“MAISHA yetu ni kama kifaranga aliyekosa mama kwani hali zetu za
kiuchumi kila kukicha zinazidi kudhoofika kama mgonjwa wa kwashiakoo’’,anasema
Julius Machia ambaye ni kiongozi wa
kikundi cha umoja wa wafugaji wahamiaji bonde la Songwe lililopo wilayani
Chunya mkoani Mbeya.
Anabainisha kuwa endapo kiwango cha kupigwa faini ambazo sio
halali kitaendelea ,mifugo yao
itamalizika na watakuwa masikini na
mzigo kwa serikali kwa
kuwa wanaishi kwa kutegemea mifugo walionayo.
Machia anasema tangu zoezi la kukamata mifugo inayozidi 70 na kutozwa
kwa kila mfugo unaozidi shilingi 20,000,kumesababisha matatizo mengi kwa
wafugaji yakiwemo baadhi yao kuuwawa na askari kwa kupigwa risasi katika
operesheni ya kamata mifugo na wafugaji kudhulumiwa kwa kupigwa faini kubwa
hali ambayo inamlazimu mfugaji kuuza mifugo kwa bei ya hasara.
Deus Mashalla mfugaji katika kijiji cha Galula anasema kitendo cha
kukamata mifugo ya wafugaji wahamiaji kimekuwa kinafanyika sio kwa kuangalia
idadi ya mifugo inayozidi 70 badala
yake hata wakikuta mfugaji mhamiaji
katika eneo lake kuna ng’ombe mmoja hukamatwa na kupelekwa katika kituo cha
polisi na kumtoza mfugaji huyo kiasi cha
shilingi 20,000.
Hata hivyo Mashalla anabainisha
kuwa wanaoendesha operesheni ya kukamata mifugo wamekuwa wanavamia hata
katika nyumba za wafugaji wahamiaji na kuwanyang’anya mifugo na kuwatendea vitendo
vinavyokwenda kinyume na haki za binadamu.
Anavitaja vitendo hivyo kuwa ni kutishiwa risasi hewani ili wenye
mifugo wajifiche na kuogopa kuuwawa,kupiga nyumba risasi hadi kubomoa ambapo
wametolewa mfano nyumba ya mfugaji Jikolela Mihambo wa kijiji cha Swela nyumba
yake iliteketea kwa moto baada ya kupigwa kwa risasi.
Vitendo vingine ambavyo vinakiuka haki za binadamu ni kuporwa kwa
fedha za wafugaji,mgambo na askari kuwakimbiza wafugaji kwa magari na
kuwasababishia majeraha wakati wakijitahidi kukimbia ili kujiokoa.
Wafugaji wahamiaji hao wamebainisha zaidi kuwa wafugaji wa bonde la
Songwe ndiyo jamii inayooongoza kwa kilimo
kwa kuwa wanazalisha mazao mengi ya chakula kama vile
mahindi,mpunga,mtama na viazi vitamu na kwamba wafugaji hawapati tatizo la njaa
ukilinganisha na wakulima wenyeji ambao karibu kila mwaka wanapata tatizo la
njaa.
Gamaya Bunga mfugaji katika
kijiji cha Chang’ombe anasema utozwaji
wa faini unaonekana kufanyika kwa upendeleo kwa kuwa wakulima wanaovunja sheria
na kulima kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria kama vile kwenye vyanzo
vya maji vya mto Songwe na ziwa Rukwa
hawakamatwi.
Bonde la Songwe lenye kata za Galula, Mbuyuni, Totowe, Namkukwe na
Khanga lina utajiri mkubwa wa mifugo inayomilikiwa na wafugaji wahamiaji kutoka
wa mikoa ya Tabora ,Shinyanga, Mwanza, Singida na Kagera ambapo inakadiriwa kuna mifugo zaidi ya 727,230 hadi kufikia
mwaka jana.
Takwimu ambazo zimetolewa na afisa mifugo,kilimo na ushirika katika
Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale
zinaonesha kuwa kati ya mifugo
hiyo ng’ombe ni 286,800, mbuzi 46,501, kondoo 24,803, nguruwe 11,223 na kuku wa
kienyeji 357,903.
Mbale anabainisha kuwa Kutokana na uwepo wa mifugo mingi serikali
mwaka 2002 ilitoa sheria ya Halmashauri ya wilaya ya Chunya kuhakikisha kila mfugaji katika bonde hilo awe
na mifugo isiyozidi 70 na kwamba mfugaji atakayezidisha kiwango hicho cha
mifugo anapigwa faini ya shilingi 20,000
kwa kila mfugo unaozidi.
Julius Machia anasema faini wanayotozwa na serikali kwa kila mfugo
unaozidi imekuwa inafanyika katika
mazingira ya kifisadi kwa kuwa kiwango cha faini ni kikubwa na kwamba kinachoandikwa
kwenye risiti za malipo ya Halmashauri ya wilaya na hali halisi ni tofauti.
Baadhi ya risiti ambazo gazeti
hili imepata nakala zake zinaonesha kuwa
mfugaji Materemki Lugola wa kijiji cha Wanzani alilipa faini ya shilingi
milioni 4,740,000 mwaka 2001 kwa ajili ya mifugo 948 kula katika mashamba ya
wakulima.
Aliyetakiwa kupokea fedha hizo ni mkulima ambaye shamba lake limeliwa na
mifugo kupitia ofisi za vijiji badala yake mpokeaji wa fedha hizo ni Afisa
mifugo,kilimo na ushirika wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya ambaye amesaini
katika risiti kuwa amepokea kiasi hicho cha fedha.
Risiti nyingine ya mwezi Mei mwaka 2011 inaonesha kuwa mfugaji Julius
Machia wa kijiji cha Chang’ombe alilipa
faini ya shilingi milioni sita kwa ajili ya kuzidi mifugo 300 ambapo kila mfugo
uliozidi ulitozwa shilingi 20,000,hata hivyo risiti hiyo imeandikwa mfugaji
huyo amelipa shilingi laki sita badala ya milioni sita.
“Tumepumzika kwa miezi sita,tu Mei 16 na Juni mosi mwaka huu afisa
mifugo akiwa na viongozi wengine wamefika tena kwenye bonde letu safari hii
wametoza faini ya uharibifu wa mazingira ng’ombe na mbuzi zinazozidi kila mfugo
shilingi 20,000,wamekusanya mamilioni ya shilingi,tumewandikiwa risiti ambazo
sio halali tunaomba serikali isikilize kilio chetu, anasema mfugaji Machia.
Wafugaji wahamiaji wengine waliopigwa faini ya kuzidi kwa mifugo na
kuandikiwa risiti kuwa ni faini kwa ajili ya kulisha mifugo kwenye mashamba ni
Misa Njigula wa kijiji cha Totowe ambaye alipigwa faini ya shilingi 1,275,000
kwa ajili ya ng’ombe 255,Masale Gidai wa kijiji cha Magamba alipigwa faini ya
shilingi 770,000.
Masele Julius wa kijiji cha Ifuko alipigwa faini ya shilingi
140,000,Mashala Kwilasa wa kijiji cha Galula
alipigwa faini ya shilingi 115,000 na mfugaji John Kasema wa Totowe
ametozwa faini ya shilingi milioni nane kwa ng’ombe 400.
“Tanzania ni nchi inayosifika
kuongoza kwa kufuata utawala wa sheria,sisi wafugaji wahamiaji tumechoka
kunyanyaswa, kukandamizwa, kukamatwa ovyo,kutozwa faini zisizo za haki kwanini
kama sisi ni wahalifu tusipelekwe mahakamani ili haki itendeke’’,anasema
mfugaji Machia.
Sisi wafugaji tulio wengi
hatujasoma,tunadhulumiwa mifugo yetu kwa miaka kumi sasa,wewe nenda ukaone
maisha ya watumishi wa umma wakiwemo watendaji , madiwani pamoja na viongozi ngazi
ya wilaya sisi wenye mifugo tunaonekana masikini,watumishi hao wametajirika
kutokana na mifugo yetu’’,anadai Machia.
Asilimia 90 ya wafugaji wahamiaji
katika Bonde la Songwe hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu hali ambayo
inawafanya baadhi ya watendaji serikalini kutumia mwanya huo kuwadhulumu kwa
kuwapiga faini ambazo sio halali.
“Kuna watendaji wawili kutoka vijiji vya Bonde la Songwe ambao wamechunguzwa
na TAKUKURU baada ya kubainika kufanya
udanganyifu kwenye risiti za malipo na kesi zao zipo mahakamani’’,anasema Adamu
Mbale afisa mifugo wa wilaya ya Chunya.
Beston Mwambene mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ihovyo anasema“Wafugaji
wanaamini kuwa kutajirika kwao ni kuongeza mifugo na sio kupunguza mifugo kwa
kuwa hata wakulima wanakuwa na maisha bora kwa kuongeza uzalishaji katika
mashamba yao hapa kinachotakiwa waelimishwe zaidi kuwa na mifugo bora’’,anasema
Mwambene.
Operesheni ya kukamata mifugo iliyozidi ilikuwa inafanyika tangu mwaka
2001 hadi 2010 katika Bonde la Songwe kwa kuhusisha wadau mbalimbali wakiwemo
watendaji wa serikali, mgambo, na polisi, hata hivyo kuanzia mwaka jana mkuu wa
wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro alipiga marufuku operesheni hiyo akitaka
wafugaji kwanza wapewe elimu ya kutosha.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro katika
kukabiliana na uingizaji wa mifugo ametoa wito kwa wakuu
wa wilaya tisa zinazopakana na wilaya yake wasitishe utoaji wa vibali vya
kusafirishia mifugo hasa Ng'ombe wanaoingia wilayani humo.
Wilaya
zilizofikia muafaka wa kutotoa vibali vya uingizaji na utoaji wa vibali vya
mifugo ni pamoja na Chunya, Mbarali, Mbeya, Mbozi, Mpanda, Sumbawanga, Sikonge,
Urambo na Manyoni.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment