Monday, February 14, 2011

Utalii wa kiutamaduni mwambao mwa ziwa Nyasa una nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa mtu binafsi na Taifa

Picha inaonesha ngoma maarufu ya mganda mwambao mwa ziwa Nyasa
Na Albano Midelo.

UTALII wa kiutamaduni bado ni nadharia changa katika nchi za ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania,kutokana na ukweli kuwa katika nchi hizo wamezoea kuona utalii wa asili wa kutembelea mbuga za wanyama.

 Utalii wa kiutamaduni ni nadharia mpya hapa nchini ambapo serikali imeanza kuutambua utalii wa kiutamaduni na kuupa nguvu kubwa aina hiyo ya utalii miaka ya hivi karibuni,zamani vivutio vya utalii wa kiutamduni kama majengo ya kale,maeneo ya kihistoria na makumbusho hayakupewa mtazamo wa kiuchumi zaidi.

Maeneo hayo yalipewa mtazamo wa kielimu zaidi na kuundwa idara za mambo ya kale na idara ya makumbusho ambazo zote awali zilikuwa katika wizara ya elimu na utamaduni ambavyo viliwekwa kama vyanzo vya elimu zaidi kuliko vyanzo vya utalii kwa sababu wakati ule  watalaamu walifanya tafiti mbalimbali za mambo ya kale wakiwemo wakina Dk.Leakey

Hata hivyo baadaye kulikuwa na mabadiliko katika ulimwengu mzima hali iliyosukuma kuwepo kwa utalii wa kiutamduni na nchi zilianza kutoa kipaumbele katika utalii wa kiutamaduni ndiyo maana hapa nchini idara za mambo ya kale na makumbusho zilihamishwa kutoka wizara ya elimu na kuingia katika wizara ya utalii na maliasili.

 Utalii wa kiutamadini hivi sasa unakuwa na  hata mabadiliko ya utalii huo hayawezi kuonekana kwa haraka badala yake inatakiwa watalaamu kuwahamasisha wananchi kutambua fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii na kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo wao binafsi na Taifa kwa ujumla wake.

Ni vigumu sana kutenganisha utalii asili na  utalii wa kiutamduni kutokana na aina hizo mbili za utalii kuwa na mahusiano ya karibu.Watalii wanapongia nchini wote wanavutika na utalii wa aina zote mbili  .

Mtalii anapokwenda kutembelea utalii wa asili kama mbuga za wanyama pia anaweza kupita katika maeneo yenye utalii wa kiutamaduni na kwamba fursa ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa kwa wananchi wa kawaida kuliko aina nyingine za utalii.

Mhadhili msaidizi kutoka idara ya utalii wa kiutamaduni chuo kikuu kishiriki cha Tumaini mkoani Iringa Frank Kimaro anabainisha kuwa  utalii wa kiutamaduni unazungumzia jamii husika na kwamba jamii hiyo inaweza kufaidika kutokana na utalii wa kiutamaduni ambao unapatikana katika eneo husika hadi kufikia hadi ngazi ya kitaifa.

“Unaweza kuona aina hii ya utalii ni tofauti na utalii wa asili ambao tunaangalia zaidi mbunga za wanyama na maeneo ambayo yametengwa na serikali ambapo wahusika wakubwa ni serikali yenyewe na siyo watu binafsi,katika utalii wa kiutamaduni wahusika wakuu ni  wananchi wenyewe”,anasisitiza  na kuongeza

“Wananchi katika utalii wa utamaduni wanaweza kunufaika kuanzia kiwango cha familia,mtaa,kitongoji,kijiji,wilaya,mkoa na kitaifa kwa hiyo utalii wa kiutamaduni unatoa fursa kubwa sana ya ukuaji wa uchumi kuanzia kwa mtu binafsi hadi kwa taifa”

Hata hivyo inalezwa kuwa licha ya utalii wa utamaduni kuonekana kumlenga zaidi mwananchi wa kawaida ,lakini kipato anachopata mwananchi huyo kwa kucheza ngoma au kuuza bidhaa za jadi na kazi nyingine za mikono kipato chake kimekuwa cha chini na kuwakatisha tamaa wananchi.

Kimaro anasema kuwa vitu anavyovifanya mwananchi katika utalii wa kiutamaduni vina thamani kubwa kuliko mapato anayopata na kwamba katika hali ya kawaida vitu vya utamaduni vina thamani kubwa  na vikiachwa kupotea haviwezi kupatikana tena na kwamba hakuna kiwango cha malipo kamili kwa shughuli za utalii wa kiutamaduni.


Bidhaa zinazotokana na utalii wa kiutamaduni kama samani zilizotengezewa kwa miti pamoja na sanamu za kuchonga zimekuwa zinauzwa na watu binafsi kwa watalii na wageni wengine kwa bei za juu sana kwa mfano kiti kinachotengezwa kwa kutumia miti ya mianzi kinauzwa kati ya shilingi 200,000 hadi 300,000,

kofia inayotengenezwa kwa ukindu inauzwa kati ya shilingi 3500 hadi 5000,mkanda unaotengenezwa kwa ngozi  yenye shanga unauzwa kati ya shilingi 5000 hadi 10,000,kigoda kilichotengenezwa kwa mti wa kawaida kinauzwa kati ya shilingi 10,000 hadi 15,000 wakati kinyago cha kuchongwa kinauzwa kuanzia shilingi 20,000 hadi 500,000 kutegemea na ukubwa wa kinyago hicho.

Nafasi ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa katika kukuza uchumi wa nchi  kutokana na ukweli kuwa utalii unachangia uchumi wa Tanzania katika kiwango kikubwa  na kuchukua nafasi ya pili hivyo utalii endelevu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo endelevu. Watu wanaonufaika katika sekta ya utalii wa kiutamduni kutoka katika migongo ya watu wengine  ni pamoja na watu wenye hoteli,nyumba za kulala wageni,watu wanaouza maji na vyakula mbalimbali na kwamba  utalii huo unafungua milango ya ajira.

Akizungumzia utalii wa kiutamaduni kuhusu ngoma za mganda na kioda ambazo ni maarufu kwa wakazi wa mwambao mwa  ziwa Nyasa  mbunge wa viti maalum wanawake Injinia Manyanya anasema ngoma hizo ambazo ni kivutio adimu  huchezwa kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba kila mwaka ambapo kikundi kimoja cha ngoma kinalika vikundi saba hadi kumi vya ngoma kutoka vijiji vingine mwambao mwa ziwa Nyasa na kufanya mashindano makubwa ya ngoma.

“Ngoma hizi za asili huchezwa wakati wa kiangazi isipokuwa iwapo watalii wanataka kuziona ngoma hizo  kikundi hicho kinaweza kucheza ngoma hizo wakati wowote ngoma hizo kwa kawaida zinachezwa wakati wa kiangazi kwa sababu ni wakati wa mavuno wananchi wanakuwa wamemaliza kazi ya kilimo,ngoma hizi hukusanya idadi kubwa ya watazamaji kutoka mwambao mzima wa ziwa Nyasa,ngoma hizi hujenga urafiki mkubwa  pamoja na mshikamano”,anasema Manyanya.
Tovuti ;www.maendeleo ni vita.blogspot.com


No comments:

Post a Comment