Tuesday, August 23, 2011

SAUT kufungua tawi jipya Songea

Picha inamuonesha Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega ambaye amesimama mbele ya jengo la utawala la chuo kikuu  cha mtakatifu Agustino SAUT tawi la Songea
Na Albano Midelo,Songea.
CHUO kikuu kishiriki cha  SAUT Mwanza yaani Songea SAUT university college kinatarajia kufunguliwa rasmi katika jimbo kuu la Songea kati ya mwezi Desemba na Februari mwakani.
Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega akizungumza na kiongozi katika mahojiano maalum ofisini kwake mjini hapa alisema jimbo kuu katoliki la Songea limetoa majengo matano ambayo  yameazimwa na SAUT kwa ajili ya chuo kikuu hicho.
Mhashamu Mtega alibainisha kuwa mchakato wa kuyafanyia ukarabati majengo hayo unaendelea ambapo aliyataja majengo ambayo yametolewa na jimbo kuu la Songea kwa SAUT kuwa ni pamoja na jengo la redio Maria ambalo litatumika kwa ajili ya utawala na baadhi ya vyumba kulala wanachuo.
Majengo mengine aliyataja kuwa ni majengo yaliotumika kuhifadhiwa  vitu mbalimbali,majengo  mawili ambayo yalikuwa kumbi za Donbosko za vijana pamoja na jengo la chekechea  na kwamba chuo hicho kinatarajia kuanza na wanachuo wasiopungua 500.
’’Kwa kuanzia chuo kikuu kishiriki cha Songea SAUT kitaanza na masomo ya sayansi za jamii kikiwemo kitivo cha elimu pia chuo hicho kitatoa masomo katika kitivo cha tiba ambapo kanisa limetoa majengo yaliyotumika kwa ajili ya wagonjwa wa ukoma katikia kijiji cha Morogoro Peramiho’’,alisisitiza.
Hata hivyo alisema mradi huo wa elimu katika chuo kikuu kishiriki cha Songea SAUT   unashirikisha Baraza la maaskofu katoliki Tanzania na jimbo kuu katoliki la Songea na kwamba  siku za usoni vitivo vingine vinatarajia kuanzishwa  lengo likiwa  ni kuinua elimu ya juu kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine ya maendeleo katika elimu Askofu mkuu Mtega alisema watawa wa  shirika la masista wa Imakulata DMI kutoka nchini India wanatarajia kuanzisha chuo kikuu cha kilimo university college  katika eneo la Ruhuwiko mjini Songea.
Alisema chuo kikuu hicho ambacho kinaanza kwa ushirikiano wa watawa wa DMI na chuo kikuu cha nchini India  kinatarajia kuanza rasmi Januari 2012 ambapo madarasa matano tayari yamekamilika na hivi sasa wahadhiri sita kutoka nchini India tayari wamewasili nchini.
Kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho cha kilimo kutalifanya shirika hilo la watawa wa DMI kuwa na vyuo vikuu viwili baada ya awali kuanzisha chuo kikuu sayansi ya kompyuta cha mtakatifu Joseph chenye matawi yake Dar es salaam na Songea.
Hata hivyo alibainisha kuwa hivi sasa kinachosubiriwa ni kupata kibali kutoka Tume ya vyuo vikuu nchini TCU ili  chuo hicho kiweze kuanza rasmi pamoja na kupata usajiri  toka serikalini.
Mawasiliano andika albano.midelo@gmail.com





No comments:

Post a Comment