Na Albano Midelo
WANAFUNZI zaidi ya 2000 wa shule nne za msingi mjini Namtumbo
mkoani Ruvuma wapo katika hatari ya
kupata magonjwa ya milipuko kutokana na shule hizo kukatiwa maji ya bomba.
Shule hizo ni Namtumbo yenye wanafunzi 669,Rwinga yenye
wanafunzi 592,Selous yenye wanafunzi 477
na shule ya msingi Kidugalo yenye wanafunzi 453.
Mamlaka ya maji katika Halmashauri ya Namtumbo imeamua
kuzikatia shule hizo maji kutokana na kile ambacho kinaelezwa kuwa shule hizo
ni wadai sugu wa bili za maji hali ambayo inasababisha wanafunzi kutumia maji ya mto na visima ambayo sio salama na yanapatikana mbali .
Akizungumza kwa niaba ya mwalimu mkuu,mwalimu wa taaluma
katika shule ya msingi Namtumbo Habibu Omary alisema tangu wamekatiwa huduma ya
maji imekuwa ni kero kubwa kwa walimu na wanafunzi ambao walikuwa wanagemea maji
hayo kwa matumizi mbalimbali yakiwemo kunywa,kufanyia usafi ,chooni pamoja na
matumizi mengine.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kidugalo Owini Mpangala
anasema shule hiyo haina maji ya bomba ,hivi sasa wanatumia wanatumia maji ya mto na visima vya jadi
ambavyo vipo mbali na maji yake sio salama hivyo ametoa wito kwa mamlaka ya
maji kupeleka huduma ya maji kwenye shule hiyo .
Naye mwalimu anayeshughulikia kitengo maalumu cha wanafunzi
wenye ulemavu wa akiri katika shule ya msingi Namtumbo Lanziry Kampango anasema
hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wake wenye ulemavu wapatao 26 kwa kuwa
mahitaji ya maji kulingana na mahitaji yao ni muhimu.
“Wanafunzi wenye ulemavu ni lazima wapate chai,sasa chai
inatengenezwa vipi kama hakuna maji,wanafunzi hawa wana masomo mengi yanayotakiwa kufundishwa kwa vitendo mfano
usafi chooni ,wakitoka kujisaidia maji hakuna tunaomba serikali ilipe bili na
kurejesha maji shuleni’’,alisisitiza.
Mwalimu Onesmo Mbawala wa shule ya msingi Rwinga anasema
tangu wamekatiwa huduma ya maji hali ni mbaya na kwamba huduma hiyo
isiporejeshwa haraka kuna hatari wanafunzi na walimu wakapata magonjwa ya
milipuko kama vile kuhara kwa kuwa
wanafunzi wanakwenda kujisaidia chooni bila kunawa jambo ambalo ni hatari
kiafya.
“Hatua ambazo tunazichukua ili kukabiliana na hali hiyo ni
kuwaagiza wanafunzi wanapofika asubuhi waje na maji,wengine wanasaidiwa na
walimu kuwapatia maji ya kunywa pale wanapohitaji lakini maji katika shule yetu
ni tatizo kubwa’’,alisisitiza mwalimu Mbawala wa shule ya Rwinga.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo
Kassimu Ntara amesema hakuwa na taarifa kuwa baadhi ya shule katika zimekatiwa
huduma ya maji hivyo ameahidi kufuatilia na kuhakikisha kuwa maji yanarudi
katika hali ya kawaida.
“Tatizo la wanafunzi kukatiwa maji ndiyo kwanza nakusikia
wewe nitafuatilia na kukaa na wataalamu wangu wa maji kwenye Halmashauri
kuhakikisha kuwa maji yanarejeshwa haraka ingawa mamlaka ya maji ni mamlaka
inayojitegemea nitafuatilia ili taasisi hizo ziweze kupata huduma ya
maji’’,alisisitiza.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment