Na Albano Midelo.
WAPO wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu wanaoamini kuwa ulemavu ni laana kutoka kwa mwenyezi Mungu hali ambayo inasababisha wanapokuwa wa watoto wenye ulemavu kuwatelekeza au kuwafungia ndani ili kuficha aibu ya laana hiyo.
Jambo la kusikitisha zaidi kuwa wapo baadhi ya wazazi na walezi wanadiriki kuwaua watoto wenye ulemavu eti kuficha aibu na laana ambayo imetokea kwenye familia,jamii inatakiwa kutambua kuwa ulemavu sio laana bali ni mipango ya Mungu kwa kuwa mtu anaweza kupata ulemavu kutokana na sababu mbalimbali.
Uchunguzi ambao umefanywa katika wilaya ya Mtwara umebaini kuwa wazazi na walezi wengi bado wana mtazamo potofu kuhusu watoto wenye ulemavu hali ambayo imesababisha kuwanyanyapaa,kuwatenga na kutowapatia haki za msingi ikiwemo kupata elimu ya awali, msingi,sekondari na elimu ya juu.
Wanafunzi viziwi wanaosoma katika shule ya Rahaleo manispaa ya Mtwara wapatao 28 akiwemo Abdalah Said na Seleman Ng’itu wanasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na kusoma shule hiyo ambayo haitoi chakula wala malazi hivyo wanafunzi wakishamaliza muda wa masomo wanarudi nyumbani.
Walemavu hao wanasema wanajisomesha wao wenyewe kwa kufanya vibarua kwa lengo la kujipatia vifaa muhimu vya shule kama vile sare za shule na vifaa vya kuandikia kama daftari na kalamu kutokana na wazazi na walezi wengi wilayani Mtwara kuwa na mtazamo hasi kuhusu wenye ulemavu.
Tufanye Ahmed mwalimu wa walemavu katika shule ya Rahaleo anasema ameshawatembelea karibu walemavu wote viziwi wanaosoma katika shule hiyo na kukutana na wazazi pamoja na walezi wao na kubaini kuwa robo tatu ya watoto hao wanajitegemea wenyewe karibu kila kitu kwa kufanya vibarua wanaporudi shuleni.
Ahmedi anabainisha zaidi kuwa wanafunzi viziwi wanaosoma katika shule hiyo akiwa Abdalah Said ambaye anasoma darasa la sita baada ya kurudi nyumbani anafanyakazi ya kuuza mafuta kwenye kituo kimoja cha mafuta eneo la Magomeni mjini Mtwara hivyo kuweza kumudu kujipatia mahitaji yake muhimu ya shule.
“Mwanafunzi huyu ni very active na hesabu za mafuta anazifanya vizuri,ingawa ni kiziwi anaweza kuwasiliana na wenye magari ambao wanafika kununua mafuta kwenye kituo anauza na wengi wanafurahia huduma yake na wanamkubali licha ya ulemavu na umri mdogo alionao’,anasema.
Hata hivyo anasema mlemavu huyo anaishi na mama yake mzazi ambaye ameshindwa kumpatia huduma muhimu kwa ajili ya mtoto wake hali ambayo imemlazimu mtoto wake kuamua kujitafutia mwenyewe fedha ambazo zinamwezesha kupata vifaa muhimu vya shule.
Mwanafunzi Abdalah mwenye umri wa miaka tisa anasema anajisomesha mwenyewe kwa kufanya vibarua kwa lengo la kujipatia vifaa muhimu vya shule kama vile sare za shule na vifaa vya kuandikia kama daftari na kalamu kutokana na wazazi na walezi wengi wilayani Mtwara kuwa na mtazamo hasi kuhusu wenye ulemavu.
“Nikitoka shuleni mchana nakwenda kufanyakazi ya kuuza mafuta kwenye kituo cha Magomeni na hata mahesabu haya ya mafuta nayafanya vizuri kiasi kwamba boss wangu ananiaamini sana na kuniachia kazi pia wateja wangu wenye magari tunawasiliana vizuri ,wamenizoea licha ya kuwa mimi ni kiziwi’,anasema Abdalah.
Abdalah anasema anaishi na mama yake ambaye hana kazi wala uwezo wa kuendesha maisha hivyo yeye ndiyo msaada mkubwa katika familia yao ambayo haina baba na kwamba mmiliki wa kituo cha mafuta amefanya naye kazi kwa muda mrefu ambaye anamuhudumia kila kitu pamoja na vifaa muhimu vya shule vikiwemo sare,viatu na vifaa vya kuandikia.
Mwanafunzi mwingine mlemavu kiziwi wa darasa la tatu katika shule ya Rahaleo Seleman Ng’itu(13) anasema alizaliwa akiwa hana ulemavu wowote lakini alipokuwa darasa la pili aliugua malaria na kutibiwa kwa dawa za kwinini ambazo zilimsababisha kupata ulemavu alionao hivi sasa.
Anasema baada ya kupata ulemavu baba yake mzazi aliyemtaja kwa jina la Sulemain Ng’itu mfanyabiashara mwenye mabasi ya abiria mkoani Mtwara alimtenga na kutompatia huduma zozote hivyo akiwa anamtegemea zaidi mzazi mmoja ambaye hana uwezo wa kumsaidia kupata mahitaji muhimu.
“Naishi na mama tu baba ameachana mama, mama hana uwezo wa kunihudumia,nafanya vibarua, napenda shule hasa masomo ya Kiingereza na Jografia kila mwaka katika mitihani hapa shuleni nakamata nafasi ya kwanza tu”,anajigamba mwanafunzi huyo.
Hata hivyo anasema anamatumani makubwa ya kufaulu darasa la saba kwenda shule ya sekondari ingawa ana mashaka makubwa ya kukosa mtu wa kumsomesha kutokana na kutengwa na baba yake ambaye anadai ana uwezo mkubwa wa kifedha lakini ameshindwa kumpatia mahitaji muhimu ya shule baada ya kupata ulemavu.
“Baba ana pesa nyingi lakini kwa kuwa mimi ni mlemavu anakataa kunisaidia,baba yangu ana magari mengi yakiwemo mabasi ambayo yanabeba abiria katika mkoa wa Mtwara,baba anafahamu kabisa kuwa mimi ni mtoto wake lakini hataki kunisaidia amesema nisiende kabisa nyumbani kwake hivi karibuni tulikutana mahakamani kwenye kesi aliyofungua mama”,anadai Ng’itu.
Caroline Chitumbi mwalimu wa walemavu anasema wanafunzi wengi wenye ulemavu wazazi,walezi na jamii kwa ujumla imewatenga kutokana na ulemavu wao hali ambayo imesababisha kukosa haki zao za msingi ikiwemo ya kupata elimu ambayo ni ukombozi katika maisha yao.
Deodatha Mnunduma anaelezea idadi kubwa ya wazazi na walezi katika wilaya ya Mtwara kuwa na mtazamo finyu kwa watoto wenye ulemavu hivyo kushindwa kuwapeleka shule pamoja na kuwapatia mahitaji muhimu kama sare za shule na vifaa kwa wale ambao wamepelekwa shuleni.
Mratibu wa elimu maalum katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara Daniel Mbena anasema wakati anazunguka kutafuta idadi ya walemavu mbalimbali waliopo katika eneo lake alibaini kuwa wazazi na walezi wengi licha ya kuwa na uwezo wa kifedha hawana mwamko wa kuwasaidia watoto wenye ulemavu mahitaji muhimu ya shule hivyo wanawaacha wakisoma bila kuwa na sare,viatu na vifaa vya kuandikia.
“Jamii nzima wakiwemo watendaji wote wa serikali,viongozi wa siasa na taasisi za dini wanatakiwa waone kwamba mlemavu ana haki sawa na watu wengine wasiokuwa walemavu na anatakiwa kupata haki zote za msingi kulingana na mahitaji yao,sera za elimu katika nchi zifanyiwe marekebisho ili zibainishe wazi haki za watu wenye ulemavu kupata elimu”,anasisitiza.
Baruapepe mailto:amidelo@yahoo.com,simu
simu 0766463129
No comments:
Post a Comment