Pichani mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.
Na Albano Midelo
HALI ya amani na usalama imerejea katika mji wa Songea baada
ya serikali kwa kushirikiana na wananchi kudhibiti mauaji ya watu yaliokuwa
yanafanyika kwa mfululizo na kuleta hofu .
Tangu mwanzoni mwa mwaka huu yamekuwa yakitokea mauaji
mfululizo ya watu ambayo yalidaiwa yanatokana
na imani za kishirikina ambayo yamesababisha vifo vya watu 14 hali
ambayo ilizua hofu na mashaka kwa wakazi wa mji wa Songea.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu wiki hii
amezungumza na waandishi wa habari
ofisini amesisitiza kuwa mji wa Songea sasa umerejea katika hali amani na utulivu na kwamba hakuna tena matukio ya mauaji tangu .
“Serikali imefanikiwa kuwakamata karibu watuhumiwa wote
waliohusika na mauaji yaliyosababisha vifo vya watu 14 na hivi sasa watuhumiwa
hao wakiwemo askari wanaotuhumiwa kuuwa watu wawili kwa risasi kwenye
maandamano wapo mbele ya vyombo vya sheria na upelelezi zaidi
unaendelea’’,alisisitiza.
Amewatahadharisha
wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi
pamoja na kuacha kufanya maandamano yasiokuwa ya vibali kwa kuwa
yanachangia kuleta ghasia na uvunjifu wa amani ambao unaleta athari na kwamba
wanapokuwa na malalamiko au kero wazifikisha kwa viongozi wao kwa njia halali.
Hata hivyo uchunguzi ambao umefanywa na gazeti hili katika
viunga mbalimbali vya mji wa Songea umebaini kuwa licha ya mkuu wa mkoa kudai
hali ya amani na utulivu imerejea,bado wananchi wengi wanaishi kwa hofu na
mashaka kuhofia usalama wao.
Mohamed Kudeka ni mkazi wa Msamala mjini hapa anadai
kuwa wakazi wa eneo hilo bado wanaogopa
kwenda kuweka mbolea na kufanya palizi kwenye mashamba yao kuhofia kuuwawa na
kwamba mashamba mengi ya mahindi
yamedumaa kwa kukosa matunzo.
Hamza Abdalah mkazi wa Matarawe anadai kuwa nguvu ya wananchi kufanya maandamano ingawa
hayakuwa halali imesaidia kuiamsha
serikali kufufua ulinzi shirikishi kwenye mitaa yote ya mji wa Songea na kwamba
amani na utulivu iliyozoeleka katika mji wa Songea bado haujarudi katika hali
yake ya kawaida.
“Baadhi ya maeneo klabu za
usiku zinafungwa kabla ya saa tatu usiku mfano maeneo ya
Mkuzo,Matarawe,Ruhuwiko,maeneo ya katikati ya mji klabu za usiku kama Ikweta, zinaendelea kutoa huduma zaidi ya saa tano usiku,hata
hivyo wateja ni wachache ukilinganisha na hali kabla matukio ya
mauaji’’,alisema Abdalah.
Madereva pikipiki waliohojiwa Rashid Juma,John Komba,Frank
Haule,Hamis Rajabu na Musa Ngongi walidai kuwa hawakubali kuwabeba abiria
wasiwafamu vizuri majira ya mchana na usiku kutoka katikati ya mji kuelekea
pembezoni kwa sababu bado wana hofu kuporwa pikipiki na usalama wa maisha yao.
Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Sabaya alisema serikali
imejipanga kila kata katika mji wa Songea kuwatafutia sare maalum madereva wote
wa pikipiki ili kuwatambua maeneo wanayotoka
hali ambayo itasaidia kuzuia uharifu unaofanywa na baadhi ya madereva wa
pikipiki au abiria wanaowabeba.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment