Na Albano Midelo
TAKRIBAN watu 14 hadi sasa wamekufa na 48 kujeruhiwa kutokana
na maandamano na vitendo vya mauaji vinavyoendelea
kwenye viunga vya mji wa Songea ambao ndiyo makao makuu ya mkoa wa Ruvuma.
Mauaji hayo yakinyama yalianza tangu mwezi Novemba mwaka jana
ambapo awali mauaji yalikwenda sanjari na vitendo vya unyang’anyi wa pikipiki
kisha madereva wa pikipiki hizo kuuwawa kikatili na miili yao kutupwa katika
misitu iliyopo nje kidogo ya mji wa Songea.
Mwanzoni mwa mwaka huu vitendo vya mauaji viliendelea na
kusababisha hofu kubwa kwa wakazi wa mji wa Songea ambao walitarajia mauaji
hayo yangekomeshwa na jeshi la polisi lenye dhamana ya kulinda uhai wa raia
pamoja na mali zake.
Katika hali isiyotarajiwa kasi ya mauaji iliendelea ambapo
sasa ilidaiwa wauaji walianza kuuwa wasichana na wanawake kisha kuondoa baadhi
ya viungo vya mwili zikiwemo sehemu za siri
kwa madai viungo hivyo vilitumika kwa ajili ya vitendo vya kishirikina.
Mwezi Februari mwaka huu hali ya mauaji iliendelea kwa kasi
ambapo matukio ya mauaji yaliendelea kuripotiwa mara kwa mara.Hali hiyo
iliwafanya wakazi wa mji wa Songea kuamua kuingia vitani ili kupambana na janga
hilo ambalo linatishia usalama na amani ya wakazi wa mkoa wa Ruvuma ambayo
walikuwa wameizoea kuiona tangu kuzaliwa kwa mkoa wa Ruvuma.
Wananchi baada ya kuona ndugu zao wanaendelea kuteketea
waliamua sasa kujilinda wao wenyewe ikiwemo kuchukua sheria mkononi bila
kutambua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Kwa mfano wakazi wa eneo la Ruhuwiko ambao ndugu zao kadhaa
wameteketea kwa kuuwawa na watu wasiojulikana,mwezi Februari mwaka huu waliamua
kuwachoma kwa moto watu wawili ambao walidaiwa kuwa ni majambazi.
“Tuliwakamata watu hawa wawili wakijaribu kufanya mauaji
katika eneo letu ambapo walidai walitumwa kumuua mama mmoja,baada ya kuwakamata
tuliwahoji na kuanza kuwapa kipigo ili watueleze ukweli ndipo walidai kuwa wao
ni wauaji tayari wameua watu 10 hadi
wanakamatwa’’,alidai mwananchi mmoja ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Mwananchi huyo alidai kuwa watu hao baada ya kukiri wao
wenyewe kuwa ni wauaji ndipo wananchi
wanawake kwa wanaume walichachamaa na kuanzia kuwapiga ,kuwafunga kamba
miguu na mikono kisha kuanza kuwachoma moto wakiwa hao.Tukio la wananchi
kuchukulia sheria mkononi pia limefanywa na wakazi wa Mkuzo ambao waliwauwa
watu wawili wakidai kuwa ni wauaji.
Baada ya matukio hayo jeshi la polisi liliamua kufanya
mkutano wa pamoja na wakazi wa maeneo hayo na kuwataka wanapowakamata watuhumiwa
wasichukue sheria mkononi badala yake wawafikishe kwenye vyombo vya dola ili
haki itendeke.
Hata hivyo kasi ya mauaji ya wananchi iliendelea katika
viungo mbalimbali vya mji wa Songea hali ambayo
iliongeza hasira kwa wananchi ambao walidai kuwa jeshi la polisi limeshindwa
kukomesha mauaji.
Kamanda wa polisi wa
mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhada mara kadhaa alikaririwa katika vyombo vya
habari akitoa rai kwa wakazi wa mji wa Songea kutulia kwa kuwa jeshi hilo
linajipanga ili kuhakikisha kuwa mauaji hayo yanakwisha na hali ya usalama na
utulivu inarudi kama kawaida.
Kitendo cha kuchelewa kuchukua hatua za kumaliza tatizo la
mauaji ndicho ambacho kilisababisha wananchi kuamua kufanya maandamano bila
kibali kwa kuwa mauaji yaliendelea kutokea mfululizo na jeshi la polisi pamoja
na serikali ya wilaya na mkoa ilidai kuwa inajipanga kukabiliana na wauaji bila
mafanikio.
Hatimaye wananchi waliandamana bila kibali na kuleta athari
zaidi katika mji wa Songea ikiwemo kusababisha vifo vya watu wanne ambao
waliuwawa na polisi katika harakati za kutuliza maandamano hayo kwa kutumia
mabomu na risasi za moto.
Wanaharakati wamelaani jeshi la polisi mjini Songea kutumia
risasi za moto kwa lengo la kusambaratisha maandamano hayo na kusisitiza kitendo cha kuuwa raia ni cha kinyume
na haki za binadamu .
“Tatizo la polisi ni kutumia nguvu ya ziada hata katika mambo
yatayotakiwa kucheza na saikolojia ya watu,mbinu ambayo naamini makamanda wa
polisi wanapaswa kuitumia ili kutuliza
hasira za wananchi wanaolalamika kutotendewa haki’’, anasema Daniel Mwaijega.
Anabainisha kuwa wananchi wa Songea waliandamana kwenda kwa
mkuu wa mkoa wa Ruvuma kutoa kilio chao kutokana na hofu na uchungu wa
kutosikilizwa ,nguvu kubwa ya polisi iliyotumika kuwapiga mabomu,risasi pamoja
na vitisho vingine.
Nguvu gani hiyo ya kuamua kutumia risasi za moto ghafla,mbona
kule Mbeya ambako hali ilikuwa mbaya polisi waliishia kutumia mabomu ya machozi
na maji ya kuwasha kwa siku tatu mfululizo?anahoji Mwaijage na kutokubaliana na
maelezo ya kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamunda kwamba walilazimika
kutumia risasi za moto ili kujihami na umati wa watu uliokuwa unawazidi nguvu.
Naye Neville Meena mhariri wa Mwananchi Jumapili anadai polisi wanachotakiwa ni kueleza ukweli
wa wao kuuwa raia wasikuwa na hatia na
kwamba wananchi hao walichokuwa wanahitaji ni neno la faraja kutoka kwa polisi
ambao ni walinzi wa amani ili wajue
usalama wao dhidi ya mauaji.
“Jambo hili tuwe wakweli kama wananchi waliwazidi nguvu
polisi,je polisi wangapi waliojeruhiwa,haiingii akilini katika ukubwa wa vurugu
kama zilivyoelezwa na jinsi waandamanaji wanavyotajwa kwamba walikuwa
wanapambana na polisi halafu asiwepo hata askari mmoja aliyejeruhiwa’’,anahoji
Meena.
Meena anasisitiza kuwa nguvu iliyotumika kuwadhibiti
waandamanaji zikiwemo risasi za moto,mabomu,fedha na gharama nyingine
zingetumika kuwadhibiti wauaji wa raia kitu ambacho ndiyo kiini cha wakazi wa
Songea kuandamana.
Kwa upande wake Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea
mhashamu Norbert Mtega akizungumzia maandamano na mauaji yanayofanywa na
polisi anasema yanatokana na
serikali kuchelewa kutoa ufumbuzi wa
matatizo yanayowakabili wananchi pamoja na serikali kutoa majibu ya juu juu
hivyo kuchochea chuki na kuleta vurugu.
Kamishina wa operesheni maalum Paul Chagonja akizungumzia
maandamano yaliosababisha vifo vya raia alidai kuwa askari watatu walijeruhiwa baada ya
kushambuliwa na wananchi kwa mawe,fimbo,nondo,kuchoma matairi na zana nyingine
za jadi huku wakipaza sauti kwamba askari polisi hao lazima wauawe.
Hata hivyo kamishina huyo wa operesheni maalum
anatahadharisha kuwa polisi wanaruhusiwa kuuwa chini ya kifungu cha sheria
namba 18(c)cha sheria za kanuni za adhabu .
“Iwapo polisi watashindwa kuzima vurugu kwa kutumia
maneno,virungu,mabomu ya machozi na maji ya kuwasha,njia pekee inayobakia ni ya
kutumia risasi za moto ili kuepusha maafa makubwa,ni vema hilo likaeleweka ili
kuondoa dhana potofu kwamba polisi hawaruhusiwa kuuwa’’,anasisitiza.
Chagonja ameitaja
mikakati na jitihada ambazo zimechukuliwa na polisi kuwa ni kuundwa kwa kamati
ya kuchunguza kiini cha maandamano na
fujo zilizojitokeza katika mji wa Songea.
Mikakati mingine ameitaja kuwa ni kukutana na
madiwani,maafisa tarafa,watendaji kata,mitaa na wenyeviti wa mitaa ili kupata
suluhisho la kuondoa uharifu,kuimarisha ulinzi na usalama kupitia polisi jamii
na kuendelea kutoa mafunzo kwa askari juu ya matumizi sahihi ya silaha katika
udhibiti wa vurugu,fujo na maandamano kwa kuzingatia sheria na kanuni.
Athari nyingi zimejitokeza hadi sasa kutokana na mauaji hayo
zikiwemo vifo vya watu,majeruhi na vilema na kwamba mauaji hayo yanaleta hofu
kubwa kwa wananchi wa rika zote wakulima,wafanyakazi ,wafanyabiashara na
wanafunzi.
Uchunguzi umebaini kuwa wakulima wa mji wa Songea ambao
wanalima pembeni mwa mji huo huenda mwaka huu wakapata njaa kwa kuwa
wanashindwa kwenda shambani kutia mbolea na kupalilia mashamba yao kwa hofu ya
kuuwawa na wauaji .
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi katika manispaa ya
Songea wanaogopa kwenda shuleni kuhofia kutekwa na wauaji ambao hivi sasa
wanadaiwa kutumia magari yenye vioo vyeusi na pikipiki kuwateka wanafunzi na
hata watu wazima.
Mji wa Songea ambao unakadiriwa kuwa na pikipiki zaidi ya
6000 hivi sasa biashara ya kubeba abiria
kwa pikipiki imepata dosari kutokana na abiria wengi kuogopa kupanda pikipiki
hizo kwa madai kuwa baadhi ya madereva wanatumiwa na wauaji kuwapeleka abiria
baada ya kulipwa fedha nyingi na wauaji hao.
“Sisi madereva wa pikipiki tunauwawa ovyo siku hizi kisha
kunyang’anywa pikipiki,biashara hii hivi sasa haifai kwa kuwa ni sawa na
kujitafutia kifo wewe mwenyewe,madereva wengi wameacha biashara hii na kufanya
kazi nyingine za kujipatia kipato wengine wamerudi kwenye uhalifu’’,alidai Abdalah
Ally dereva wa pikipiki mjini Songea.
Ally alidai kuwa wanaoendelea kufanya biashara ya kuendesha
pikipiki ni wale tu ambao wana roho ngumu na kwamba wanachukua tahadhari kubwa
ikiwemo kuhakikisha kuwa abiria wanaembeba wanamfahamu.
Mauaji ya Songea sio tu yanaleta athari kwa madereva wa
pikipiki,bali pia hata kwa wafanyabiashara kwa mfano wanaoendesha biashara ya
vinywaji kama vile bia hivi sasa wanakwama kwenye mauzo kwa kuwa wananchi wengi
jua linapozama wanarudi majumbani kwao kuhofia kuuwawa.
Kwa ujumla maendeleo ya mji wa Songea yanarudi nyuma kutokana
na mauaji yaliyotokea na kwamba kazi hazifanyiki ipasavyo,wakazi wa mji
wa Songea wana hofu kubwa ,licha ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu kutoa
rai kwamba wananchi warudi kazini wasiwe na hofu.
Wakazi wa mji wa Songea bado wana hofu kubwa .Hofu ya wakazi
wa Songea itamalizika pale ambapo jeshi la polisi litakomesha kabisa mauaji
haya ambayo hadi sasa bado uchunguzi na utafiti unaendelea kufanyika ili kujua
nini hasa sababu ya vifo hivyo vya kinyama.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129


No comments:
Post a Comment