Na Albano Midelo
ASKOFU mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert
Mtega amewafunda mapadre nchini kutambua kuwa upadre sio kazi ya ajira bali ni
kazi ya utume na majitoleo.
Mhashamu Mtega alitoa somo hilo wakati anahubiri kabla ya kuwapatia
daraja takatifu la upadre mashemasi wawili
katika adhimisho la misa takatifu iliyofanyika katika kanisa la parokia
ya Mjimwema jimbo kuu la Songea.
Mashemasi waliopatiwa daraja takatifu la upadre na Askofu mkuu Mtega ni shemasi David Mhagama
kutoka kigango cha Lizaboni parokia ya Songea na shemasi Markus Komba kutoka
Kigango cha Mwengemshindo parokia ya Mjimwema.
“Upadre sio kazi bali
ni utume,leo mnapokea utume hapa siwapatii kazi,wala mimi sio mwajiri
wenu,anayefikiri askofu ni mwajiri wake amekosa imani ,nenda kwa Rais Jakaya
Kikwete utaajiri,nenda kwa waziri wa TAMISEMI utaajiriwa,unapojiweka hapa mbele
ya Taifa la Mungu wewe ni sadaka ’’,alisisitiza.
Askofu mkuu Mtega pia
amewakumbusha waumini kuwa na moyo wa kujitolea katika shughuli mbalimbali za
kanisa na kuacha kuona kichefuchefu
kutoa sadaka na huduma za kanisa la Mungu kwa kuwa kufanya hivyo ni kumtumikia mwenyezi Mungu.
Alisisitiza kuwa bila kufikia kilele cha kutoa sadaka na
kujitoa sadaka ni kazi bure na kwamba anayesali,anayepokea ekaristi takatifu na
anayepata daraja takatifu kama upadre ajue siri yake yote ni majitoleo kama Yesu Kristo alivyojitolea mwili wake kwa
wanadamu.
Mhashamu Mtega amewatahadharisha mapadre kuwa upadre unaweza
kuonekana mgumu iwapo tu watashindwa kuwa na moyo wa kujitolea sadaka katika mwili,muda,roho na uzima na kuacha kuona kichefuchefu kwenda
kufanyakazi kwa waumini katika maeneo mbalimbali mijini na vijijini.
Amewaasa mapdre hao wapya kuwa wameitwa na Mungu hivyo
wanatakiwa kuifanya ipasavyo kazi ya Mungu ambayo wametumwa kwenda
kuifanya kwa unyenyekevu mkubwa kwa
kumtukuza Mungu kwa kuhubiri, kufungisha ndoa, kubatiza, kutoa kitubio na misa
takatifu.
Kwa upande wake paroko wa parokia ya Mjimwema padre Nowe Duwe
amemshukuru askofu mkuu Mtega kukubali kutoa daraja takatifu kwa mashemasi
mawili katika kanisa la parokia hiyo licha ya kwamba ujenzi wake bado haujakamilika hali ambayo
inasababisha waumini kupigwa na jua,upepo na vumbi.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment