoro,nyuma waliosimama ni walimu wao picha na Albano Midelo
Na Albano Midelo.

MTAZAMO wa jamii kwa watu wenye ulemavu bado umekuwa ni hasi kwa kuwa anachukuliwa kuwa ni tegemezi,ombaomba na mtu asiyeweza kuwa na mchango wowote katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Mtazamo huu wa jamii umemtenga mwenye ulemavu na kumnyima haki za kimsingi kama binadamu wengine na kumdidimiza mlemavu huyo kimaendeleo hali ambayo inamfanya ashindwe kujikomboa katika dimbwi la umaskini hivyo kusababisha umasikini wake kuwa mara dufu.

Mtazamo potofu dhidi ya watu wenye ulemavu umesababisha hata wakati mwingine watu kushindwa kuwasaidia wakidhani kuwa ulemavu unaambukiza kitu ambacho sio sahihi kwa kuwa ulemavu ni kasoro katika mwili ambazo husababisha na sababu mbalimbali kama vile magonjwa,ajali na sababu nyingine ,pia jamii inatakiwa kutambua kuwa ulemavu sio laana kwa kuwa sisi sote ni walemavu watarajiwa.

Ni wajibu wa jamii kuanzia ngazi ya familia,mtaa,kitongoji,kijiji,kata,wilaya,mkoa hadi Taifa kupambana na mitazamo potofu  inayosababisha walemavu kubaguliwa hivyo kushindwa kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu,afya,michezo pamoja na haki nyingine ambazo wanapatiwa watu wasiokuwa na ulemavu.

Inasikitisha unapokuta unakwenda mahali nchini na kukuta watu wenye ulemavu jamii inashindwa kuwapatia haki sawa na watu wengine wasiokuwa na ulemavu hali hii inaonesha ni ubaguzi katika kundi hili maalum ambalo linatakiwa kukombolewa ili kupunguza utegemezi katika jamii.

Hivi karibuni nimetembelea wilaya ya Mtwara kwa lengo la kuchunguza  iwapo walemavu wanatendewa haki na jamii  katika haki zao za msingi ,hata hivyo nililenga zaidi katika elimu ambayo ndiyo ukombozi pekee kwa watu wenye ulemavu wa aina zote .

Nafika katika Halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo katika Halmashauri nzima kuna kitengo kimoja tu cha walemavu viziwi ambacho kinaitwa Rahaleo ambacho kina wanafunzi viziwi kuanzia darasa la kwanza hadi la sita wapatao 28 pamoja na  walimu wa walemavu watatu  .

Michael Mrekoni ni mkuu msaidizi wa kitengo hicho cha walemavu cha Rahaleo  anasema kitengo hicho kina vyumba viwili tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba saba na kwamba kutokana na hali hiyo darasa la kwanza hadi la tano wapatao 22 wanasoma katika chumba kimoja cha darasa kwa kutumia ubao mmoja ambapo darasa la sita pekee lenye wanafunzi watano ndiyo wanasoma katika chumba ambacho hata hivyo bado hakijakamilika.
Licha ya kitengo hicho kukabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa Mrekoni anazitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa walimu watalaamu,vitabu,vifaa vya kufundishia  na kujifunzia na nyumba za walimu na ametoa wito kwa serikali kukiangalia kitengo hicho kwa macho mawili ili kiweze kutoa elimu bora.

“Kitengo chetu kina upungufu wa madawati 25,meza nne,viti 11,kabati sita,benchi nane,upungufu wa nyumba za walimu tano.stoo moja,maktaba moja,ofisi moja ya walimu,madarasa sita, vyumba viwili vya speech room,seti ya speech trainer moja,seti ya kutengenezea ear mould moja audiometer hearing aids moja,ottoscope moja na looking mirrors moja pia tunaomba watoto wapatiwe chakula cha mchana hapa shuleni”,anasema.

Carolinie Chitumbi ni mkuu wa kitengo cha  walemavu shule ya msingi Rahaleo anaelezea adha ambayo wanaipata walimu kutokana na kufundisha madarasa matano ya walemavu katika chumba kimoja cha darasa wakiwa wamepangwa kimadarasa hali ambayo anasema inasababisha watoto hao walemavu kushindwa kupata elimu bora kama wanayopata watoto wengine  nchini.

“Naomba serikali itusaidie hebu angalia madarasa matano wanasoma katika chumba kimoja,walimu tumekata tamaa ya kuendelea kufundisha katika kitengo hiki,hali ni mbaya sio kwa walimu tu hata wanafunzi wenyewe baadhi yao wamekuwa watoro wanashindwa kuvumilia vipindi darasani tumejaribu kuweka awamu mbili za ufundishaji  awamu ya kwanza kuanzia saa mbili  na awamu ya pili kuanzia saa nne  kwa walemavu  hali ni mbaya sana”,anasisitiza.

 Ahmadi Tufanye ni mmoja wa walimu wa walemavu katika kitengo hicho anasema wanafanyakazi katika mazingira magumu ya ufundishaji kwa watoto wenye ulemavu kutokana na walimu wote kufundisha madarasa matano katika chumba kimoja ,wazazi ,walezi na wadau wengine wa elimu hapa Mtwara hata hawashituki,sisi wasiporekebisha hali hii ni afadhali tuhamie katika Halmashauri nyingine nchini”,anasema.

“Tunaomba tuongezewe vyumba vya madarasa,tunafanyakazi katika mazingira magumu sana,hatuna vifaa vya kufundishia na kujifunzia,vifaa vya upimaji,tunaomba chakula cha mchana kwa wanafunzi ili iwe chachu kwa wanafunzi kama ilivyo katika shule nyingine za walemavu nchini ambazo zinatoa chakula na wanafunzi wanalala bwenini hivyo kupunguza utoro katika kiwango kikubwa”,anasema.

Hata hivyo Ahmed anadai kuwa katika manispaa ya Mtwara kuna walimu karibu saba ambao wamesomea kufundisha watu wenye ulemavu lakini hawataki kuomba kufundisha katika kitengo hicho kutokana na mazingira duni ya kufundishia hivyo wameamua ni bora waendelee kufundisha katika shule za kawaida ambazo zina mazingira bora ya kufundishia.

Juma Nasoro ni mwanaharakati wa mjini Mtwara anasema amesikitishwa na taarifa za watoto wenye ulemavu katika kitengo cha Rahaleo madarasa matano kufundishwa katika chumba kimoja  hali ambayo anasema kwa vyovyote vile walemavu hao hawawezi kupata elimu bora na hata walimu hawawezi kutoa elimu bora na yenye tija katika mazingira kama hayo.

“Siamini  hivi sasa kama kuna sehemu hapa nchini  wanafunzi wanasoma kuanzia darasa la kwanza hadi la tano  katika chumba kimoja cha darasa,hii ni aibu kwa wananchi wa manispaa ya Mtwara na hasa Baraza la madiwani  kwa kuwa inadhihirisha wazi kuwa hawatambui kama kuna watu wenye ulemavu wanaohitaji elimu maalum wanawekwa kama mifugo kwenye chumba kimoja”,anasema.

“Ninachojua mimi serikali katika Halmashauri zote nchini inatoa fedha za kuendeshea  elimu ikiwemo elimu maalum mimi sielewi inakuwaje katika Halmashauri ya Mtwara Mikindani kwamba eti wanakosa fedha za kujengea vyumba vya madarasa kwa ajili ya walemavu au hata kuanzisha shule za walemavu je pesa za walemavu zinatumika kwa matumizi gani “,anahoji mwanaharakati huyo kwa hasira.

Amina Bakari mkazi wa mjini Mtwara anadai kuwa  mwamko wa elimu hasa kwa wanafunzi wenye ulemavu  bado ni tatizo kwa makundi yote wakiwemo wanasiasa na viongozi wa serikali ambapo wengi wao bado wana imani potofu kutokana na kutobahatika kuishi au kuchangamana na watu wenye ulemavu.

“Viongozi wa serikali na wanasiasa katika ngazi mbalimbali wapo katika kundi la mtazamo zaidi ya uhalisia kuhusu watu wenye ulemavu hivyo wanasita kujiuhusisha na kujua mahitaji ya walemavu au kutoa mchango kwa lengo la kumkomboa mwenye ulemavu,walemavu wanatakiwa wajengewe mazingira rafiki kulingana na mahitaji yao”,anasema.

Wanafunzi viziwi wanaosoma katika shule ya Rahaleo  akiwemo Abdalah Juma na Said Ng’itu wanasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali  kutokana na kusoma shule hiyo ambayo haitoi chakula wala malazi hivyo wanafunzi wakishamaliza muda wa masomo wanasumbuliwa na makondakta wanapokuja asubuhi shuleni na wanaporudi nyumbani.

 “Sisi ni viziwi mawasiliano yetu tunategemea zaidi lugha ya alama baadhi ya makondakta tunawasiliana wale ambao wametuzoea lakini makondakta wapya hatuelewani hivyo mara nyingi wanatuacha kwenye vituo vya daladala tuna sota kwa muda mrefu hali ambayo imesababisha wengi kuwa watoro na wengine kuamua kuacha kabisa shule”,wanasema.

Ally Ndale ni mratibu wa elimu maalum katika Halmashauri ya manispaa ya Mtwara Mikindani amekiri walemavu katika Halmashauri hiyo kukabiliwa na changamoto mbalimbali na kwamba hivi sasa wamejipanga kuhakikisha kuwa changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana serikali,wadau wa elimu pamoja na wananchi ili kuboresha elimu kwa wenye ulemavu.

Baruapepe amidelo@yahoo.com,simu 0766463129.









No comments:

Post a Comment