|
| Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mkapa Hans Mwailima |
Na Albano
Midelo
KATIKA hali isiyokuwa
ya kawaida shule ya msingi Mkapa
iliyopo katika kata ya Rwinga
wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma ambayo imepewa jina la Rais mstaafu Benjamin
Mkapa haina nyumba hata moja ya walimu.
Mwalimu mkuu wa shule
hiyo Hans Mwailima alisema kuwa shule hiyo ina walimu 11 lakini hakuna nyumba
hata moja ya mwalimu hali ambayo imesababisha walimu kuhangaika kupanga nyumba
kwa wanakijiji ambazo hazipatikani kwa urahisi na kusababisha kero kubwa kwa
walimu.
“Sijawahi kuona shule
inakosa hata nyumba ya mwalimu mkuu,lakini hapa licha ya shule yetu kupewa jina
la Rais mstaafu Benjamin Mkapa shule ina matatizo makubwa katika miundombinu
yake kwa kuwa hata vyumba vya madarasa vilivyopo ni vinne tu inakatisha tamaa’’alisisitiza.
Baadhi ya walimu
wanaofundisha katika shule hiyo wakizungumzia kero hiyo ya nyumba za kuishi
walidai kuwa inawakatisha tama kwa kuwa wamelazimika kupanga kwa wanannchi
ambao wengine wana nyumba zilizoezekwa kwa
nyasi hivyo mwalimu kuishi katika nyumba ambazo hazina viwango.
Waemtoa wito kwa
kamati ya shule hiyo kwa kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa walimu wa
shule hiyo wanajengewa nyumba bora haraka ili waweze kutimiza majukumu yao ya
kufundisha wanafunzi kwenye mazingira yanayovutia kwa walimu na wanafunzi.
Uchunguzi umebaini
kuwa moja ya sababu kuu zinazochangia kuzorotesha maendelea katika shule hiyo
ni mgongano wa sera katika siasa kwa
kuwa uongozi ni wa vyama viwili vya CCM na CUF vyenye itikadi tofauti vinavyochangia
kukataza baadhi ya kazi za kujitolea kama vile kuwa na benki tofali kwa ajili
ya miradi ya maendeleo.
Mkuu wa shule ya
msingi Mkapa Mwailima anasema wakazi wa
eneo hilo hawataki kushiriki katika kazi za kujitolea hasa ufyatuaji wa
tofali hali ambayo inasababisha serikali kupitia ofisi ya mkurugenzi kushindwa
kuwasaidia vifaa vya viwandani kama mabati na saruji.
Uchunguzi umebaini
kuwa tatizo la nyumba za kuishi lipo karibu katika shule zote saba zilizopo
katika kata ya Rwinga mjini Namtumbo ambapo katika shule ya msingi
Kidugalo kuna nyumba moja tu ya mwalimu
kati ya mahitaji ya nyumba 13.
Mratibu elimu kata ya
Rwinga Thomas Komba amezitaja shule nyingine zinazokabiliwa na upungufu mkubwa
wa nyumba za walimu kuwa ni Rwinga,Selous,Minazini na Mandepwende.
Hata hivyo makamu
mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Kassimu Ntara amesema
anatarajia kuzitembelea shule hizo ili kubaini ukubwa wa tatizo na kushirikiana
na mkurugenzi ili kupunguza kero hizo zinazochangia kushusha elimu katika
wilaya hiyo.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment