Monday, February 7, 2011

Mkakati wa kuboresha huduma za afya hospitali ya mkoa wa Ruvuma


Na Albano Midelo.

WATUMISHI wa hospitali ya serikali ya mkoa wa Ruvuma iliyopo mjini Songea wanakabiliwa na malalamiko mbalimbali ambayo yamekuwa kero kubwa kwa wananchi ambao wafika kupata huduma ya afya.Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasifia huduma za hospitali hiyo huku wengine wakiponda kuwa huduma ni mbovu .

Miongoni mwa malalamiko ambayo yanatolewa na wananchi kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Ruvuma ni pamoja na kuchelewa kuwapatia huduma kwa makusudi au kutaka kitu kidogo,lugha ya matusi,kutopewa madawa na kulazimika kununua dawa katika maduka.

Malalamiko mengine ni wagonjwa wanaofika kutibiwa majira ya usiku wakiwemo wajawazito wanafika kujifungua au kujitazamia pamoja na wagonjwa waliopata ajali za pikipiki au gari kuchelewa kupata huduma na wengine kutohudumiwa hadi watoe kitu kidogo.

Kufuatia malalamiko hayo ambayo uongozi wa serikali na watumishi wa afya baadhi yao wamekiri yanafanywa na baadhi ya wauguzi na madaktari wasiokuwa na maadili yametolewa mapendekezo ya kupunguza au kumaliza matatizo hayo na kufanya hospitali hiyo kuwa kimbilio la wanyonge katika mahojiano maalum na watu mbalimbali yaliofanywa na mwandishi wa makala haya .

Mohamed Kudeka mkazi wa Msalama mjini Songea anasema viongozi ngazi ya wilaya na mkoa waende kutibiwa kwenye hospitali ya mkoa kama wananchi  wa kawaida bila kwenda na magari yao ili wakaone shida wanazopata wananchi wa kawaida ni saa ngapi wanatumia bila kufanikiwa kumuona daktari ili wajifunze athari wanazopata wanyonge na kuwajibika kuwasaidia.

Anasisitiza kuwa matatizo haya yanaendelea kutokea katika hospitali ya mkoa kwa sababu hakuna anayewajibika ipasavyo kuwasimamia watumishi wenye tamaa ya kujipatia mali na kusahau wajibu wao kwa jamii wa kuwahudumia wagonjwa hali ambayo inasababisha wananchi kuendelea kupoteza maisha na kukosa huduma bora.

Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela ameahidi kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za haraka kukabiliana na malalamiko  kwa baadhi ya watumishi kukiuka maadili ya kazi ambapo ameahidi moja ya hatua zitakazochukuliwa ni wauguzi wote kupiga kura ili kutambua nani wanafanya mchezo huo mchafu unaowapaka matope watumishi wote wa hospitali ya mkoa.

 “Tutawabadilisha wauguzi wote watuhumiwa kutoka  zamu za usiku na kuwapangia zamu za mchana chini ya usimamizi maalum,Sasa nadhani tabia hiyo iliyokuwepo siku za nyuma inajirudia Itakuwa inachangiwa na  baadhi ya watumishi hawa wapya. Unajua kutokana na uhaba mkubwa wa watumishi katika idara ya afya, serikali imepeleka vijana wengi kusomea fani hii na wengine wameingia ‘bora kupata ajira huku wakikiuka maadili’” anafafanua.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma anasema jitihada zinafanywa na serikali ili kuhakikisha watumishi wa afya wanatoa huduma bora ,yamewekwa  masanduku ya maoni ili wananchi wenyewe watakapoana hawakutendewa haki katika huduma watoe taarifa ili serikali iweze kuchukua hatua kali kwa wahusika.

Hata hivyo anasema wakati mwingine anasikia mitaani kuwa muuguzi au daktari fulani amemnyanyasa mama mjamzito hadi amepoteza maisha bila kutoa taarifa rasmi katika ofisi husika hivyo ametoa wito kwa wananchi wasichoke kutoa taarifa namna walivyotendewa na watumishi wa afya ili kupunguza vifo na kupata huduma bora ya afya.

 "Katika hospitali ya mkoa tumeweka masanduku mawili moja ni kwa ajili ya uongozi wa ndani ya hospitali ambapo baada ya kufunguliwa sanduku hilo timu ya utawala itakaa na kusoma maoni hayo ili kujua wananchi wanasema nini na katika sanduku la pili litafunguliwa katika ofisi ya mkoa ili kujua wananchi wanasema nini kuhusu huduma wanazopewa katika hospitali hiyo ili kuchukua hatua pale penye mapungufu ",anasisitiza Dk. Ishengoma.

Anasema sio lengo la mkoa kuona huduma za afya kwa akinamama wajawazito zinazorota na kusababisha vifo, fistula na ulemavu wa kudumu na kwamba mkoa unajitahidi kuajiri watumishi wa afya,na kwamba ajira hizo hazitekelezeki katika kasi inayotakiwa kutokana na watumishi wengi kutofika katika mkoa kutokana na baadhi ya mazingira kudhani ni ya kutisha kama vile Tunduru ya zamani.

 Ametoa wito kwa wataalamu wa afya wanaoajiriwa kufika mkoani Ruvuma kufanyakazi wafike katika vituo walivyopangiwa badala ya kuogopa na kudhani ni mkoa wa pembezoni jambo ambalo amesema sio sahihi kwa kuwa Ruvuma ni sawa na mikoa mingine ya Tanzania na kwamba kutofika kwao kunafanya uhaba wa watumishi kuendelea hivyo kuwaathiri wanawake na watoto.

 "Taifa hivi sasa linafanya jitihada mbalimbali za kusomesha wanafunzi wengi zaidi,katika mkoa wetu chuo cha Tunduru kilichokuwa MCH kimefunguliwa na kuanza kutoa mafunzo ya uuguzi tena,chuo cha maofisa tabibu cha Songea mjini, sasa kinachukua wanafunzi wengi walio makazini na wanaotoka moja kwa moja sekondari hivyo tutapata wataamu wengi wa afya watakapohitimu",anasema.

Huduma katika hospitali  ya serikali ya mkoa wa Ruvuma  endapo itaboresha na kusimamia utendaji kazi kwa watumishi wake pamoja na uwepo wa madawa na vitendea kazi  naamini wagonjwa wanaofika kutibiwa katika hospitali hiyo watapata huduma bora na kwa wakati  isingeweza kutokea kwa mfano hai wa mwandisi wa ujenzi wa wilaya ya Namtumbo Nelson Mpangala aliyepata ajali ya gari na kupoteza maisha Oktoba 28,2010  baada ya kukaa kwa zaidi ya saa mbili akisubiri huduma katika hospitali ya mkoa huku akivuja damu kwa wingi hadi akafariki dunia .
Simu 0766463129














No comments:

Post a Comment