Pichani ni Mwenyekiti wa chama cha kuweka na kukopa cha walimu wa manispaa ya Songea Martin Challe
Na Albano Midelo
JINAMIZI huenda likaikumba Saccos ya walimu wa manispaa ya Songea kutokana na kile ambacho kinaonekana kuwa ni baadhi ya wanachama wake kutoridhika na uendeshaji wa chama hicho na kukifanya chama kuwa njia panda huku viongozi wake wakionekana kukalia kuti kavu.
Baadhi ya wanachama wakizungumza kwenye mkutano mkuu wa 14 kwenye ukumbi wa Songea Club jana wameyataja baadhi ya mambo ambayo yamekuwa kero kubwa kwa wananchama wake ikiwemo kushindwa kutoa fedha za mikopo kulingana na maombi ya wanachama hali ambayo inaleta usumbufu mkubwa kwa wanachama.
Mwalimu Ajaba Chitete ambaye ni mwanachama katika saccos hiyo amedai kuwa kitendo cha saccos hiyo kushindwa kutoa mikopo kwa wanachama wake kwa wakati na kutoa kiwango ambacho hakilingani na maombi ya mwanachama kumesababisha idadi kubwa ya wanachama kujiondoa uanachama na kuhamia kwenye vyama vingine .
Wanachama hao pia wamedai uongozi uliopo madarakani umeshindwa kusimamia ujenzi wa mradi wa jengo lao ambao walidai unatia mashaka kutokana na mradi huo kutumia muda mrefu na fedha nyingi za wanachama zinaendelea kutumika bila mradi wa kitega uchumi kukamilika.
Baadhi ya wanachama hao walidai kwenye mkutano huo kuwa wana mashaka na matumizi mabaya ya fedha zao hasa kwenye mradi wa ujenzi wa jengo lao la kitega uchumi ambao licha ya kutumia muda mrefu hadi sasa umefikia hatua ya kupiga ripu.
Katika mkutano huo uongozi wa Saccos hiyo umewaomba wanachama kuidhinisha mkopo wa shilingi milioni 150 ili kukamilisha ujenzi wa kitega uchumi cha walimu kinachojengwa katika eneo la Majengo mjini Songea.
Mwenyekiti wa Saccos hiyo Martin Challe alizitaja changamoto ambazo zinakikabili chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1998 ni pamoja na uwezo mdogo wa rasilimali fedha ambao unasababisha chama kuyumba na kushindwa kutoa huduma za fedha zinazohitajika.
Changamoto nyingine alizitaja kuwa ni wimbi kubwa la wanachama wake kuondoka pamoja na ushirikiano mdogo baina ya wanachama na viongozi.
Chama cha kuweka na kukopa Saccos cha walimu katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma mwezi uliopita kimesambaratika kufuatia upotevu wa shilingi milioni 400 ambazo hadi sasa haijafahamika zimekwenda wapi.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment