Na
Albano Midelo
“SAMAKI
wengi wametoweka akiwemo aina ya
kachinga ambaye ni maarufu katika ziwa Rukwa kutokana na ladha yake hivi sasa hatumuoni tena’’,anasema mvuvi Stanley Rwamba(65) wa kijiji cha Totowe
Bonde la Songwe Chunya mkoani Mbeya.
|
Rwamba
anabainisha kuwa jamii ya Samaki ambao wapo katika hatari ya kutoweka katika
ziwa Rukwa ni ngogo,shibe na kachinga
ambao walikuwa wanapatikana kwa wingi wakati wa mvua miaka kumi iliyopita.
Sensa
ya samaki ambayo ilifanywa mwaka 1999 katika ziwa Rukwa ilibaini kuwa ziwa hilo linazalisha samaki tani 7000 kwa
mwaka wakiwemo aina tatu za kambale ambazo ni kibonde,singa na poroko, magege, dagaa,
kapimoja na kachinga.
Uvuvi
wa kutumia kokoro unaofanyika katika fukwe za ziwa Rukwa
katika kata za Totowe, Ivuna na Kamsamba mkoani Mbeya umechangia kusababisha samaki katika ziwa hilo
kupungua kwa kasi.
Wavuvi
kwenye fukwe hizo wamebainika kutumia nyavu za kokoro kuvulia samaki licha ya
kwamba nyavu hizo haziruhusiwi kisheria kwa kuwa zinaharibu mazalia ya samaki pamoja na kuvua samaki
wadogo.
Fukwe
ambazo uvuvi wa kutumia kokoro umekithiri katika kata ya Totowe ni Handeni, Ihovyo, Mtanda, Kambipotea, Kwaboko, Mchangani
na Kisiwani.Wavuvi wamekuwa wanavua bila kuwa na hofu ya kukamatwa na maofisa
uvuvi ambao wanadaiwa kuchangia hali hiyo kuendelea kwa kuwa hawaonekani katika
sehemu zao za kazi.
Staniley
Rwamba mvuvi mkongwe katika ziwa Rukwa anasema wavuvi wameamua kutumia kokoro
ambazo haziruhusiwi kisheria kutokana na samaki wanaoruhisiwa kuvuliwa kisheria
katika ziwa hilo kuanza kutoweka.
Hata
hivyo wavuvi ambao walikuwa wanavua
katika ziwa hilo kila mahali walionekana kukosa samaki ,ambapo wavuvi
wanadai hali hiyo inachangiwa na idadi kubwa ya ng’ombe ambao wametia kambi
kwenye fukwe za ziwa Rukwa ambapo hula malisho ambayo ni mazalia ya samaki
ndani ya ziwa hilo.
Bonifasi
Yamlinga ni mvuvi katika fukwe ya Mchangani anasema maelfu ya ng’ombe kila siku
wanaingizwa hadi mita 300 ndani ya ziwa Rukwa kula nyasi ambazo ni mazalia ya
samaki .
Yamlinga
anabainisha kuwa licha ya samaki wengi wanaovuliwa ziwa Rukwa upande wa Chunya
kuwa ni wale ambao hawaruhusiwi kuvuliwa kisheria, amedai hakuna afisa samaki
wa kata anayehoji uhalali wa kuvua samaki hao hali ambayo inasababisha wavuvi
kuwa huru na kuendelea kufanya uvuvi haramu katika ziwa Rukwa.
Hata hivyo afisa uvuvi na maliasili wa Halmashauri ya wilaya Mbozi Agrey Ngalunga baada ya kuona samaki wengi wachanga wanaovuliwa ziwa Rukwa katika kata za Ivuna na Kamsamba serikali ilitoa ombi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ili wafunge shughuli za uvuvi kwa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili kila mwaka ili samaki waweze kuzaliana.
Hata
hivyo Ngalunga anabainisha kuwa ombi hilo ambalo walituma barua mwaka jana bado
halijakubaliwa na wizara husika.Ameongeza kuwa Halmashauri imetengeneza boti ya
kufanyia doria ziwani yenye thamani shilingi milioni 4.8
Anabainisha
zaidi kuwa kwa kutumia boti hilo mwaka
2010 wameweza kukamata kokoro 133 zenye thamani ya zaidi ya shilingi
milioni 79.5 na nyavu ndogo chini ya
nchi tatu 56 zenye thamani ya shilingi 168,000 ambazo hazikubaliki kisheria.
Kulingana
na Ngalunga mwaka 2010 kamati ya ulinzi
na usalama wilaya ya Mbozi kwa
kushirikiana na kikosi cha usimamizi wa raslimali uvuvi cha Tunduma wameweza
kukamata nyavu haramu kwenye maduka
mjini Tunduma zipatazo 2236 zenye
thamani zaidi ya shilingi milioni 137 ambazo ziliteketezwa hadharani kwa moto.
Utafiti
umebaini kuwa samaki aina ya kachinga wanaovuliwa katika ziwa Rukwa kwenye fukwe za kata ya Totowe wilayani
Chunya na kata za Kamsamba na Ivuna wilayani Mbozi wameanza kutoweka katika ziwa hilo na pale wanapopatikana wanauzwa kwa
bei ya juu.
Wavuvi kutoka fukwe za Kwaboko, Mtanda, Handeni na kisiwani ambao ni Peter Sasawata,Staniley Rwamba na John Sichalwe wanadai kuwa kutoweka kwa aina hiyo ya samaki kunatokana na kina cha maji kupungua,uvuvi wa kutumia kokoro unaofanywa na baadhi ya wavuvi katika ziwa hilo pamoja na mifugo mingi inayokula nyasi ambazo ni mazalia ya samaki.
Peter Sasawata mvuvi katika ziwa Rukwa anasema kuwa kwa wiki moja hadi mbili wavuvi wamekuwa wakivua si zaidi ya samaki watano aina ya kachinga ambapo miaka michache nyuma samaki hao walikuwa wanapatikana kwa wingi,ameshauri juhudi za watalaamu na serikali zinahitajika ili kukabiliana na uharibifu wa mazalia ya samaki ili kuzinusuru aina mbalimbali za samaki.
John Sichalwe amewataja samaki wengine ambao hivi sasa wameanza kutoweka kuwa ni magege na kapimoja na kwamba samaki aina ya kambare bado wanapatikana kwa wingi kwa kuwa samaki hao wanapenda kuishi katika matope ambayo yapo mengi ndani ya ziwa Rukwa ambalo kina chake kimejaa tope na mchanga.
Hata hivyo Sera ya Taifa ya mazingira
ya mwaka 1997 kuhusu sekta ya uvuvi kifungu cha 60 inaelekeza wazi kuwa uvuvi
utaendelezwa vema kwa kutumia vifaa vya
uvuvi vinavyofaa na njia bora za kuendeleza bidhaa zinazotokana na uvuvi
ambapo njia zinazoharibu mazingira
katika uvuvi zitadhibitiwa kwa sheria na kuhakikisha unafuu wa upatikanaji wa vifaa bora vya uvuvi
.
hotuba ya kambi ya upinzani wizara ya
uvuvi na mifugo katika Bunge la bajeti la mwaka 2011 iliyotolewa na Silvester
Kasulumbayi ilisema lipo tatizo kubwa la serikali kushindwa kusimamia
sekta ya uvuvi na kusababisha kuendelea
kuvuliwa kwa samaki wachanga wanaotokana na tatizo la uvuvi haramu.
“ Kupambana na uvuvi haramu huku nyavu
ndogo na vifaa vingine vikiendelea kuingia nchini kunakwamisha jitihada zote….
swali la kujiuliza….. kwa nini upande wa nchi jirani za Kenya na Uganda hawana
tatizo la nyavu ndogo? Huu ni mradi haramu wa maafisa uvuvi wa Tanzania dhidi
ya wavuvi wetu’’,anadai msemaji mkuu wa kambi ya upinzani.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

Asante kwa taarifa hii na taarifa zako zingine, ambazo nazisoma kwa makini. Unafanya kazi kubwa ya kutuelimisha. Ubarikiwe.
ReplyDelete