Ndege mwenye uwezo wa kuvua samaki anapatikana ziwa Nyasa
Na Albano Midelo
ZIWA nyasa ambalo linatumiwa na nchi tatu za Tanzania,Malawi na Msumbuji limebahatika kuwa na vivutio adimu na vya kipekee vya utalii ambavyo hata hivyo inatakiwa kuviibua na kuvitangaza ili vifahamike na kuvutia watalii wengi ambao sasa wamechoka kuangalia vivutio vya wanyamapori ambavyo vinafanana sehemu nyingi kwa kuwa wanyama ni wale wale.
Kivutio kingine kikubwa na cha kipekee ambacho kinapatikana kwenye mlima Litembo kata ya Kihagara ziwa Nyasa ni mahali penye mti mmoja mrefu ambako anapenda kupumzikia ndege maarufu katika ziwa Nyasa anaitwa Ngwazi ambaye katika nchi ya Malawi amepewa heshima ya pekee kama alama ya Taifa la Malawi .
Katika nchi ya Malawi imepigwa marufuku kuwinda ndege huyo kwa kuwa kabla ya kutaja jina la Rais wa nchi hiyo ni lazima uanze na jina la ndege huyo yaani Ngwazi Kamuzu Banda ambaye ni hayati ndiye aliayeanzisha matumizi ya jina la ndege huyo na kuanzia hapo ilipigwa marufuku kumua ndege huyo na kwamba yeyote anapatikana na hatia ya kumua Ngwazi anahukumiwa kifungo gerezani.
Uchunguzi umebaini kuwa ndege aina Ngwazi ameweka kituo cha kudumu katika kilele cha mlima Litembo kilichopo katika kata ya Kihagara ambapo ndege huyo ana uwezo wa kuvua samaki akiwa juu ya mti analenga mahali ndani ya ziwa na kushuka kwa kasi ya ajabu hadi mahali alipomuona samaki na kumvua ambapo uchunguzi umebaini kuwa ndege huyo kwa kawaida huwa hamkosi samaki anayemkusidia kumvua kwa kutumia mdomo wake.
Wavuvi wa ziwa Nyasa ambao mara kwa mara wamekuwa wanamshuhudia samaki huyo akivua samaki kwa mdomo wake wanasema akishavua samaki ngwazi anapenda kulia kwenye mti maalum kwenye msitu huo wa Litembo ambao wenyeji mti huo wanauita ungwazi, pia sehemu hiyo kuna nyumba yake maalum kubwa ya miaka mingi aliyoijenga kwa vipande vya miti na nyasi ambayo anatagia mayai mawili pamoja na kutotolea vifaranga vyake.
“Eneo hili ni muhimu kwa utalii kwa kuwa ndiyo eneo pekee mwambao mwa ziwa Nyasa ambalo lina mti ambao unamlea ndege ngwazi ambaye anaheshimika sana katika nchi ya Malawi ,mti huu kwa kabila la wanyasa wa eneo hili unaitwa ndelangwai ,ndege huyo anatua katika mti huo pekee katika eneo hili,ndege huyo endapo utamsikia siku hiyo anapiga kelele sana juu ya mti wake ujue kuwa siku hiyo ziwani kutakuwa na dhoroba kali hivyo wavuvi hawaendi kuvua wanabakia nyumbani “,anasema mvuvi Martin Ndomba wa Kihagara.
Ndomba anabainisha kuwa ndege huyo akilia sana huwa anatabiri vitu vingi na kwamba siku za nyuma ndege hao walizaliana kwa wingi katika eneo hilo ambapo miaka ya hivi karibuni walijitokeza watu ambao walikuwa wanafika na kuwapiga risasi ndege hao hali ambayo imesababisha kupungua kwa kasi kwa kuwa Tanzania hakuna sheria ya kuzuia kuwauwa ndege hao ambao inaaminika nyama ya ngwazi ambao wanaishi kwa kula samaki ni tamu kuzidi nyama ya kuku.
Ndomba anayataja maajabu mengine ya ndege aina ya ngwazi kuwa akitanua mabawa yake yote mawili urefu wake ni sawa na binadamu mtu mzima aliyenyoosha mikono yake yote miwili wa kulia na kushoto na kwamba uchunguzi umebaini kuwa ndege huyo akiwa juu ya mti wake ana uwezo wa kuona samaki akiwa ziwani pamoja na kuona pande zote kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kuwaona maadui zake.
Mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma Injinia Stella Manyanya anasema sehemu ambayo ndege huyo anapenda kuishi pia inafaa kwa kufanyia picnic kutokana na kuwa na mandhari nzuri na kwamba kutokana na mlima wa Litembo kuwa mkali kutokea ziwani unafaa kwa utalii wa kupanda mlima kwa kutembea.
Baruapepe amidelo@yahoo.com
Tovuti ;www.maendeleo ni vita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment