Monday, April 2, 2012

RPC yapata viongozi wapya

                                        
                                               
Na Albano Midelo
KLABU ya  waandishi wa habari mkoa wa Ruvuma imejipatia viongozi wake wapya ambao wataiongoza  klabu hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Viongozi hao wapya wamechaguliwa kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa EMAU Peramiho nje kidogo ya mji wa Songea na kusimamiwa na mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Songea Richard Mbambe.
Waliochaguliwa kwenye uchaguzi huo ni pamoja na mwenyekiti Andrew Kuchonjoma,makamu mwenyekiti Leticia Nyoni,katibu mkuu Andrew Chatwanga na katibu mkuu msaidizi amechaguliwa kuwa ni Julius Konala.
Wengine ambao wamechaguliwa ni mweka hazina mkuu Joyce Joliga,mweka hazina msaidizi Imanuel Msigwa,wajumbe wanne wa kamati ya utendaji ni Geofrey Nilahi,Cresensia Kapinga,Mpenda Mvula na Joseph Mwambije.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa mwenyekiti mteule Andrew Kuchonjoma ameahidi kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa wanachama na kuepusha migogoro ambayo imechangia kurudisha nyuma maendeleo ya klabu hiyo.
“Ndugu wanachama katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa kushirikiana na viongozi wenzangu naahidi kuleta mabadiliko makubwa ndani ya klabu yetu,ikiwemo kuanzisha mradi wa redio yetu ya klabu’’,alisisitiza.
Kwa upande wake makamu mwenyekiti Leticia Nyoni aliahidi kushirikiana na wanachama wote na hasa kusukuma maendeleo kwa waandishi wa habari wanawake waweze kujiunga kwenye klabu hiyo na kuleta maendeleo kwa kuwa mwanamke ni nguzo ya familia.
Katibu mkuu wa klabu hiyo Andrew Chatwanga  aliyataja matarajio katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kuwa licha ya kuanzisha redio ,pia wanatarajia kuanzisha kitega uchumi cha kudumu vikiwemo nyumba ya kulala wageni na mashamba.
Matarajio mengine aliyataja kuwa ni kutafuta wafadhili watakaosaidia wanachama wa klabu hiyo kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu yatakayofanyika ndani na nje ya mkoa kwa lengo la kuwajengea uwezo waandishi ili waweze kukabiliana na mabadiliko yanayotokea katika nyanja mbalimbali.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:

Post a Comment