Saturday, February 19, 2011

Wanyama adimu wanaotafutwa na wizara ya maliasili wanapatikana ziwa Nyasa kwa wingi

Picha inamuonesha mnyama aina ya mbega weupe na weusi ambao wapo katika hatari ya kutoweka na wanapatikana mwambao mwa ziwa Nyasa hivi sasa

 Na Albano Midelo
MKOA  wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache hapa nchini ambayo imebahatika kuwa na vivutio vya kipekee na adimu ambavyo hata hivyo bado havifahamiki vizuri kutokana na kutotangazwa.

Baadhi ya vivutio hivyo ni pori la akiba la wanyama la Selous ambalo limepitia katika wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma,Makumbusho ya Taifa ya mashujaa wa Majimaji,Ziwa Nyasa,pori la Liparamba na hifadhi ya asili ya Luhira iliyopo mjini Songea.

Mkoa wa Ruvuma pia umejaliwa kuwa na misitu mizito ya asili iliyoshona na kuwa kivutio kikubwa cha viumbe hai wakiwemo wanyama,ndege,wadudu na vyanzo vya maji  ambavyo ni tegemeo kwa  uhai wa viumbe hai wote wanaoonekana na wasioonekana.

Miongoni mwa misitu hiyo ni msitu wa milima ya Livingstone uliopo wilayani Nyasa mkoani Ruvuma eneo  la pekee katika ukanda wa juu wa misitu ya miombo,lipo karibu na ziwa Nyasa,  eneo  hilo ni kivutio kikubwa cha watalii na wanyama adimu wakiwemo  pimbi,chui,nungungungu,pimbi na wanyama aina ya mbega weupe ambao wapo katika hatari ya kutoweka duniani.
 Milima ya Livingistone  ni  ya asili ina msitu mnene ambao unaishia ziwa Nyasa kwa kuungana na msitu mwingine wenye mawe unaoingia ziwa Nyasa unaofahamika kwa jina la msitu wa Ntembo uliopo katika kata ya Kihagara ambao zamani miaka kabla ya uhuru kulikuwa na wanyama wengi kama vile tembo,simba,chui,nyati pamoja na viumbe wengine wengi.
Hata hivyo kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao umekuwa unafanywa na watu kwenye mlima Ntembo baadhi ya wanyama walikimbia na kwenda katika mstu mwingine wa asili wa Liparamba ambao ni ushoroba wa wanyamapori kutoka Tanzania hadi Msumbuji.Wanyama wanaupenda msitu wa Liparamba kutokana na kuwa na msitu mnene na maji yanayotiririka kutoka mto Ruvuma ambao unaanzia milima ya Matogoro  Songea na kuendelea hadi bahari ya Hindi.

Nilifanikiwa kufika katika msitu wa  Ntembo uliopo katika kijiji cha Njambe kata ya Kihagara na milima ya Livingstone nikiwa na wadau mbalimbali wa utalii wakiwemo mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma na mjumbe wa Bodi ya utalii injinia Stella Manyanya,akiwa na diwani wa kata ya Kihagara kwa tiketi ya CHADEMA Steven Pata pamoja na  baadhi ya kikundi cha waongoza watalii  cha Ntembo Tours ambacho kinahamasisha utalii katika kata za Kihagara na Liuli mwambao mwa ziwa Nyasa.

Msitu wa Ntembo ni wa asili  unaohifadhiwa na serikali ya kata ya Kihagara ambao bado una wanyama wachache licha ya kuharibiwa.Wanyama hao adimu ambao bado wapo kwenye msitu huo  ni pimbi,sungura,nyungunyugu,ndege wa aina mbalimbali wakiwemo njiwa pori,kanga na kware.
Msitu wa Ntembo unaungana na  msitu wa milima ya Livingistone ambao upo jirani kabisa na vijiji vya kata ya Kihagara, ambapo Kutokana na mazingira mazuri ya milima Livingstone imesababisha kuwa kivutio cha viumbehai wengi wakiwemo wanyama adimu ulimwenguni yaani mbega weupe na weusi ambao wanaitwa kitalaam  white and black colobus monkey.

Afisa wanyamapori mstaafu Ngwatura Ndunguru  anabainisha kuwa colobus monkey au mbega weupe maisha yao yote wanapenda kuwa juu ya miti,vyakula wanavypenda kula vipo juu ya miti ambapo humudu kula kati ya kilo mbili hadi nne za majani maalum ambayo huota juu ya miti mingine na kwamba ni   na mara chache mno wanyama hao hushuka chini.

Ndunguru  anasema akiwa afisa wa wanyamapori  wa mkoa wa Ruvuma mwaka 1973  alitembelea msitu  wa asili wa Liwilikitesa wilayani Mbinga  ambapo alifanikiwa kuwaona mbega weupe na kwamba tangu wakati huo hakubahatika kuwaona tena wanyama hao adimu na ambao  hawapatikani popote katika ukanda wa kusini zaidi ya milima ya Livingstone baada ya kutoweka katika msitu wa Liwilikitesa milima ya Umatengo.
.
 Mbega weupe wanaishi juu ya miti na kujificha kwenye mimea inayofanana na ndevu nyeupe ambayo humwezesha mnyama huyo kutoonekana kirahisi na maadui zake akiwemo binadamu na kwamba mnyama huyo mwenye sura ya kuvutia na rangi nzuri ana tabia ya kuzaa mtoto mmoja ambaye huwa na rangi nyeupe mwili mzima hadi anapofikisha umri wa miezi mitatu ndipo anapoanza kubadilika kuwa na rangi nyeusi na kubakia na rangi nyeupe maeneo ya usoni,kichwani na shingo yenye manyoya meupe yaliochanua  na mkia wake kuwa na rangi nyeupe.

Manyoya mengi meupe aliyonayo mbega mweupe kwenye mkia na shingoni, wakati anaruka yanakuwa mfano wa mwamvuli ambao humwezesha kumudu kuruka toka mti mmoja hadi mwingine na unapomwaangalia kwenye miguu yake hana kidole gumba badala yake  ana vidole vinne tu .
  Hata hivyo diwani wa kata ya Kihagara anazitaja changamoto zinaukabili msitu huo wa asili kuwa ni uchomaji moto ovyo unaoanzia nje ya mipaka ya hifadhi ambao ukiwaka katika msitu huo kuuzima uchukua muda mrefu kutokana na msitu huo kuwa na tabaka kubwa la mabaki ya mimea takribani mita moja,uwindaji haramu wa wanyama ni changamoto nyingine na kwamba sababu kubwa ni wananchi wengi bado hawana elimu ya kutosha ya utunzaji wa mazingira na kupanda miti sehemu ambazo hazina miti ya kutosha.
Wananchi wa kijiji cha Njambe wamekiri kuwaona mbega weupe katika msitu huo na kusisitiza kuwa huwa wanaonekana alfajiri wanapoamka kwenda kutafuta chakula na majira ya jioni wanaporudi kulala na kwamba  hawaonekani wakati mwingi kutokana na kujihami na maadui hasa kabila la wamatengo ambao hutumia mbwa na silaha za jadi kuwawida ingawa tatizo la uwindaji mwambao mwa ziwa Nyasa sio kubwa kwa kuwa wananchi wanapendelea zaidi kitoweo aina ya samaki wanaopatikana kwa wingi ziwa Nyasa..
Afisa maliasili  wa wilaya ya Mbinga Peter Mdaki anasema alifanikiwa kuwaona mbega weupe katika msitu wa Liwilikitesa mwaka 1994 na kwamba wanyama hao walikuwa wachache mno kutokana na tabia ya kabila ya wamatengo kuvamia katika msitu huo kuwauwa kwa ajili ya kitoweo na mkia wake kuutumia katika ngoma za jadi na kwamba tangu wakati huo hajabahatika kuwaona tena wanyama hao adimu na kivutio cha watalii duniani.
 Mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma na mjumbe wa Bodi ya utalii Injinia Stella Manyanya  ameshauri wizara ya maliasili na utalii nchini kuelekeza nguvu zake kwenye msitu wa milima ya Livingstone kata ya Kihagara ambako wanyama aina ya mbega weupe wanapatikana ili kufanya uchunguzi na kubaini idadi ya mbega weupe waliosalia katika msitu huo wa asili pamoja na  kuimarisha jitihada za kuulinda msitu huo dhidi ya wananchi wanaofanya uharibifu wa mazingira kila mwaka ili kuunusuru msitu na viumbe hai adimu waliopo kama mbega weupe.
Tovuti;www.maendeleo ni vita.blogspot.com





No comments:

Post a Comment