-Wanawake 250,000 hufariki kila mwaka
Na Albano Midelo.
WANAWAKE ni kundi mojawapo muhimu katika jamii hasa kutokana na ukweli kuwa mwanamke ndiyo nguzo ya familia kwa kuwa anahusika zaidi katika malezi ya familia.
Picha kulia inamuonesha mke wa Rais Salma Kikwete akikabidhi kitanda kwa ajili ya akinamama wajawazito wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Pamoja na ukweli huo mwanamke hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo matatizo wakati wa kujifungua ambapo kila mwaka akinamama zaidi ya 8000 hufariki kutokana na matatizo ya uzazi.
Kana kwamba hilo halitoshi wanawake pia wanakabiliwa na tatizo jingine la kiafya ambalo ni ugonjwa wa kansa ya kizazi ambayo inaelezwa ndiyo kansa inayoongoza katika kusababisha vifo vitokanavyo na kansa kwa akinamama waliopo katika nchi zinazoendelea.
Utafiti unaonesha kuwa akinamama zaidi ya 500,000 hupatwa na ugonjwa wa kansa ya uzazi kila mwaka ulimwenguni,ambapo kati ya hao akinamama 250,000 hufariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kutoka katika hospitali ya misheni ya Peramiho iliyopo nje kidogo ya mji wa Songea mkoani Ruvuma Dk.Gaudence Komba ansema hapa nchini takwimu zinaonesha kuwa kansa au saratani ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo.
Dk.Komba anabainisha saratani nyingine ambazo zinafuatia katika kusababisha vifo kwa wanawake kuwa ni pamoja na saratani inayoitwa kitaalamu Kapodsarcoma na saratani ya matiti.
Hata hivyo anasema zaidi ya asilimia 80 ya wagonjwa wa saratani ya kizazi hufika katika vituo vya kutolea huduma za afya wakiwa wamechelewa yaani ugonjwa ukiwa tayari umeenea sana jambo ambalo anasema kutibika kwake inakuwa vigumu sana.
Daktari huyo bingwa wa magonjwa ya wanawake anasisitiza kuwa ugonjwa wa saratani ya kizazi ukiwa katika hatua za mwanzo unaweza kutibika kabisa kwa njia ya upasuaji au kwa njia ya mionzi.
Hata hivyo kulingana na Dk.Komba,katika nchi zilizoendelea uchunguzi wa awali uonafaywa mara kwa mara katika nchi hizo,umepunguza kabisa saratani ya uzazi kwa akinamama na kwamba njia inayotumika kufanya uchunguzi iitwayo kitaalum Cytology,imeonekana kuwa ni ngumu kutumika katika nchi za dunia ya tatu kama Tanzania.
Anabainisha zaidi kuwa njia hiyo inahitaji wataalamu wa hali ya juu hali ambayo anasema inasababisha gharama ya huduma hiyo kuwa ni kubwa na hatimaye kushindwa kufanyika katika nchi zinazoendelea.
Kutokana na hali hiyo shirika la afya duniani(WHO) kwa kushirikiana na wadau wengine wa afya ulimwenguni limegundua njia inayoonekana kuwa mbadala kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania,njia ambayo kitaalaum inaitwa visual inspection with acetic acid(VIA) ambapo huduma hiyo inaweza kutolewa hata katika vituo vya afya na zahanati kwa kuwatumia wahudumu waliopo kama wauguzi na waganga.
Dk.Komba anasema tayari WHO inasaidia serikali za nchi mbalimbali kuanzisha na kuendeleza huduma hiyo ambapo wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ni miongoni mwa wilaya hapa nchini zilizobahatika kuanzisha huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya afya za wanawake.
Licha ya saratani hiyo ya kizazi ambayo inaongoza kwa kusababisha vifo vingi vya wanawake ulimwenguni,saratani nyingine ambayo inatajwa kuwa ni miongoni mwa saratani zinazowapata wanawake ni saratani ya matiti.
Mawasiliano albano.midelo@gmail.com
No comments:
Post a Comment