Hapa waliposimama watu ndiyo sehemu juu ya mlima Tumbi ambako huwa wanaonekana kuku weupe ambao hawafugwi ukiwa kwa mbali lakini unapowasogelea jirani kuku hao upotea pamoja na theruji inayojitokeza na kubakia pakavu pia mlima huo una ndege watatu aina ya kware ambao idadi yao haipungui wala kuongezeka
-Kuna kuku weupe wasiofugwa
Na Albano Midelo
MKOA mpya wa Njombe una msitu unaoitwa Nyumbanitu ambao ndani yake kuna kuku weusi ambao hawafugwi na huonekana kwa nadra sana hali ambayo inaufanya msitu huo kuwa kivutio cha utalii kutokana na ukweli watalii wengi wanapenda kutembelea msitu huo ili kufanya utafiti kuhusu kuku hao weusi walionawiri ,wanaonekana mara chache lakini ni tofauti na kuku wanaofugwa.
“Nilipotembelea msitu wa Nyumbanitu mara kadhaa nilipokwenda nilijenga mashaka kama kweli kuku hao wapo sikuweza kubahatika kuwaona , lakini nilipotembelea mwezi Desemba mwaka jana nilibahatika kuonana nao uso kwa uso kuku mmoja aliyenawiri alivuka barabara kuingia msituni na baadaye akawika kama jogoo wa kawaida na akadonoa vyakula kama kuku wa kawaida baadaye akatoweka”,anasema mama Heri mkazi wa Njombe.
Moja ya maeneo ambayo ni muhimu kuyatembelea na kujifunza vitu adimu na vya kipekee ambavyo ni kivutio cha utalii ni mlima wa asili wa Tumbi uliopo katika kijiji cha Tumbi kata ya Kihagara mwambao mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma .
Mlima Tumbi ni msitu wa asili ambao unakwenda moja kwa moja hadi katika ziwa Nyasa,ukiwa katika msitu huu unaweza kuona wakati wa usiku magari ya nchi jirani ya Malawi kwa kuwa ni umbali wa takribani kilometa 70 ambapo boti hutumia saa mbili hadi nne kufika nchini Malawi kutegemea na aina ya boti iliyotumika kusafiria na ambapo kusafiri kwa kutumia mtumbwi ni mwendo saa nane .
Mzee Alen Ngongi ambaye ni mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Tumbi anasema mlima Tumbi una wanyama kama vile mbawala,swala,sungura,pimbi ambao wanapenda kuishi sehemu yenye mawe,jamii ya nyani,nungunungu,nguruwe pori pamoja na aina mbalimbali za ndege wakiwemo kuku weupe ambao wanapatikana katika sehemu maalum ya mlima huo wakiwa kwenye maji meupe ambayo yanafanana na barufu jirani kabisa na ziwa Nyasa.
“Kuku hawa weupe sana wanapendeza na kuvutia lakini katika hali ya kushangaza ukiwasogelea wanapotea lakini ukiwaona kwa mbali wanaonekana kwa wingi mimi mwenyewe nimeshawahi kuwaona mara kadhaa miaka ya nyuma nikiwa na wazazi wangu lakini miaka ya karibuni kuku hawa wamekuwa nadra sana kuonekana kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na vijana ambao wameshindwa kufuata mila unapoingia katika eneo hili ikiwa ni pamoja na kuharibu msitu huu wa asili”,anasema Ngongi.
Hata hivyo Ngingo anasema serikali ya kijiji hicho hivi sasa imeanza kuchukua hatua kali za kukabiliana na wakazi ambao wanavamia msitu huo wa asili kwa kulima,kukata miti ,kuchoma moto msitu na kuwinda wanyama waliopo katika msitu wa mlima Tumbi na kwamba anaamini utunzaji wa msitu wa mlima huo ukifanyika kuku hao wa ajabu wanaweza kurudi na kuonekana mara kwa mara kama ilivyokuwa kabla msitu haujaharibiwa.
Wakati katika msitu wa asili wa mlima Tumbi mwambao mwa ziwa Nyasa wanapatikana mamia ya kuku weupe ambao huwezi kuwakamata wala kufanya kitoweo kwa kuwa wanaonekana na kutoweka ,uchunguzi uliofanywa katika wilaya ya Njombe katika msitu mmoja jirani na Njombe mjini umebaini kuwepo kwa mamia ya kuku weusi ambao wanapatikana kwa wingi lakini unapowasogolea wanapotea hivyo huwezi kuwakamata na kwamba ni lazima kuongozwa na wazee wa mila wa kabila la wabena.
Mwenyekiti huyo mstaafu wa kijiji cha Tumbi anashauri msitu huo kuhifadhiwa na kutunzwa ili maajabu yote ambayo yalikuwepo katika msitu huo tangu miaka ya nyuma yaendelee kutokea na kuleta watalii wengi kutoka nje na ndani ya nchi kama ilivyokuwa miaka ya 1980 ambapo wazee walikuwa wanafika katika msitu huo kuomba vitu mbalimbali kama vile mvua ambayo mara baada ya kumaliza kuomba ilianza kunyesha kwa wingi.
.Msitu wa mlima Tumbi una utajiri mkubwa wa madawa ya asili ambapo waganga wa jadi kutoka sehemu mbalimbali nchini wanafika katika msitu huo kutafuta madawa mbalimbali,pia katika msitu huo zinachezwa ngoma za asili usiku kucha hata mtu anayesumbuliwa na mapepo anapelekwa katika msitu huo kuombewa hatimaye anapona kabisa.
.Mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma na mjumbe wa Bodi ya utalii injinia Stella Manyanya anasema mlima Tumbi unafaa kuingizwa katika sehemu ya makumbusho kwa kuwa katika mlima huo wanajeshi walitumia kama sehemu maalum ya kupambana na nchi ya Malawi hivyo kuwa ni sehemu ya utalii wa kishujaa na kwamba mlima Tumbi tangu zamani unatumika kama dira ya kuongozea mitumbwi ,boti na hata meli zinapotoka katika nchi za Tanzania,Msumbiji na Malawi.
Uchunguzi umebaini kuwa mlima Tumbi unafaa kwa mawasiliano yote na kutoa rai kwa makampuni ya simu nchini yakiwemo vodacom,Airtel,Zantel,Tigo pamoja na makampuni mengine kufunga minara yao juu ya mlima Tumbi hali ambayo ingemaliza kabisa tatizo la mawasiliano ya simu mwambao mwa ziwa Nyasa ambapo hivi sasa kuna baadhi ya vijiji mawasiliano hayapatikani kabisa au yanapatikana kwa shida.
Mlima Tumbi una ndege aina ya kware watatu ambao hawaongezeki wala kupungua ,wawindaji wamejitahidi kuwapiga risasi lakini wameshindwa kuwauwa ambapo ukiwa juu ya mlima Tumbi unaweza kuona fukwe nzuri ambazo huwezi kuamini kuwa zipo Tanzania na kuonekana kuwa kivuti adimu cha utalii katika mwambao mwa ziwa Nyasa.
“Nchi kama Mauritius ni kisiwa kidogo ndani ya Bahari ya Hindi ,kitu wanachojivunia ni utalii ambao wameziendeleza fukwe zao kwa kupanda miti na kutunza mazingira vizuri kiasi kwamba mtalii yeyote anapotembelea katika nchi hiyo anajisikia raha kukaa kwenye maeneo hayo hivyo ni muhimu kutunza maeneo yetu ya utalii kwa kuhakikisha hatuchomi moto pia kupanda miti na kuitunza,tukifanya hivyo watalii wengi watakuja na tutapata fedha za kutosha hivyo kukuza pato la Taifa”,anahitimisha Stella Manyanya.
0766463129
Baruapepe amidelo@yahoo.com
Website;www.maendeleonivita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment