Na Albano Midelo
TANGU mwaka 1961 hadi 1970 Bonde la
Songwe wilayani Chunya mkoani Mbeya lilikuwa ni ardhi oevu,yenye uoto wa
kijani na msitu mnene wenye miti mbalimbali ya asili.
Wakati huo wakulima waliweza
kuzalisha mazao ya chakula kwa wingi kutokana na bonde kuwa na ardhi oevu yenye
maji yaliokuwa yanatiririka kutoka mto Songwe ambao unaanzia milima ya Umalila
Mbeya na kumwaga maji yake ziwa Rukwa .
Bonde la Songwe ambalo linaundwa na
kata za Totowe,Galula,Namkukwe,Kanga na Mbuyuni wakati huo lilikuwa
linavutia maisha ya viumbehai wakiwemo binadamu, wanyamapori na ndege wa
aina mbalimbali ambao walikuwa wanaimba kwa furaha.
Mtu ambaye alifika kwenye bonde la
Songwe miaka ya 1970 akitembelea leo kwenye bonde hilo hawezi kuamini kwa kile
ambacho atakiona kutokana na mabadiliko makubwa ya kimazingira ambayo
yamejitokeza hivi sasa na kutaharisha maisha ya viumbe hai.
Katika bonde la Songwe hivi sasa miti
imetoweka na ardhi imebaki uchi,mto Songwe ambao ndiyo mto pekee unaomwaga maji
yake ziwa Rukwa kwa mwaka mzima upo katika hatari ya kutoweka,ziwa Rukwa
limesinyaa kuwa dogo na kina chake kinapungua kwa kasi.
Miti karibu yote iliyokuwa kivutio
katika Bonde la Songwe haipo tena,Bonde limejaa makorongo makubwa ambayo
yanatokana na mmomonyoko wa ardhi,vumbi zito na vimbunga vya mara kwa
mara limekuwa ni jambo la kawaida katika bonde hili.
Unapofika kwenye bonde hili kuanzia
mwezi wa Aprili hadi Novemba utaona upepo wenye vumbi zito ambao unaweza
kudhani mvua inataka kunyesha,vumbi hilo huwa zito kiasi kwamba huwezi kumuona
mtu aliye mbele yako.Hali hii inawafanya wakazi wa Bonde hilo kujifungia ndani
ya nyumba zao kuepukana na vumbi hilo.
Vumbi hilo ambalo unaweza kuliita
mvua ya vumbi huchukua kati ya saa nne au siku nzima,hali ambayo huleta kero
kwa wakazi kushindwa kuwajibika ipasavyo katika kazi mbalimbali za
kiuchumi,kijamii na burudani.
Katika Bonde la Songwe wakulima
waliweza kulima mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, alizeti, ufuta,
mtama,viazi vitamu,mpunga bila kuweka mbolea ya chumvichumvi,hivi sasa
Bonde hilo linakabiliwa na njaa kila mwaka kutokana na ukame unaotokana na
bonde kukosa mvua za uhakika.
Ziwa Rukwa kwenye bonde hili,tangu
uhuru limetoa ajira katika sekta ya uvuvi ambapo wavuvi wameweza kusomesha
watoto wao,kujipatia kipato kwa kuuza samaki na kupata kitoweo ambacho
kinajenga afya kutokana na samaki wanaopatikana kwenye ziwa hilo.
Hata hivyo maisha ya wakazi wa Bonde
hili yapo hatarini baada ya athari za kimazingira kuanza kujitokeza kutokana na
uharibifu wa mazingira ikiwemo kuanza kusinyaa kwa vyanzo muhimu vya maji
ambavyo ni mto Songwe na ziwa Rukwa .
Wakati wa masika maelfu ya tani za
mchanga,tope na takataka nyingine husombwa na kuingia mto Songwe na
kupelekwa ziwa Rukwa hali ambayo inasababisha kina cha maji cha mto na
ziwa kupungua kwa kasi.
Athari hizo za kimazingira zinachangiwa
na idadi kubwa ya mifugo ambayo inaendelea kuongezeka kwa kasi
kubwa kwenye Bonde la Songwe huku wafugaji hao wahamiaji kutoka kanda ya ziwa
wakifanya uharibifu wa mazingira kwa kufyeka miti ovyo kwa lengo la kujipatia
kuni,mkaa na mashamba.
Afisa mifugo,kilimo na ushirika katika
Halmashauri ya wilaya ya Chunya Adamu Mbale anasema idadi ya ng,ombe
katika bonde zima kati ya mwaka 1961 hadi 1970 ilikuwa ni 800 tu hali
iliyosababisha mazingira katika bonde hilo kuwa ya kuvutia.
Mbale anabainisha kuwa idadi ya ng’ombe
kwenye Bonde hilo iliongezeka kwa kasi na kuathiri mazingira katika
kipindi cha kuanzia mwaka 1981 hadi 1990 ng’ombe walifikia 173,681,mwaka 2000
ng’ombe walifikia 186,800 na hadi kufikia mwaka 2010 idadi ya ng’ombe ilifikia
286,800.
Mbale anasema eneo linalofaa kwa
ajili ya malisho wilayani Chunya ni hekta 1,353,300 na kwamba eneo ambalo
limepimwa na kutengwa kwa kwa ajili ya malisho ni 622,397.
Diwani mstaafu na mwenyekiti wa kamati
ya mazingira Bonde la Songwe William Mahenge anabainisha kuwa wafugaji
katika bonde hilo wanamiliki makundi makubwa ya ng’ombe kati ya 200 hadi 5000
kwa mfugaji mmoja na kusisitiza kuwa mifugo ni sababu kubwa ya
mazingira ya bonde hilo kuharibika.
Mifugo mingi imesababisha fukwe za ziwa
Rukwa upande wa Bonde la Songwe zilizopo kwenye vijiji vya kata ya Totowe
kukauka na kusababisha ziwa hilo kupungua ukubwa na kina hali
inayohatarisha uwepo wa ziwa hilo ambalo linashika nafasi ya nne kwa ukubwa
hapa Tanzania likitanguliwa na maziwa ya Tanganyika,Viktoria na Nyasa.
Fukwe ambazo zinapotea kwa kasi ni
pamoja na fukwe ya Handeni ambayo imekauka kwa kilometa 10,Ihovyo kilometa
tatu,Mtanda kilometa saba,kisiwani kilometa tisa,kambipotea kilometa
tano,Kwaboko kilometa sita na fukwe ya Mchangani kilometa tano.Kina cha
maji katika fukwe hizo hivi sasa ni chini ya meta moja .
“Fukwe hii ya kisiwani mwaka 1998
ilikuwa kilometa nane kutoka hapa ,unaweza kutembea katika kina cha maji chini
ya magoti hadi umbali wa meta 300 ndani ya ziwa,hali hii ikiendelea ziwa hili
linaweza kukauka au kuwa bwawa ’’, anasema John Mwakyoma mvuvi katika ziwa
Rukwa.
Peter Sasawata na Stanley Rwamba
ni wavuvi katika fukwe ya Mtanda wanasema fukwe hiyo mwaka 1994 ilikuwa
kilometa saba kutoka hapo ilipo leo na kwamba chanzo kikuu cha kukauka kwa
fukwe ni mifugo mingi ambayo inaingia kunywa maji na kula malisho ndani ya ziwa
kila siku.
“Mimi nimeishi katika kijiji cha Ihovyo
kwa miaka 11 wakati nafika hapa maji ya ziwa hili ulikuwa unayakuta baada ya
kutembea kwa dakika tano tu lakini hivi sasa inakulazimu kutembea zaidi ya saa
mbili ndipo unalikuta ziwa ’’,anasema Beston Mwambene mwalimu wa shule ya
msingi Ihovyo .
Mwambene anabainisha kuwa Kupungua kwa
kina cha maji kisanyasi kunasababisha ukubwa wa ziwa Rukwa kupungua,kina
kikiwa kifupi ziwa litaongezeka kwa muda kisha litarudi nyuma kwa kasi na
kwamba kuongezeka kwa joto kutasababisha kiasi kikubwa cha maji kupotea kwenda
angani hatimaye ziwa hilo linaweza kuwa bwawa.
“Kama kweli serikali inataka kuliokoa
bonde la Songwe lisigeuke jangwa na ziwa Rukwa lisipotee kwenye uso wa
Dunia,waache kuendekeza siasa kwenye mazingira, ziwa Rukwa litakauka, wakulima
wanazidi kusogeza mashamba ya mpunga kwenye fukwe za ziwa’’,anasisitiza
Mwambene.
Kuwepo kwa mifugo mingi kwenye Bonde la
Songwe sio tu kumechangia kuleta athari za kimazingira kwenye bonde hilo,bali
pia kumesababisha migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Migogoro hiyo imesababisha majeruhi na
vifo kwenye bonde hilo kwa mfano mwaka 2006 wafugaji watano walikufa na
wengine 11 kujeruhiwa vibaya katika kijiji cha Totowe bonde la Songwe.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Totowe
Paskalia Luwi anasema wafugaji walifikwa na mauti hayo kutokana na chuki ya
muda mrefu iliyojengeka kutokana na tabia yao ya kulisha mifugo yao kwenye
mashamba ya wakulima.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus
Kinawiro katika kukabiliana na uingizaji wa mifugo ametoa wito kwa
wakuu wa wilaya tisa zinazopakana na wilaya yake wasitishe utoaji wa
vibali vya kusafirishia mifugo hasa Ng'ombe wanaoingia wilayani humo.
Wilaya zilizofikia muafaka wa
kutotoa vibali vya uingizaji na utoaji wa vibali vya mifugo ni pamoja na
Chunya, Mbarali, Mbeya, Mbozi, Mpanda, Sumbawanga, Sikonge, Urambo na Manyoni.
Afisa wa bonde la maji la Rukwa
Idris Msuya anasema“mifugo iliyopo ziwa Rukwa inatisha hata mimi mwenyewe
nilipoiona mara ya kwanza ilinichanganya,nimeshuhudia maelfu ya mifugo
ambayo inaishi, kula na kunywa maji ziwa Rukwa kwenye fukwe
za kijiji cha Totowe.hali hii inatisha’’,anasema.
Hata hivyo Msuya anakiri kina cha maji
cha ziwa Rukwa kinaendelea kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na uharibifu wa
mazingira unaochangiwa na idadi kubwa ya ng’ombe katika wilaya
zinazozunguka ziwa Rukwa ambazo alizitaja kuwa ni Chunya, Mbeya, Sumbawanga,
Mpanda, Mbozi na Nkasi.
Kulingana na Msuya, Ziwa Rukwa hivi
sasa lina wastani wa kina cha juu cha maji cha mita 800, kina cha chini ni mita
nne , eneo la maji la ziwa hilo ni kati ya kilometa 800 hadi 2300
kutegemeana na kiasi cha mvua inayonyesha.
Makamu wa Rais Dk.Mohamed Ghalib Bilal
akizungumza siku ya mazingira duniani mwaka jana alisema baadhi ya
gharama za uharibifu wa mazingira tumekwishaanza kuzibeba
ambapo kutokana na uharibifu huo vina vya maji katika mabwawa, mito
na maziwa vimekuwa vikishuka.
Amebainisha kuwa Ziwa Rukwa limepungua
kwa kiasi cha kilomita saba, kina na ukubwa wa ziwa Manyara umepungua kwa
asilimia 65, na katika kipindi cha mwaka 1970 hadi 2006 ukubwa wa Ziwa Jipe
umepungua kwa asilimia 65.
“Ni dhahiri kuwa, hatuwezi kuitazama
miaka 50 ijayo kwa matumaini bila kutafakari hali ya mazingira. Hali hii
isipodhibitiwa haraka, mifumo ya mvua itabadilika, vyanzo vya maji vitakauka,
ubora wa maji utaathirika, bioanuai itatoweka, maeneo mengi yatakuwa
kame.’’,anasisitiza Dk.Bilal.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment