Nini ukweli kuhusu msitu wa serikali wa milima ya Matogoro na athari zake kimazingira?
Na Albano Midelo.
MGOGORO wa kiutendaji unaoendelea katika msitu wa serikali wa milima ya Matogoro uliopo katika manispaa ya Songea mkoani Ruvuma unadaiwa kusababishwa na menejimenti mbili tofauti za kiutawala kufanyakazi katika eneo moja ambapo kila moja inafanyakazi kulingana na taratibu zao kitaaluma.
Uchunguzi umebaini kuwa msitu wa serikali wa Matogoro unamilikiwa na kuhifadhiwa na wizara ya maliasili na utalii tangu miaka 1960 ambapo wizara ya maji kupitia mamlaka ya maji safi na maji taka Songea SOUWASA pia wanatumia vyanzo vya maji vilivyopo kwenye msitu wa Matogoro kwa ajili ya kusambaza maji kwa wananchi wa mji wa Songea.
Hata hivyo kwa mujibu wa watalaamu kutoka wizara ya maliasili na utalii baada ya utafiti uliofanywa na watalaamu wa mazingira kutoka nchini Ujerumani kubaini kuwa miti aina ya mikaratusi na mibani iliyopandwa kwenye msitu huo inapunguza maji kwenye vyanzo, kuchafua maji na kusababisha kupoteza rangi yake ya asili pamoja na kusababisha mmomonyoko wa udongo kutokana na maji mengi kushindwa kuzama ardhini.
Kufuatia matokeo ya utafiti huo,serikali kupitia wizara ya maji iliagiza miti yote kuvunwa kwa awamu kidogo kidogo katika maeneo tofauti hadi kumaliza miti yote na kupandwa miti mingine ya asili kwenye Msitu wa milima ya Matogoro ambapo wizara ya maliasili na utalii ilipendekeza miti yote ya zamani zaidi ivunwa kwanza katika eneo moja na kupanda miti mingine hali ambayo imeleta mgogoro katika menejimenti mbili tofauti.
“Sisi katika wizara ya maliasili tunatakiwa kuvuna miti yote ya zamani zaidi katika eneo moja na kupanda miti ya asili katika eneo moja hadi kumaliza kulingana na umri wa miti hiyo,haiwezekani kuvuna kidogo kidogo kwa maeneo tofauti bila kujali umri wa miti zoezi hilo ambalo watu wa maji walitaka tufanye halitekelezeki ndilo ambalo limeleta mgogoro kati ya watu wa maji na watu wa maliasili”,anasema Enock Buja afisa maliasili wa mkoa wa Ruvuma.
Ofisa wa maliasili wa mkoa wa Ruvuma Enock Buja anasema shamba la miti la serikali la milima ya Matogoro lilianzishwa miaka ya 1950 likiwa na hekari 2259 aina ya mikaratusi na mibani ambapo kutokana na utafiti uliofanywa na Wajerumani mwaka 2000 ulibaini kuwa miti hiyo sio rafiki ya vyanzo vya maji hivyo hivyo serikali ilitoa kibali kwa uongozi wa hifadhi ya msitu wa milima ya Matogoro kuvuna miti hiyo na kupanda miti ya asili.
“Mkataba wa kuvuna miti hiyo unatakiwa ukamilike mwaka 2012 kwa kuhakikisha miti yote ya kupanda inavunwa na kupanda miti ya asili ili kuepusha vyanzo vya maji katika milima hiyo visikauke kutokana na athari za miti hiyo kuonekana kuathiri vyanzo vya maji katika milima ya Matogoro ambavyo vinategemewa na Mamlaka ya maji safi na maji taka Songea SOUWASA kuzalisha maji kwa wananchi wa mji wa Songea”,anasisitiza.
Baada ya serikali kutoa kibali cha kuvunwa miti hiyo hadi sasa tayari uongozi wa msitu wa hifadhi ya milima Matogoro umevuna zaidi ya hekari 1389 na kuuza miti hiyo kwa wafanyabiashara mbalimbali wa mbao kutoka ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma ambapo hadi sasa chini ya hekari 780 tu ndiyo ambazo bado hazijavunwa baada ya serikali ya mkoa wa Ruvuma hivi karibuni kupiga marufuku kuendelea kuvunwa msitu huo katika eneo ambalo limebakia.
Serikali imeamua kupiga marufuku uvunaji wa miti katika msitu wa Matogoro kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unatokea katika msitu wa serikali wa milima ya Matogoro na kusababisha uchafuzi wa maji katika chanzo cha Mto Luhira na chanzo cha mto Ruvuma ambavyo ni miongoni kati ya vyanzo tisa vya maji vinategemewa na SOUWASA kusambaza maji mjini Songea.
Hata hivyo uchunguzi zaidi umebaini kuwa vyanzo vya maji vya mto Ruhila na mto Ruvuma pamoja na vyanzo vingine saba ambavyo vinategemewa na SOUWASA kusambaza maji kwa wakazi wa mji wa Songea havitoshelezi kwa mwaka mzima kutokana na vyanzo hivyo kutokuwa na maji ya kutosheleza idadi kubwa ya wakazi wa mji wa Songea.
Afisa uhusiano wa SOUWASA Silas Bwena anabainisha kuwa mamlaka yake inategemea vyanzo vya maji tisa vikiwemo vya chemchem kutoka katika milima ya Matogoro ambayo hutiririsha maji yake hadi kwenye mtambo wa kuchuja na kutibu maji uliopo Matogoro mjini Songea.
Anabainisha zaidi kuwa vyanzo vya maji vyote tisa vina uwezo wa kutoa meta za ujazo za maji wakati wa kiangazi 6448 na kwamba mahitaji ya maji katika manispaa ya Songea ni meta za ujazo 8138 kwa siku hali ambayo inadhihirisha wazi kuwa vyanzo vya maji katika milima ya Matogoro havitoshelezi mahitaji ya wakazi wa mji wa Songea unaokuwa kwa kasi kubwa.
Kutokana na hali hiyo serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya nchi ya Ujerumani ilifadhili mradi mkubwa wa kuwapatia maji wakazi wa Songea uliyogharimu sh.bilioni 33.2 ambapo uchunguzi wa awali ulipendekeza mradi huo kujengwa kwenye vyanzo vya maji vya mto Lumecha na Luhimba vilivyopo kilometa 29 kutoka mjini Songea vyenye uwezo wa kuzalisha maji meta za ujazo 24,000 kwa siku.
Endapo mradi huo mkubwa wa maji ungejengwa katika vyanzo hivyo ina maana kuwa tatizo la maji katika manispaa ya Songea lingebakia kuwa ni historia kutokana na ukweli kuwa vyanzo vya maji vya Matogoro ambako mradi huo mkubwa umejengwa havitoshelezi mahitaji ya maji kwa wakazi wa mji wa Songea ambapo kumekuwa na mgawo mkali wa maji hasa wakati wa kiangazi na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Hata hivyo afisa uhusiano wa SOUWASA Silas Bwena anadai kuwa mamlaka hiyo iliamua kujenga mradi huo mkubwa katika vyanzo vya maji vya milima ya Matogoro badala ya Lumecha kutokana na gharama kubwa ambazo anadai zingetumika endapo wangejenga mradi katika chanzo cha mto Lumecha ukilinganisha na fedha zilizotolewa na wafadhili wa serikali ya shirikisho la Ujerumani kiasi cha bilioni 33.2 .
Kufuatia mgogoro wa msitu wa Serikali wa milima ya Matogoro kuongozwa na menejimenti mbili tofauti yaani wizara ya maliasili na utalii ambao wanahusika na uhifadhi pamoja na kufanya biashara ya kuuza magogo na wizara ya maji kupitia SOUWASA ambao wanavuna maji kutoka vyanzo vya maji katika milima hiyo ili kusambaza maji kwa wakazi wa mji wa Songea ,mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma amepiga marufuku kazi ya kuvuna miti katika msitu huo hadi Tume aliyoiunda itakapokamilisha kazi ya uchunguzi kutokana na uharibifu wa mazingira ambao unadaiwa kufanywa kwenye chanzo cha mto Ruvuma kilichopo kwenye msitu wa serikali wa Matogoro.
Msitu wa serikali wa milima ya Matogoro unakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo uchomaji holela wa moto karibu kila mwaka hali ambayo inasababisha maelfu ya miti ya asili kuteketea kwa moto,pia wananchi wanaozunguka msitu huo bado wanaendelea kulima mbogamboga katika vyanzo vya maji pamoja na kupulizia dawa za kuulia wadudu kwenye mbogamboga hizo zenye kemikali zenye sumu zinazochuruzika na kuingia kwenye vyanzo vya maji hali ambayo inahatarisha maisha ya viumbehai wakiwemo binadamu.
Wafanyabiashara wanaovuna misitu kwenye msitu huo wa serikali ambao hawakuwa tayari majina yao kuandikwa gazetini, wanadai kuwa wamepewa kibali na wizara ya maliasili na utalii katika mkataba maalum wa kiserikali na kwamba kuzuiwa kuendelea kuvuna misitu kwenye msitu huo licha ya kuwatia hasara kubwa lakini pia ni kuvunja mkataba na kwamba wanatarajia kuifikisha serikali mahakamani.
Mkurugenzi wa misitu na nyuki kutoka wizara ya maliasili na utalii ambao ndiyo wamiliki wa misitu yote ya serikali nchini wanatarajia kufika mkoani Ruvuma ili kutafutia ufumbuzi wa kudumu sakata hilo linalozikabili menejimenti mbili za serikali jambo linalowachanganya wadau na wanaharakati wengi wa mambo ya mazingira katika mkoa wa Ruvuma.
Baruapepe amidelo@yahoo.com
Simu:0766463129.
No comments:
Post a Comment