Na
Albano Midelo
WATU 13,706 katika
Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma hawajui kusoma,kuandika na
kuhesabu.
Afisa elimu watu wazima katika Halmashauri hiyo
Christopher Mwamalili alibainisha kuwa idadi hiyo imetokana na sense
iliyofanyika mwezi Februari mwaka huu
idadi ambayo ni sawa na asilimia 14 ya watu wote wazima.
Kulingana na sensa hiyo kati ya watu hao
wanaume ni 6069 na wanawake ni 7637 ambapo takwimu za mwezi Februari mwaka huu
zinaonesha kuwa Halmashauri ya wilaya ya Songea ina watu wazima wanaojua kusoma,kuandika na kuhesabu 94,800
kati yao wanaume ni 45,900 na wanawake 48,981.
Kata ambazo
zinaongoza kwa idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu katika
Halmashauri hiyo ni Ndongosi watu 585,Muhukuru watu 882,Matimira watu 664 na
Mpitimbi watu 832.
Afisa elimu watu
wazima huyo alikitaja chanzo cha Halmashauri hiyo kuwa na idadi kubwa ya watu
wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu kuwa ni
kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto ambao hawakuandikishwa darasa la kwanza
kabla ya kuanza kwa Mpango wa uboreshaji
wa Elimu ya Msingi (MMEM).
Kwa mujibu wa
Mwamalili sababu nyingine zilizochangia kuongezeka kwa idadi kubwa ya wajinga
katika Halmashauri hiyo ni michango mingi waliokuwa wanatozwa wazazi na
walezi,upungufu wa vyumba vya madarasa,utoro na mimba.
Hata hivyo amezitaja
hatua ambazo idara yake imeanza kuzichukua ili kukabiliana na tatizo hilo
ikiwemo ya kuanzisha madarasa 92 ya
Mpango wa uwiano kati ya elimu ya watu
wazima na jamii yaani MKEJA na kwamba walimu wa kujitolea waliohitimu kidato
cha nne watatumika kufundisha madarasa hayo.
“Lengo ni kuhakikisha
kuwa hadi kufikia mwaka 2013 idadi ya watu wazima wasiojua kusoma,kuandika na
kuhesabu inapungua kutoka asilimia 14 hivi sasa hadi asilimia kati ya sita na
saba na kufuta madarasa ya Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Walioikosa yaani
MEMKWA kwa kuwa sio mpango endelevu kama ilivyo kwa mfumo rasmi wa utoaji
elimu’’,alisisitiza Mwamalili.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment