Saturday, February 19, 2011

Puulu kisiwa cha utalii wa kihistoria ndani ya ziwa Nyasa

Kinachoonekana kwa mbali ni kisiwa kidogo cha Puulu chenye vivutio lukuki
Wagonjwa wa ukoma walifichwa katika kisiwa hiki tangu mwaka 1910 
Na Albano Midelo.

WASWAHILI walinena tembea uone mambo,ukibahatika kufika eneo la Liuli wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma  kuna kisiwa kimoja kidogo cha Puulu ambacho kina kina historia ya kipekee katika Tanzania na hasa ukanda wa kusini.

Kisiwa kidogo cha Puulu  ndani ya ziwa Nyasa  ambacho ili uweze kufika inabidi usafiri kwa boti au mtumbwi,kina msitu mnene,wanyama adimu kama pimbi na mazingira tofauti na nchi kavu,kisiwa kipo katika mzunguko wa maji,vitu vingi vya asili ambavyo vinaweza kuwavutia watalii wengi wa ndani na nje ya nchi ambao watabahatika kutembelea kisiwa hicho.

kisiwa cha Puulu kinatakiwa kufanyiwa utafiti na watalaamu ili kiweze kuendelezwa,kwa kuwa mwaka 1917 kisiwa hicho walikuwa wanaishi watu wenye ugonjwa wa ukoma ambao walitengwa na serikali ya kikoloni ili kuogopa wasiweze kuambukizwa watu wengine hivyo kuna utalii wa kihistoria.

Historia inaonesha kuwa mara baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961 serikali ya Tanzania wakati huo ukiwa chini ya hayati Baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere iliona ni kinyume na haki za binadamu kuwatenga wagonjwa wa ukoma hivyo mwaka 1973  walijengewa eneo jingine la Makazi wenye ukoma katika kijiji cha Ngehe kata ya Kihagara wilayani Nyasa ambao wanaishi hadi leo wakihudumiwa na serikali chini ya wizara ya afya na ustawi wa jamii.

Kwa mujibu wa wagonjwa  wenye ukoma ambao bado wanaendelea kuishi katika kijiji cha Ngehe, wakati wanahamishwa na serikali kutoka katika kisiwa hicho walikuwa wagonjwa 50 na kwamba hivi sasa  wengi wamekufa ,wamebakia wagonjwa wa ukoma wapatao sita tu ambao wana umri zaidi ya miaka 80 wakiendelea kuishi na kuhudumiwa kila kitu na serikali kama wazee wasiojiweza kwenye kambi yao ya Ngehe licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.
EMAIL;amidelo@yahoo.com
WEBSITE;www.maendeleonivita.blogspot.com

1 comment:

  1. Nilikuwa Finland, katika mji wa Turku, kwa siku kadhaa mwaka 1991 mwanzoni. Katika ziara tulizofanya maeneo ya jirani, tulionyeshwa kisiwa cha aina hiyo, ambapo walikuwa wanapelekwa wakoma. Mambo ya walimwengu yanafanana sana.

    ReplyDelete