Na Albano Midelo.
VYANZO vya maji katika maeneo mbalimbali nchini vimekuwa vikiendelea kufanyiwa uharibifu mkubwa licha ya serikali kupiga marufuku shughuli zozote ambazo zinaharibu vyanzo hivyo.
Serikali mnamo mwaka 2002 ilipitisha mwongozo wa namna ya kutunza vyanzo vyote vya maji vilivyopo ili visipotee wala kuchafuliwa.Sera hiyo ya maji inalenga kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vilivyopo vinatunzwa,kulindwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaozingatia uwiano wa mahitaji ya viumbehai wote wakiwemo binadamu,wanyama,mimea,wadudu pamoja na viumbe hai wote ambao hawawezi kuishi bila maji.
Ili kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa na kuwa endelevu kwa manufaa ya viumbehai vya sasa na vijavyo ni vema kutotupa wala kumwaga uchafu au kemikali za sumu karibu na vyanzo hivyo,,kutochoma misitu ovyo,kupanda miti inayofaa au miti rafiki kwa maji karibu na vyanzo vya maji,kutojenga vyoo karibu na vyanzo vya maji,kutochimba mchanga au madini ndani au karibu na vyanzo hivyo pamoja na kutosafishia madini au kitu kingine katika vyanzo.
Katika hali ya kusikitisha baadhi ya wananchi wanafanya uvuvi haramu kwa kutumikia kemikali zenye sumu katika mto Ndumbi ambao unamwaga maji yake ziwa Nyasa hali ambayo inahatarisha usalama wa wakazi zaidi karibu 3000 wanaishi katika kijiji cha Mkili pamoja na vijiji vingine jirani kwa kuwa wanategemea mto huo kwa maji ya kunywa,kuoga,kupikia,kumwagilia bustani pia kutaharisha maisha ya viumbe hai.
Wananchi wanaoishi kwenye milima ya Livingstone iliyopo mwambao mwa ziwa Nyasa ambako mto Ndumbi unaanzia wanadaiwa kufanya uharifu wa kumwaga sumu mbalimbali zikiwemo madawa ya kuulia wadudu kwenye kahawa yakiwemo gramakson,DDT,Blue copper,mbolea ya urea pamoja na sumu za kienyeji aina ya mtunyungu ambazo zinauwa samaki pamoja na viumbe wengine kwenye mto huo.
Uchunguzi umebaini kuwa wakazi wa Mkili ,kijiji ambacho kipo mwambao mwa ziwa Nyasa wanaathirika na madawa yanayomwaga kwenye mto huo na kwamba athari zinakuwa kubwa zaidi katika kipindi cha kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba kila mwaka wakati ambao kina cha maji katika mto huo kinakuwa kimepungua katika kiwango kikubwa.
Ikumbukwe kuwa katika kijiji cha Mkili wananchi wanategemea mto huo kwa kila kitu ikiwemo maji ya kunywa hivyo sumu zinazomwagwa kwenye mto huo zimeleta athari kubwa ikiwemo wananchi kuugua magonjwa ya homa za matumbo wakati wote na wengine wameripotiwa kupoteza maisha.
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka jana pekee katika kipindi cha mwezi Septemba hadi Novemba watu watano wamepoteza maisha katika kijiji cha Mkili kati yao wanafunzi watatu baada ya kupata magonjwa ya homa za matumbo yanayotokana na unywaji wa maji yenye kemikali katika mto Ndumbi au kula chakula ambacho kimeathirika na kemikali hizo.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa wanaoathirika sio wakazi wa kijiji cha Mkili pekee bali wakazi wa vijiji vingine vya jirani mwambao mwa ziwa Nyasa wanaolazimika kunywa maji ya sumu za kemikali za viwandani na mimea vikiwemo vijiji vya Ngumbo,Yola,Mbuli,Ndonga,Liwundi na Ngumbo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wanakunywa maji ambao sio safi na salama.
Tilia Woka ni mkazi wa kijiji cha Mkili ambaye anaishi eneo la milimani jirani na mto Ndumbi unapoanzia anasema wakazi wa kijiji cha Mahande ndiyo wanaofanya vitendo vya kutia kemikali zenye sumu kwa lengo la kuvua samaki waliopo kwenye mto Ndumbi.
“Wavuvi hao haramu kila mwaka kwa siri wanatia sumu katika eneo la chanzo cha mto kisha dawa hiyo kadri maji yanavyoshuka kuelekea ziwani ijichanganya na kuwalewesha samaki huku wengine wanakufa ,wavuvi hao hufuata mto huo huku wakiwakamata samaki waliolewa na kuwafanya kitoweo”,anasema.
“Wavuvi hawa haramu ni wajanja sana wanawahi asubuhi majira ya saa 12 wakiwa katika kikundi na kuweka dawa kwenye mto Ndumbi ,dawa hiyo inafika ziwani majira ya kumi jioni,wao hawafiki hadi ziwani wanakuwa wameshapata samaki kabla ya kufika ziwani,wengi wanaokula samaki hao wanalalamika kuumwa matumbo na tunaomba serikali iongeze ulinzi ili kuwakamata waharifu hawa wanaohatarisha maisha ya wananchi’,anasema Moses Hyera mkazi wa kijiji cha Mkili.
Januari Haule mkazi anayeishi kando kando mwa mto Ndumbi katika kijiji cha Mkili mwambao mwa ziwa Nyasa anasema wakazi wa eneo hilo wanaathirika kutokana na madawa yanawekwa kwenye mto huo ikiwa ni pamoja na wananchi kuugua matumbo,kupoteza maisha na mifugo mingi inakufa na kusababisha umaskini mkubwa .
“Mwaka 2010 wavuvi hao haramu wameweka kwa awamu tano dawa hizo zenye kemikali na kuleta athari kubwa hasa kwenye mazalia ya samaki aina ya magege,mbelele ambao wanapenda kuzaliana mahali ambapo maji ya mto yanaingia ziwa Nyasa hivyo wanauwa samaki wengi kwenye mto Ndumbi samaki wanatoweka hasa mwaka 2010 hali ilikuwa mbaya zaidi”,anasema.
Utafiti ambao umefanywa katika mto Ndumbi umebaini kuwa maji yake hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu pamoja na viumbe wengine kwa kuwa yameonekana yana kemikali mbaya za sumu hasa kutokana na na kumwaga sumu mbalimbali zikiwemo zile zinazodaiwa kutoka katika mabomba ya maji taka yaliotegwa katika hospitali ya misheni Litembo ambayo yanamwaga maji kwenye mto huo na kuishia ziwa Nyasa.
Mganga mkuu wa kituo cha afya Mkili Thomas Magulilo anasema maji katika mto Ndumbi hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu na kwamba wananchi wa kijiji hicho waliagizwa kuhakikisha kuwa wanachemsha maji hayo kabla ya kunywa ambapo uchunguzi umebaini kuwa asilimia 99 ya wakazi wa kijiji hicho wanakunywa maji kutoka kwenye mto Ndumbi au ziwa Nyasa bila kuchemsha wala kuweka dawa za kuyatibu kama water guard.
“Asilimia 90 ya watu wanaofika kupima katika kituo hiki wanagundulika kuwa na vijidudu vya ugonjwa wa homa za matumbo hivyo hali ni mbaya,katika kijiji kizima hakuna kisima cha maji,wananchi tunawaelimisha kuchemsha maji wengi wanadai hayana radha wanaendelea kunywa maji bila kuchemsha”,anasema mganga wa kituo cha afya.
Bosko Ndimbo mkazi wa kijiji cha Mahande anasema katika kijiji hicho watu wengi wanatumia mbolea aina ya urea kuulia samaki kwenye mto huo hivyo mifugo mingi inateketea iwapo inakula vyakula vilivyochanganywa na mbolea ya urea pamoja na dawa za asili aina ya utupa.
“Mwenyekiti wa kijiji cha Mkili Kisika Mahoya anasema utiaji wa sumu sio tu kwamba unafanyika kwenye mto Ndumbi pekee bali pia unafanyika kwenye mito mingine inayopita katika kijiji hicho inayoitwa Mnywamaji na Chipindi inayomwaga maji yake ziwa Nyasa.
Imanuel Kipera ni kaimu afisa mtendaji wa kata ya Ngumbo anasema madawa ya kahawa yalipigwa marufu kutumika hata hivyo baadhi ya wananchi ambao wamezificha dawa hizo ndiyo wanatumia kufanya uvuvi haramu kwenye mito na kuhatarisha maisha ya viumbe hai.
“Mimi kitaaluma ni afisa wa mifugo na kilimo,madhara ya madawa hizi kwa samaki ni kwamba kuanzia eneo ambalo unakuwa umemwaga sumu hadi mto unakoelekea viumbe wote wanaathirika kuanzia samaki,mifugo na watu ambao wanatumia maji hayo,mtu anayekula samaki wenye sumu anaweza kupata magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo na kansa ambayo hutokea baada ya muda mrefu”,anasema.
Hata hivyo anasisitiza wananchi kupatiwa elimu ili kutambua afya ni jambo bora zaidi kuliko kupata kitoweo na kwamba kuna baadhi ya madawa ya kahawa ya maji ambayo wanayatumia yana athari na madhara makubwa na kwamba serikali ya kata inachukua hatua za kukabiliana na wavuvi hao haramu ambao wanafanya kazi hiyo kwa siri na hata wengine wanatia dawa hizo usiku.
“Kwa kweli tatizo hili la kuweka sumu kwenye maji ambayo yanategemewa na wakazi zaidi ya 3000 katika kijiji cha Mkili ni zito ,wananchi wengi wanaugua ugonjwa wa homa za matumbo ,baadhi yao wanafariki kila mwaka,kata yetu haina kisima hata kimoja wala bomba tunagemea kupata maji ya mito na ziwa,tunaomba serikali yenye nguvu itusaidia
Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela ameahidi ofisi yake kuendelea kuwaelimisha wananchi umhimu wa kuchemsha maji pamoja na kufuatilia athari ambazo wanazipata wananchi wa kijiji cha Mkili ambao wanaugua homa za matumbo kutokana na kutumia maji yenye kemikali tena bila kuchemshwa.
“Naomba wananchi wa mwambao mwa ziwa Nyasa wazingatie maagizo ya watalaamu wa afya hasa kuhakikisha kuwa wanachemsha maji,waachane na mila potofu eti maji ya kuchemsha hayana radha”,alisisitiza.
Email: amidelo@yahoo.com,
Tovuti;www.maendeleonivita.blogspot.com
No comments:
Post a Comment