Wakazi wa kijiji cha Kihagara mwambao mwa ziwa Nyasa wakimuonesha mwandishi wa makala haya eneo ambalo wanapatikana vyura wenye uwezo wa kuimba sauti za kuvutia kama binadamu
Na Albano Midelo.
WAZIRI wa maliasili na utalii Ezekiel Maige ameagiza katika nchi nzima kuhakikisha kuwa wadau mbalimbali wanaibua vivutio mbalimbali vya utalii ambavyo vimesahaulika ili kuvitangaza kwa lengo la kuwavutia watalii wa ndani na nje ili kuvitembelea na serikali kupata kipato.
Katika eneo la Kihagara mwambao mwa ziwa Nyasa kuna eneo oevu ambalo lina ukubwa wa karibu meta 300 ambalo linajaa maji na kuwa kivutio cha wanyama mbalimbali wakiwemo ndege aina ya nyangenyange pamoja na chura wenye uwezo wa kuimba nyimbo nzuri kwa sauti tamu na tofauti na chura ambao unawafahamu.
Felician Komba mkazi wa kijiji cha Kihagara anasema eneo hilo ambalo linafanana na ziwa au bwawa ambalo lipo umbali wa kilometa moja na nusu kutoka kijiji cha Kihagara, miaka ya nyuma lilikuwa na maji muda wote hali ambayo ilisababisha idadi kubwa ya samaki wa aina mbalimbali kuzaliana kwa wingi na kulisha karibu kata nzima ya Kihagara ambayo ina vijiji vitano ambavyo ni Kihagara,Mango,Tumbi,Njambe,Ngehe ambapo baada ya kutokea uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji umesababisha bwawa hilo kuanza kukauka na kujaa maji kwa msimu.
Uchunguzi umebaini kuwa mwezi wa tatu hadi wa tano kila mwaka bwawa hilo ujaa maji ambayo yanatoka kwenye mto Mbuchi ambapo maji yanapopungua watu hufika katika bwawa hilo kukamata maelfu ya samaki na kwamba bwawa hilo linapojaa maji linakuwa kivutio cha viumbehai wengi wakiwemo,mamba, maelfu ya ndege aina ya nyangenyage,bata maji wanafika kwa wingi na kuzaliana katika eneo pamoja na bata maji wenye umbo dogo ambao wanamilio ya kuvutia na kupendeza.
“Katika hali ya kustaajabisha bwawa hili likijaa maji lina aina Fulani ya chura warefu,wana ngozi laini weusi kidogo wana uwezo wa kuimba nyimbo nzuri ambazo huwezi kuamini kama wanaoimba chura,nyimbo hizo zinasikika umbali hata wa kilometa tano,chura hao huimba kwa pamoja katika sauti ya kwanza na ya pili,ukiwasogolea wanaendelea kuimba lakini akipita mnyama ambao wanadhani kuwa ni adui wote kwa pamoja wananyamaza”,anasema Felician Komba na kusisitiza kuwa hayo ni maajabu ya mwenyezi Mungu.
Hata hivyo Komba anasema chura hao uendelea kuimba nyimbo hizo hadi mwezi wa nne kila mwaka wakati ambao maji yanakuwa yameanza kukauka katika eneo hilo ambapo chura hao hutoweka tena hadi kipindi kingine ambacho maji yanaanza kujaa kwenye bwawa hilo na kwamba katika kipindi ambacho chura hao wanazaana hawaendelei kuimba tena nyimbo hizo.
Anamtaja adui mkubwa wa chura hao kuwa ni ndege aina ya nyangenyage wenye shingo ndefu ambao wanakula chura hao kwa kuwadonoa wanapowaona katika bwawa hilo ambapo anasisitiza umuhimu wa kuhifadhi bwawa hilo ili viumbe hai waweze kupatikana wakati wote na kuwa kivutio kikubwa cha watalii.
Anasema bata maji ambao wanapatikana katika bwawa hilo nyama yake ni laini yenye radha tamu,pia nyama hiyo haishiki kwenye meno kama ilivyo kwa wanyama wengine ambao humlazimisha mlaji kutafuta kijiti cha kutolea nyama ambazo zimekwama kwenye meno na kuleta kero kubwa kwa walaji.
Komba anasema hivi sasa kijiji cha Kihagara kwa kushirikiana na mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Injinia Stella Manyanya ambaye ni mzaliwa wa kijiji hicho wameweka mikakati kuanzia mwaka huu kuhakikisha kuwa bwawa hilo ambalo ni kivutio cha utalii halikauki badala yake linakuwa na maji wakati wote kama ilivyokuwa zamani na kwamba hilo linawezekana kwa kuhifadhi vyanzo vya maji pamoja na kupanda miti na nyasi ili kuhifadhi eneo hilo.
Kijiji hicho kimekusudia kujenga vibanda vya asili katika eneo la bwawa hilo ili kuwawezesha watalii kukaa wakati wanaona vivutio vilivyopo katika bwawa hilo hali ambayo itaongeza pato kwa kijiji litakalotokana na kodi watakazolipia watalii
Simu;0766463129
Baruapepe; amidelo@yahoo.com
Website;www.maendeleonivita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment