Thursday, May 31, 2012

Wenye ulemavu Namtumbo wamesahaulika


 Na Albano Midelo
KITENGO cha wenye ulemavu wa akili kilichopo katika shule ya msingi Namtumbo mkoani Ruvuma kimetelekezwa hali ambayo imesababisha kitengo hicho kubakiwa na watoto  watano kati ya 26 walioandikishwa.
Kitengo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1997 ndiyo kitengo pekee kinachotoa elimu kwa watoto wenye ulemavu katika wilaya nzima ya Namtumbo kwa kuwa hakuna kitengo wala shule ambayo inatoa elimu maalum katika makundi mengine ya wenye ulemavu wa wasioona na viziwi.
Mkuu wa kitengo hicho Lezile Kampango akizungumza kwa masikitiko makubwa alisema ni dhahiri kitengo hicho kimesahaulika kwa kuwa tangu alipoletwa katika kitengo hicho mwaka 2005 hadi sasa kitengo hicho hakijawahi kupata fedha yeyote kwa ajili ya chakula pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa watoto hao.

“Huwezi kuamini lakini ndivyo ilivyo watoto hawa wanashindwa kupata chakula hali ambayo imesababisha watoto wengi kuwa watoro kwa mfano leo ni watoto watatu tu ndiyo wamefika shuleni,mimi mwenyewe wakati mwingine nawachukua hadi nyumbani kwangu kuwapatia chai na chakula changu ili waendelee kusoma,mlemavu bila chakula hasomi’’,alisisitiza.
Kampango amedai  kuwa wananchi na  serikali  katika wilaya ya Namtumbo licha ya kitengo cha wenye ulemavu katika wilaya nzima kuwa kimoja wameshindwa hata kujenga darasa moja kwa ajili ya watoto hao hali ambayo inamlazimu kuwafundisha wanafunzi hao chini ya mti na wakati wa mvua anakwenda kuwafundishia katika nyumba yake.
“Natamani kuomba uhamisho kwenda mahali pengine ili elimu yangu niweze kuitumia katika mazingira bora na rafiki kwa wenye ulemavu,hebu fikiria mimi nawafundisha wanafunzi chini ya mti,wakati wa mvua nakwenda kuwafundishia  nyumbani kwangu,nimetoa taarifa kwa wahusika katika ngazi zote lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa’’,alisema.
Afisa elimu wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Rhoda Mbilinyi  amekiri wilaya nzima kuwa  kitengo kimoja tu chenye walemavu wa akili na kwamba wanafunzi katika kituo hicho wanachanganywa na wanafunzi wengine kwa kutumia elimu jumuishi na kwamba mfumo huo pia unatumika katika shule nyingine za wilaya hiyo kwa kuchanganyika na wanafunzi wengine wa kawaida.
Kuhusu ruzuku kwa wanafunzi wenye ulemavu katika kituo hicho Mbilinyi amesema ruzuku inawajumuisha wanafunzi wote wa shule ya msingi Namtumbo wakiwemo wenye ulemavu,hata hivyo amesema ruzuku inayopelekwa ni finyu na haitoshelezi mahitaji ya wanafunzi wakiwemo wenye ulemavu.
“Ni kweli wanafunzi wenye ulemavu ili waweze kusoma wanahitaji mazingira rafiki vikiwemo vivutio,katika kitengo cha walemavu Namtumbo kuna vivutio vichache kama vile mpira,filimbi,wakati fulani walikuwa wanapata uji,lakini hivi sasa uchangiaji umekuwa mgumu,tunahamasisha katika kipindi hiki cha mavuno wazazi waanze kuchangia kwa ajili ya kitengo cha elimu maalum Namtumbo’’,alisisitiza.
Mratibu wa elimu maalum katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo  Joseph Chengula amezitaja changamoto  ambazo zinakikabili kitengo cha elimu maalumu kwa watoto wenye ulemavu wa akili Namtumbo kuwa ni pamoja na upungufu wa walimu watalaamu ambapo katika Halmashauri nzima wapo walimu wawili tu.
Changamoto nyingine ni kitengo kukosa wafanyakazi wengine kama vile wapishi na walinzi,ukosefu wa miundombinu,vifaa vya kujifunzia na kufundishia na samani mbalimbali,ukosefu wa bajeti ya kuendeshea kitengo na kitengo kukosa usafiri .
Kulingana na mratibu huyo ,kitengo cha walemavu wa akili cha Namtumbo kinakabiliwa na matatizo makubwa katika majengo ambapo kitengo kina tundu moja la choo kati ya mahitaji ya matundu matano.
“Kitengo hakina nyumba hata moja ya mwalimu kati ya mahitaji ya nyumba mbili,hakuna stoo kati ya stoo mbili zinazohitajika, hakuna bwalo la chakula,jiko,hakuna chumba hata kimoja cha darasa kati ya mahitaji ya vyumba viwili, hakuna bweni hata moja kati ya mahitaji ya mabweni mawili na kwamba hakuna ofisi hata moja ya walimu kati ya mahitaji ya ofisi mbili’’,alisema.
Kulingana na Chengula Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo ina watoto wengi wenye ulemavu wa aina mbalimbali ambao wanastahili kuwepo shuleni lakini wanakosa fursa hiyo kutokana na wilaya hiyo kukosa shule kwa ajili ya watoto wenye ulemavu.
Takwimu za mwaka 2011 zinaonesha kuwa katika wilaya ya Namtumbo kuna wanafunzi wenye ulemavu  wapatao 181 ndiyo wanaosoma  katika shule mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu wa akiri 34,wasioona 18,viziwi 11,walemavu wa viungo 109 na albino tisa.
Hata hivyo takwimu hizo zinaonesha kuwa kuna wanafunzi wenye ulemavu wapatao 71 ambao walitakiwa kuandikishwa shule hawasomi wakiwemo wenye ulemavu wa akiri 21,wasioona mmoja,viziwi 11,wenye ulemavu wa viungo 35 na albino watatu.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Kassim Ntara anasema Halmashauri hiyo haijawahi kupata fedha kutoka TAMISEMI kwa ajili ya walemavu pekee isipokuwa kuna fedha inayoletwa kwa maendeleo mengine ya elimu,afya na huduma nyingine.
Hata hivyo Ntara anasema  katika mwaka mpya wa fedha wa 2012/2013 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni saba kwa ajili ya kitengo cha walemavu wa akili Namtumbo na kwamba kuna mpango wa kujenga shule moja ya wenye ulemavu kama ilivyoagizwa na serikali.
Takwimu za shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni(UNICEF) za mwaka 2002 zilionesha kuwa asilimia 98 ya watoto wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hawapatiwi kabisa elimu jambo ambalo ni hatari kwa walemavu.
Imeelezwa kuwa asilimia hii ndogo inasababishwa na kuwepo kwa shule chache maalum hapa nchini kwa ajili ya watu wenye ulemavu,ukosefu wa wataalamu,sera na sheria nyingi za nchi hizo  hazitaji moja kwa moja au kutoa utaratibu mzuri wa kutoa elimu kuhusu wenye ulemavu,ukosefu wa vifaa maalum na muhimu vya kuwawezesha kusoma pamoja na miundo mbinu duni  isiyokidhi mahitaji  ya watu wenye ulemavu.


No comments:

Post a Comment