Na Albano Midelo
Hakuna
ubishi kuwa Tanzania
ni nchi inayojihusisha zaidi katika
kilimo kwa kuzingatia mchango mkubwa unaotolewa kupitia sekta hiyo katika
uchumi wa taifa hali ambayo imefanya kilimo kuitwa uti wa mgongo na hivi sasa kuna kauli ambayo inasema
kilimo kwanza.
Takwimu
za kitaifa zinaonesha kilimo kinachangia asilimia 26.7 ya pato la taifa ,asilimia 95 ya pato la
chakula kinachotumika nchini ,asilimia 30 ya mauzo ya nje na kilimo kinachangia
asilimia 65 ya malighafi zinazotumika katika viwanda vya ndani.
Kilimo
ni mwajiri mkuu wa watanzania kutokana na takwimu kuonesha kuwa asilimia 80 ya
watanzania wote wamejiajiri katika sekta ya kilimo.Kwa ujumla ili Tanzania
uweze kufikia malengo yake ya maendeleo sekta ya kilimo inatakiwa ikue kutoka
asilimia nne hivi sasa angalau ifikie asilimia 10 ndiyo maana serikali iliamua
kuanzisha dhana ya kilimo kwanza.
Serikali
ya awamu ya nne ambayo inaongozwa na
Rais Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na waziri mkuu Mizengo Pinda mtoto wa mkulima inafanya juhudi za
makusudi kuhakikisha kuwa yanafanyika mapinduzi ya kilimo kwa kutoa ruzuku
katika pembejeo na kuhakikisha wakulima wanaondokana na jembe la mkono na sasa
wanaingia katika kilimo cha wanyamakazi pamoja na matumizi ya trekta dogo yaani
powertiller.
Pamoja na juhudi hizo kuchukuliwa bado sekta
ya kilimo inaonekana inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo idadi kubwa ya
wakulima kuendelea kutumia jembe la mkono,bei ya mbolea bado ipo juu licha ya
serikali kutoa ruzuku ya pembejeo pamoja na ukosefu wa soko la uhakika kwa
wakulima wanapovuna mazao yao.
Serikali kila mwaka imekuwa ikijitahidi kutoa
mbolea ya ruzuku kwa wakulima ili kupunguza makali ya bei ya mbolea ambapo utafiti
unaonesha kuwa mbolea ya ruzuku bado sio
msaada kwa wakulima wadogo wadogo kwa kuwa bei ya ruzuku bado ipo juu
ukilinganisha na uwezo wa wananchi walio wengi wenye kipato chini ,ni idadi
ndogo sana ya wakulima ambao wanapata fursa ya kupata mbolea ya ruzuku hivyo
wengi wanashindwa kumudu kununua.
Mbolea
ya ruzuku pia inakabiliwa na tatizo sugu la mawakala wasiokuwa waaminifu kwa kushirikiana na baadhi
ya viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali wanasababisha idadi kubwa ya
wakulima kushindwa kupata mbolea hiyo kutokana na kufanya ufisadi wa waziwazi
hali ambayo inasababisha wakulima wengi vijijini kushindwa kupata mbolea ya
ruzuku.
Mkoa
wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula
mikoa mingine ni Rukwa,Mbeya,Iringa pia serikali imeingiza
mikoa ya Morogoro na Kigoma hivyo kufanya ni mikoa sita itakayopewa kipaumbele katika uzalishaji wa
mazao ya chakula nchini .
Hata
hivyo uchunguzi umebaini kuwa tatizo la kutegemea mbolea za chumvi chumvi
ambazo licha ya kuuzwa kwa bei ya juu pia zinaleta madhara makubwa katika
udongo linaweza kumalizika kabisa kwa kufufua mradi wa mbolea wa kilimo mseto
Peramiho wilayani Songea mkoani Ruvuma.
Historia
inaonesha kuwa kilimo mseto kwa kutumia mradi wa kurutubisha ardhi kwa kutumia
mbolea ya marejea yaliyoletwa kutoka
porini mwaka 1942 na kutambuliwa Peramiho na padre Otmar na Bruda Krisp OSB
ambapo mwaka 1963 bruda Herman alianza
kutumia mbolea ya marejea kuzuia magugu na kulishia mifugo ambapo mwaka 1983
ilianzishwa benki ya mbegu za marejea Peramiho (sunnhemp seed bank).
Mwaka
1987 baada ya kuona umuhimu wa marejea
katika kurutubisha ardhi kilianzishwa kituo cha mradi wa kurutubisha udongo kwa kutumia marejea Peramiho(MRUMA) kituo ambacho hadi sasa kipo
kinaendelea kutoa elimu ya kutumia mbolea ya marejea kwa wakulima katika nchi
nzima.
Gabriel
Mhagama ni mkuu wa kituo cha MRUMA anasema kuna mimea mingi ambayo ina uwezo wa
kuongeza rutuba katika udongo
ikiwemo mimea jamii ya kunde
ambayo imegawanyika katika makundi matatu mimea ya porini,mimea ya mazao na
mimea ya miti.
Mhagama
anasema alikabidhiwa kuwa mkuu wa kituo hicho tangu mwaka 1991 kutoka kwa
muasisi wa kituo hicho hayati padre Gerald ambaye alifariki dunia mwaka 2000
ambapo hivi sasa wataalamu wengi wa masomo ya kilimo kutoka ndani na nje ya nchi
wamekuwa wakifika katika kituo hicho kufanya utafiti na kutunukiwa shahada za
kwanza,shahada ya pili na wengine wametunukiwa PHD.
Hata
Mhagama anasema utafiti uliofanywa katika kituo cha MRUMA tangu mwaka 1942
umebaini kuwa mimea ya porini aina marejea inachukua nafasi ya kwanza kwa
kurutubisha ardhi na mkulima akitumia mbolea hiyo ana uwezo wa kuzalisha mazao
mara dufu zaidi ya kutumia mbolea za viwandani.
Utafiti
uliofanywa na kituo cha kilimo Uyole kuhusu mbolea ya marejea umebaini kuwa
shamba la hekta moja lililolimwa marejea
mwaka uliotangulia linaweza kutoa magunia 68 ya mahindi yenye uzito wa kilo 100
badala ya magunia 14 tu iwapo haujatumia marejea.
“Iwapo
unataka shamba lililopandwa marejea kulima mwaka unaofuata unayaacha marejea
yakue hadi yatoe mbegu ambapo utavuna mbegu
na yale majani ya marejea
unayachanganya na udongo ili kurutubisha ardhi tayari kupanda mazao marejea ni bora kwa kutoa mboleavunde,rahisi
kufyeka na uoza haraka’’,anasisitiza.
Utafiti
umebaini kuwa mbolea ya marejea ndiyo majibu ya mkulima ambaye hawezi kumudu
kununua mbolea ya viwandani kwa kuwa mbolea hiyo hurutubisha na kudumisha rutuba
ardhini,vijidudu viitavyo bacteria hutoboa mzizi wa marejea na kusababisha
vijinundu ambavyo ni nyumba yao na bacteria hao hutangua hewa aina ya naitrojen
kama mbolea kwa kulishia mimea.
“Siku
zote tunawambia watu kwanini wanang’ang’ania kulima mazao ya haraka haraka kwa
kutumia mbolea za chumvi chumvi wakati zinawaumiza,badala ya kuchukua mbolea ya
marejea ambayo hayana gharama yametolewa porini,watu wamekusanya na kuyaleta
katika kituo chetu padre Gerod aliyapanda na kuyazalisha kwa wingi ambapo mwaka
1960 alipata kilo sita na kuanza kueneza mbegu za marejea nchini kote”,anasema
Mhagama.
Mbinu
aliyoitumia padre Gerod kupata marejea kutoka kwa wakulima ni kuwahamasisha
wakulima kulima marejea na kumletea ambapo yeye aliwapatia mbolea ya chumvi
chumvi na baada ya miaka mitatu padre huyo alipata maelfu ya tani za mbolea ya
marejea ndipo aliwaambia sasa wananchi waache kutumia mbolea ya viwandani na
kuanza kutumia marejea lakini padre huyo
aliendelea kununua marejea kutoka kwa wakulima.
Kulingana
na mtaalamu huyo mbolea ya marejea
husaidia wiki mbili hadi mwezi mmoja baada ya kufyeka shamba ambapo mkulima anatakiwa kupanda marejea kilo
20 kwa ekari na kutumia mfumo wa kubadilisha mazao yaani crop rotation ili
kupata mafanikio wakati wa kutumia mbolea ya marejea.
“Wakulima
ili wafanikiwe katika mbolea ya marejea wanatakiwa kubadili mazao kwa mfano
mwaka wa kwanza katika ekari moja anapanda marejea,mwaka wa pili anapanda
mahindi mwaka wa tatu anapanda mtama mwaka wa nne anapanda marejea pia anaweza
kuchanganya mazao mwaka wa kwanza anapanda marejea na kahawa,mwaka wa pili
marejea na jamii ya kunde,mwaka wa tatu marejea na mihogo na mwaka wa nne
marejea ,migomba na miti”,anasema.
Utafiti
zaidi umebaini kuwa mbolea ya marejea
hupunguza na kuzuia magugu shambani,marejea ni malisho kwa wanyama pia
majani yake ni mboga na mabua hutumika kwa ajili ya matandiko ya
wanyama,marejea pia huzuia wadudu waharibifu.
Mapato yatokanayo na matumizi ya mbolea ya
marejea ni ya kuridhisha na ya kudumu
hata katika maisha ya vizazi vijavyo kwa kuwa udongo na mazingira vinabakia na
asili ya kutotawanyika (soil structure stability).
Uchunguzi
umebaini kuwa miaka ya 1983 mbolea ya marejea ilianza kutumiwa na wakulima
wengi katika sehemu mbalimbali nchini ambapo wakulima na vikundi vya wakulima
walifika katika kituo cha MRUMA Peramiho kujifunza kuhusu uzalishaji wa mbolea
hiyo hali ambayo ilisababisha maelfu ya
tani za mbegu za marejea kununuliwa na kwenda kuzalishwa.
Mkuu
wa kituo cha MRUMA Gabriel Mhagama anasema Baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere
alitembelea kituo hicho na kufurahishwa na uzalishaji wa mbolea hiyo hali
iliyosbabisha baba wa Taifa kununua tani za mbegu za marejea pamoja na kununua
vitabu mbalimbali vinavyotoa elimu ya mbolea ya marejea.
Mhagama
anasema padre Gerodi na hayati Baba wa Taifa walikuwa ni wafuasi wakubwa wa
mbolea ya marejea ambapo mama Maria Nyerere bado anaendelea kutumia mbolea ya
marejea na mara kwa mara anaagiza vitabu vingi vinavyozungumzia mbolea ya marejea pamoja na
kilimo mseto hivi karibuni amenunua tani mbili za marejea ambazo tumempelekea nyumbani kwake Butihama”,anasisitiza Mhagama.
Mhagama
anaongeza kuwa mbegu za marejea pamoja na
vitabu vinavyoelekeza matumizi ya mbolea hiyo na kilimo hai vinaagizwa
na wakulima wengi toka nje ya nchi kila mwaka ingawa idadi ya watanzania wanaotumia marejea ni
wachache kutokana na serikali kutoa uhamasishaji zaidi katika matumizi ya
mbolea za viwandani ambazo zinauzwa kwa
bei ya juu pia sio endelevu kwa kuwa zina madhara kwenye udongo.
“Katika
kituo chetu tunatoa elimu kwa wakulima kuhusu mbolea ya marejea lakini jambo la
kusikitisha ukiachia aliyekuwa mkuu wa mkoa mstaafu wa Ruvuma hayati
Dk.Lawrence Gama, baba wa Taifa na mke wake mama Maria Nyerere ambao wametembelea
kituo chetu na walihamasisha matumizi ya mbolea ya marejea,hadi sasa hakuna
kiongozi mwingine yeyote ambaye amewahi kufika hapa hakuna watalaamu wa ugani
wa serikali mbunge,mkuu wa mkoa,mkuu wa wilaya,waziri wala Rais “,anasema.
Mhagama
anasema hayati Dk.Gama akiwa mbunge wa Songea mjini alipeleka teknolojia ya
mbolea ya marejea bungeni ili waziri wa kilimo aweze kufuatilia zaidi kuhusu
matumizi ya mbolea hiyo na kwamba jambo la kusikitisha tangu wakati huo hadi
sasa hakuna ufuatiliaji wowote wala hatua za kuhakikisha wakulima nchini
wanahamasishwa kutumia mbolea ya marejea.
“Vikundi
mbalimbali vya wakulima ambavyo vimetambua siri ya mbolea ya marejea vimekuwa
vinaniita kutoa elimu ya uzalishaji pamoja na kilimo hai kwa mfano juzi
nilikuwa mkoani Morogoro kwa siku tisa,mwezi uliopita nilikuwa mkoani Mbeya
wilayani Mbozi nikitoa elimu ya marejea kwa wakulima raia wa Uswis waliniita
kwa gharama zao, kila mwaka nakwenda katika mikoa mbalimbali nchini kutoa elimu
hii”,anasema Mhagama.
Mtaalamu
huyo wa marejea anasema dhana ya kilimo kwanza ambayo inapigiwa chapuo kwa
ushirikiano wa Rais Jakaya Kikwete pamoja na waziri mkuu Mizengo Pinda inaweza
kuwa endelevu na kupata mafanikio makubwa endapo watanzania wote watatumia
mbolea ya marejea ambayo inapatikana bure na ni endelevu kwa udongo kwa kizazi
cha sasa na kijacho.
“Nakuomba
waziri mkuu Pinda utembelee katika kituo chetu za kuzalishia mbolea ya
marejea Peramiho ikiwezekana nipeni
nafasi hata ya saa moja katika Bunge la Muungano ili niweze kutoa elimu hii kwa
wabunge wote naamini wabunge watahamasisha wapiga kura wao kuachana na mbolea za
viwandani na kuanza kutumia mbolea ya marejea ambayo ndiyo mkombozi wa wakulima
na dhana nzima ya kilimo kwanza”,anasisitiza.
Thomas
Lipuka mdau wa kilimo anasema kuwa sekta ya kilimo nchini kwa miaka mingi haijawanufaisha
wakulima wadogo na kwamba cha kusikitisha zaidi wakulima wengi wameonekana ni
kama ngazi ya kupandia wafanyabiashara wa kati na wakubwa, mashirika na makampuni makubwa kwa
kujinufaisha kupitia wakulima pamoja na mbolea ya ruzuku ambayo wanajinufaisha
mawakala na viongozi wa serikali wasiokuwa waaminifu.
Mshauri
wa kilimo katika mkoa wa Ruvuma Sixtus Msanga anasema wakulima nchini
wanajitahidi kulima lakini kilimo kinazidi kukatisha tamaa kutokana na
changamoto mbalimbali hasa bei kubwa ya pembejeo na ukosefu wa soko la uhakika kwa ajili ya mazao yao
.Naye
mwakilishi kutoka shirika la Tanzania Organic Agriculture Movement(TOAM) Noel
Kwai anasema kilimo hai sio kitu kigumu
bali mkulima wa kawaida anaweza kufanya kwa kutumia mbolea za asili ambazo ni
endelevu na hazina madhara kwenye udongo.
“Sisi
kilimo hai tunaangalia mbele zaidi kwanini utumie mbolea za viwandani zenye bei
kubwa badala ya kutumia samadi na mbolea nyingine za organic ukichukulia kuwa
mbolea ya viwandani ni bei juu na haitoshi, kilimo hai hapa nchini
historia yake imetokea Peramiho ni makosa makubwa kulima bila kutumia mbolea kwa kuwa marejea yapo tuache uvivu”,anasema.
Baruapepe amidelo@yahoo.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment