Sunday, February 5, 2012

.Namtumbo kupata umeme wa TANESCO

Pichani aliyevaa tshirt nyekundu ni injinia wa TANESCO katika kituo kipya cha Namtumbo Timoth Ramadhani akitoa maelezo kuhusu nguzo zaidi ya 220 kwa ajili ya kusambazia umeme mkubwa zikiwa zimewekwa  eneo ambalo zitajengwa ofisi za TANESCO wilaya ya Namtumbo kazi ya kuchimbia nguzo za umeme mdogo inaendelea.

Na Albano Midelo
MJI wa Namtumbo uliopo mkoani Ruvuma unatarajia kupata umeme kutoka shirika la ugavi wa umeme Tanzania TANESCO ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Kaimu meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma Haruna Mwachula alisema kuwa   wafanyakazi wa TANESCO  tayari wapo Namtumbo wanaendelea na kazi ya kusambaza nguzo za umeme mkubwa  pamoja na kutandaza nyaya.
“Wiki iliyopita gari liliosheheni nguzo za umeme  likiwa na wafanyakazi wanaendelea na kazi ambayo inatarajia kukamilika kabla ya mwezi Aprili mwaka huu,hivyo tunatarajia mji wa Namtumbo utakuwa na umeme ifikapo mwezi Mei mwaka huu’’alisisitiza.
Injinia wa  kituo kipya cha TANESCO wilayani Namtumbo Timoth Ramadhani amesema nguzo za kusambazia umeme mkubwa  157 zimewasili makao makuu ya mkoa na kwamba kati ya hizo nguzo 120 tayari zimefika Namtumbo na tayari kazi ya kuchimbia nguzo za umeme inaendelea kufanyika.
Kwa mujibu wa injinia huyo nguzo za kusambazia umeme mdogo kwa ajili ya wateja  zipatazo 88 zimefika mjini Namtumbo na kwamba nguzo zinazohitajika ili kukidhi  mahitaji halisi  ni nguzo 300.
“Mashine ambayo itatumika kwa ajili ya kuzalishia umeme mjini Namtumbo yenye uwezo wa kuzalisha kilowati 450 imefadhiliwa na wakala wa umeme vijijini,transifoma zilizonunuliwa ni sita na kila transifoma ina uwezo wa kutumia nguzo 14 za uzalishaji wa umeme mdogo,hata hivyo ili umeme uweze kusambazwa vizuri  transfoma moja inahitaji kati ya nguzo 40 hadi 80’’,alisema.
Kuhusu mkoa wa Ruvuma kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa,kaimu meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma Mwachula alibainisha kuwa  upembuzi yakinifu umekamilika na hivi sasa kinachoendelea ni    maandiko ya mradi huo yamepelekwa katika Baraza la Mazingira la Taifa NEMC kwa ajili ya tathimini ya mazingira .
“Tunaamini Propasal hiyo itaruhusiwa na NEMC wakati wowote   mwaka huu,ikisharuhusiwa kazi ya   kutoa umeme wa gridi kutoka Makambako hadi Songea inatarajia kuchukua miaka mitatu hadi kukamilika’’alisema.
albano.midelo@gmail.com

No comments:

Post a Comment