KWA mara nyingine Kisiwa cha
Zanzibar kimekumbwa na msiba mzito kutokana na kuzama kwa meli ya mv Skagit,
mali ya Kampuni ya Seagull, iliyokuwa ikisafiri kutoka jijini Dar es Salaam
ikiwa na abiria wanaokadiriwa kuwa kati ya 200 hadi 250 pamoja na mizigo
kuelekea Unguja, visiwani Zanzibar siku ya Jumatano Julai 18 saa saba mchana.
Hii ni ajali nyingine mbaya
kutokea visiwani humo ambapo Septemba mwaka jana, meli ya Spice Islander
inayomilikiwa na kampuni hiyo ilizama ikiwa safarini kuelekea Pemba ikitokea
Bandari ya Malindi, Unguja na watu zaidi ya 240 kupoteza maisha na wengine
619 kuokolewa.
Chanzo halisi cha kuzama kwa meli
hiyo kusini mwa Kisiwa cha Chumbe bado hakijafahamika wala idadi kamili ya
watu waliopoteza maisha nayo haijajulikana, ingawa taarifa za awali zinasema
hali mbaya ya hewa baharini ilichangia ajali hiyo.
Hadi tunakwenda mitamboni usiku,
taarifa zilizotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kwa Kaimu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mwinyi Haji Makame, zilisema
kuwa maiti za watu 15 zilikuwa zimepatikana, wakiwamo watoto wanne na raia
mmoja wa Kizungu, huku 124 wakiokolewa.
“Miili yote inapelekwa uwanja wa
Maitara kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao, lakini wako baadhi ya abiria
zaidi ya 124 wameokolewa wakiwamo raia 13 wa Kizungu na majeruhi wote
wamelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja,” alisema Makame.
Aliongeza kuwa shughuli za uokoaji
zinaendelea kufanywa na vyombo vyote vya usalama licha ya hali ya mawimbi
kuwa mbaya kiasi cha boti za uokozi kupata taabu ya kuwafikia abairia hao.
Naye msemaji wa Jeshi la Polisi,
Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Advera Senso, alisema meli hiyo inakadiriwa
kubeba abairia zaidi ya 200 wakiwamo watoto 31.
“Bado tunafuatilia zaidi na
tunafanya jitihada za uokoaji kwa kutumia helikopta ya Polisi na taarifa
nyingine zaidi tutatoa baadaye kadiri zinavyopatikana maana wote tunaelekea
huko,” alisema.
Hata hivyo, taarifa zilizotufikia
kutoka visiwani humo ni kwamba shughuli za uokoaji zinaendelea na boti
zisizopungua nne zimekwisha kufika eneo la tukio kwa ajili ya kuwaokoa abiria
hao.
Meli hiyo mara kwa mara imekuwa na
matatizo ya kiufundi na kusababisha kupata hililafu ikiwa katikati ya safari
baharini.
Mwezi Mei abiria zaidi ya 300
walinusurika kufa baada ya meli hiyo kushika moto ulioanzia kwenye injini
wakati ikitokea Pemba kwenda Unguja.
Kipindi hicho taarifa zilisema
meli ilikuwa ikitokea Bandari ya Mkoani na ilipokaribia eneo la Nungwi
ilikwenda mwendo usio wa kawaida na kupoteza mwelekeo na kisha kuzima kabisa
injini.
Bunge laahirishwa
Kutokana na ajali hiyo, Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Baraza la Wawakilishi, yaliahirisha
vikao vyao jana ili kutoa nafasi kwa baadhi ya viongozi kuelekea eneo la
tukio.
Hata hivyo, mjini Dodoma, wabunge
wa kambi ya upinzani walilazimika kutoka bungeni kwa nguvu baada ya Spika,
Anne Makinda, kupuuza hoja ya Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (CUF) ya
kuomba Bunge lisitishe kikao chake kutokana na ajili hiyo, wakidai anapuuza
masuala ya msingi.
Ilikuwa majira ya saa 11 wakati
Bunge likianza awamu ya pili ya jioni ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Emmanuel Nchimbi, alikuwa akijibu hoja za wabunge, ndipo Hamad aliomba
mwongozo wa Spika wa Bunge akitaka bajeti ya wizara hiyo ipitishwe kwa
mafungu ili wabunge waende kwenye tukio hilo.
Hamad alitumia kanuni ya 47 (3)
inayosema kuwa hoja itatolewa na mbunge kwa kusimama mahali pake na kuomba
idhini ya Spika kutoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge kwa madhumuni ya
kujadili jambo halisi la dharura na muhimu kwa umma.
Hata hivyo Spika Makinda alikataa
kuahirisha shughuli za Bunge akisema kanuni hiyo inatumika vibaya, kwani
ilitakiwa jambo hilo liwe limetokea eneo lililo karibu na Bunge.
Alisema watahitajika wabunge
wawahi kutoa damu au msaada wowote wa haraka lakini kwakuwa limetokea
Zanzibar, wabunge hawawezi kutoa msaada wowote kwa haraka, zaidi ya kupiga
simu kujua kilichotokea.
“Nimeshawasiliana na waziri
anayehusika na majanga na wamekubaliana kuwa awasiliane na wahusika waliopo
kwenye eneo la tukio na kisha tutajua tutakavyojipanga,” alisema Makinda.
Baada ya kauli hiyo idadi kubwa ya
wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao waliamua kuondoka ndani ya ukumbi
kuonyesha ishara ya kutokubaliana na uamuzi huo.
Wabunge hao waliamua kwenda katika
Ukumbi wa Pius Msekwa huku wengi wakilia wakionyesha kuguswa na tukio hilo.
Wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge,
Hamad Rashid, aliwaambia wenzake kuwa alipata taarifa juu ya kuzama kwa meli
hiyo na anafanya utaratibu wa kupata ndege ya serikali.
Alisema alijaribu kuwasiliana na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Uratibu na Bunge, William Lukuvi, bila mafanikio kuwajulisha na kupanga
utaratibu.
Alibainisha kuwa watachagua baadhi
ya wabunge wa Bara na Visiwani pamoja na kuomba ndege ya serikali ili waende
Zanzibar.
“Watu wamekufa Spika hataki
kuahirisha Bunge, sisi hatukubali kuendeshwa na watu wasiojali utu,” alisema Hamad.
Hata hivyo, jitihada za Spika
kutaka Bunge liendelee na hoja hiyo hazikufua dafu baada ya Waziri Nchimbi
kuwasilisha hoja yake kumwomba akubali kuahirisha shughuli za Bunge kutokana
na udharura wa kuzama kwa meli hiyo.
Dk. Nchimbi akitumia kanuni ya 58
(5) ambayo inasema endapo hoja imefikishwa bungeni, mtoa hoja anaweza
kuiondoa hoja yake kwa kusimama mahali pake na kusema: “Ninaomba ruhusa
kuondoa hoja.”
Aidha Dk. Nchimbi alisema kuwa
kutokana na Spika kumwelekeza yeye kuwasiliana na Kamishina wa Zanzibar,
ilibainika kuwa hali ni mbaya na kamishna alimweleza kuwa yupo katika eneo la
tukio, hivyo kwa muda aliofikiria kuwa angeweza kuwasilisha hoja hautoshi,
hivyo kuomba kuondoa hoja hiyo.
Spika Makinda aliwauliza wabunge
kama wanaafiki hoja hiyo kuondolewa na wabunge walikubaliana nayo na kisha
akawataka wajumbe wa kamati ya uongozi kukutana ili kujadili jambo hilo na
kuangalia njia sahihi za kuchukua.
Spika kung’olewa?
Baadhi ya wabunge wameanza
kuwahamasisha wenzao kupiga kura ya kutokuwa na imani na Spika wa Bunge.
Wabunge hao walifikia hatua hiyo
kwenye kikao cha dharura walichokifanya jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa kwa
lengo la kufanya maandalizi ya kwenda Zanzibar kuhudhuria msiba wa wenzao
waliozama katika ajali meli ya Skagit.
Mbunge wa Mji Mkongwe, Muhammad
Ibrahimu Sanya (CUF), alisema Spika Makinda hana utu ndiyo maana aligoma
kuahirisha shughuli za Bunge ili kutoa nafasi ya watu kushiriki kwenye jambo
hilo.
“Huyu Spika hatufai, yaani vifo
vikitokea kwa watu wa Bara yeye ndiyo ataona kuna uzito…hapa alikufa Amina
Chifupa tukaahirisha Bunge, sasa iweje wenzetu wamekufa kule Zanzibar yeye
akatae kuahirisha shughuli za Bunge? Jamani tujipange kupiga kura za kutokuwa
na imani naye, ameonyesha kushindwa kulihimili Bunge,” alisema.
Mbunge mwingine kutoka Zanzibar
alisema hawaoni sababu ya kuendelea na mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi kwa sababu wapiga kura wao ndio waliofariki dunia.
“Tuna raha gani ya kuendelea
kujadili hotuba ya bajeti, huyu Spika tumedhihirisha hana uwezo wa
kutuongoza, hatufai, waliokufa kule ni binadamu si paka wala wanyama,”
alisema.
CHANZO; TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment