Monday, February 28, 2011

Waziri wa maliasili na utalii azindua mnara wa mashujaa wa majimaji Songea




Picha inamuonesha waziri wa maliasili na utalii Ezekiel Maige akiweka ngao kwenye mnara mpya wa mashujaa wa vita vya majimaji ulijengwa na makumbusho ya Taifa picha na Albano Midelo
Na Albano Midelo.
WAZIRI wa utalii na maliasili Ezekile Maige amezindua mnara wa mashujaa wa vita vya majimaji uliojengwa  katika eneo la Songea klabu ambao umegharimu shilingi milioni 16.

Waziri Maige alifanya uzinduzi huo jana katika eneo ambalo walinyongwa mashujaa wa vita vya majimaji wapatoa 67 kwenye kilele cha  tamasha la utalii,utamaduni na kumbukizi ya vita vya majimaji ambalo hufanyika kila mwaka Februari 27 katika makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini hapa. 

Akizungumza mara baada ya kuzindua mnara huo ambao umejengwa na makumbusho ya Taifa waziri Maige ameahidi wizara yake kuongeza  kasi na msukumo kwa kuongeza vivutio vya utalii hasa utalii wa kihistoria na utamaduni.

“Nachukua nafasi hii kuwapongeza  kwa kujenga mnara wa kisasa mahali waliponyongewa mashujaa wetu wa vita vya majimaji,naamini kuwa mnara  huu ambao tumeuzindua leo wenye majina ya mashujaa pamoja na kumbukumbu nyingine  utaongeza hadhi ya makumbusho haya na mji wa Songea kuvutia watalii”,alisisitiza.

Hata hivyo waziri Maige ametoa wito maalum wa kuyatambua na kuyaweka vizuri maeneo yote ya kihistoria yaliyopo kusini mwa Tanzania ili yaweze kutumika katika kutolea vielelezo vya historia ya nchi kuanzia vita vya majimaji,vita vya ukombozi wa kusini mwa Afrika hususani makambi ya wapigania uhuru,biashara ya utumwa na watumwa pamoja na maeneo ya kimila yanayotumika katika shughuli za kiutamaduni ili kuvutia watalii wengi baada ya kutangazwa.

Naye mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma ameipongeza wizara ya maliasili na utalii kwa kukipandisha hadhi kituo cha makumbusho ya Majimaji kuwa cha kitaifa tangu mwaka jana pamoja na kuutangaza rasmi mji wa Songea kuwa mji wa kihistoria na kishujaa hali ambayo alisema imeongeza idadi ya watalii.

Hata hivyo Dk.Ishengoma alisema mkoa wa Ruvuma unaweza kufanya  mabadiliko makubwa katika sekta ya utalii kutokana na ukweli kuwa mkoa huo una vivutio lukuki vya utalii ambavyo bado havijatangazwa kikamilifu ili kuvutia watalii na wawekezaji.

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa makumbusho ya Taifa Jackson Kihiyo aliitaja mikakati na maazimio ya kuendeleza sekta ya utalii kusini mwa Tanzania kuwa ni pamoja na kuboresha vivutio na maeneo ya utalii,kuyatambua rasmi maeneo yote ya kihistoria yenye vivutio,kutoa elimu ya utalii kwa umma,kujitangaza kwa kutumia vyombo mbalimbali na kuboresha miundombinu kuelekea maeneo ya utalii.

Sherehe hizo za kumbukizi ya vita vya majimaji zimehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo kutoka nchi jirani ya Msumbuji,wakuu wa mikoa ya Iringa,Rukwa,Tabora,Tanga,Kilimanjaro,Morogoro,maprofesa kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam,jeshi la wananchi wa Tanzania pamoja watalaamu na wananchi wa kawaida.

Picha inamuonesha waziri wa maliasili na utalii Ezekile Maige akizindua mnara wa mashujaa wa vita vya majimaji nyuma ya ukumbi wa Songea klabu ambako walinyongwa mashujaa 67 picha na Albano Midelo
 Baruapepe amidelo@yahoo.com

No comments:

Post a Comment