Saturday, February 19, 2011

Ntembo hifadhi pekee ya wanyamapori ya asili inayoanzia ndani ya ziwa Nyasa

Mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma na mjumbe wa Bodi ya Utalii Injinia Stella Manyanya  akiwa juu ya mawe ya hifadhi ya wanyama ya mlima Ntembo ambayo inaanzia ziwa Nyasa pamoja na vijana wanaongoza watalii wa kikundi cha Ntembo tours
Ntembo ndiyo chanzo cha pori la wanyama la Liparamba Mbinga
Na Albano Midelo

WATU tulio wengi tumezoea kuona au kusikia hifadhi za wanyamapori za asili zikiwa katika maeneo ya misitu minene,nyasi,mbuga pamoja na uoto wa asili katika maeneo ya tambarare au milimani .

Sio jambo la kawaida kuona au kusikia hifadhi ya wanyama pori ikiwa imeanzia ndani ya ziwa au bahari ,ingawa kwenye maji kuna wanyama na viumbe ambao wanapenda kuishi kwenye mazingira kama hayo wakiwemo mamba,viboko,samaki wa aina mbalimbali pamoja na viumbe wengine wa majini.


Katika hali inayoonesha maajabu ya mwenyezi Mungu aliyoyafanya wakati anaumba ulimwengu huu ni hifadhi ya wanyamapori ya Ntembo iliyoanzia ndani ya ziwa Nyasa  katika kijiji cha Njambe kata ya Kihagara wilayani Nyasa mkoani Ruvuma  ambayo licha ya kufanyiwa uharibufu mkubwa wa mazingira bado ni kivutio cha utalii adimu hapa nchini.

Hifadhi ya wanyamapori ya Ntembo inaanzia ziwa Nyasa ikiwa imesheheni mawe mengi ya kuvutia,ikiendelea hadi kwenye milima ya Ntembo ambayo inaaminika miaka ya 1960 hifadhi hiyo ya asili ilikuwa na wanyamapori wengi wakiwemo tembo,simba,nyati,pundamilia,twiga,swala na wanyama adimu aina ya pimbi ambao wanapendeleo kuishi zaidi kwenye milima ya mawe pamoja na aina mbalimbali za ndege,wadudu na samaki.

Hata hivyo kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira ambao umefanyika katika hifadhi ya  mlima Ntembo imesababisha kadri miaka ilivyokuwa inakwenda wanyama wengi katika hifadhi hiyo kuhama katika mlima huo na kukimbilia kwenye pori la asili la wanyama pori la Liparamba wilayani Mbinga ambalo ni ushoroba wa wanyama kutoka Tanzania hadi Msumbiji. Hata hivyo ukweli unabakia kuwa pori la wanyama la Ntembo ndiyo limezaa mbuga ya Liparamba iliyopo wilayani Mbinga.

Uchunguzi  uliofanywa kwenye hifadhi hiyo inayoanzia ndani ya ziwa Nyasa umebaini kuwa mlima wa asili wa Ntembo bado una wanyama wa asili kama pimbi ambao wapo wengi kutokana na kupenda mazingira ya milima ya mawe ambayo imeingia hadi ziwa Nyasa,pia kuna wanyama wengine kama nungunungu,Pendu,swala,mbega weupe,njiwa pori,kware, kanga na aina mbalimbali za samaki  bado wanapatikana kwenye hifadhi hiyo adimu na ya kipekee nchini.Hifadhi ya wanyama ya Ntembo ina mandhari nzuri zinazofaa kufanyia picnic pamoja na kupigia picha na kufanya utalii wa kuogelea katika ziwa Nyasa.

  Stephano Komba mwenye mzee mkongwe mwenye umri wa miaka 85 katika kijiji cha Ntembo anasema kuanzia miaka ya  1950 hadi 1970 katika msitu wa mlima wa Ntembo kulikuwa wanyama wengi wakiwemo simba,tembo,swala ambapo hadi sasa katika vijiji vya kata ya Kihagara vikiwemo Mango,Tumbi,Njambe bado kuna aina mbalimbali za wanyamapori wakiwemo chui,pimbi,swala,sungura,nguruwe,mbega weupe  pamoja na aina nyingine za wanyama.

Uchunguzi umebaini kuwa wanyama aina ya pimbi wamezaliana kwa wingi katika milima ya Ntembo ambayo imeanzia katika milima hiyo na kuingia hadi ziwa Nyasa hivyo kuwa kivutio cha wanyama aina ya pimbi ambao wanapenda kuishi katika mbuga ya asili yenye mawe makubwa iliyopo jirani na ziwa.

Mjumbe wa Bodi ya utalii na mbunge wa viti maalum wanawake mkoa wa Ruvuma injinia Stella Manyanya anasema anaamini wengi ambao watabahatika kutembelea eneo la mlima Ntembo wataona vivutio vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine yeyote katika mkoa wa Ruvuma .
Tovuti ;www.maendeleo ni vita.blogspot.com


No comments:

Post a Comment