Na Albano
Midelo
Wakazi zaidi ya 4000 wa kijiji cha Mkili kata ya Ngumbo
wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma kilichopo
mwambao mwa ziwa Nyasa, wanaathirika na madawa yanayomwaga kwenye mto Ndumbi ambao maji yake wanayatumia katika
shughuli mbalimbali ya nyumbani.
Wananchi wa kijiji hicho wanategemea mto huo
kwa kila kitu ikiwemo maji ya kunywa hivyo sumu zinazomwagwa kwenye mto huo
zimeleta athari kubwa ikiwa ni pamoja na wananchi kuugua magonjwa ya homa za matumbo
wakati wote na wengine wameripotiwa kupoteza maisha.
Takwimu
zinaonesha kuwa mwaka jana pekee katika kipindi cha mwezi Septemba hadi Novemba
watu watano walipoteza maisha katika kijiji cha Mkili baada ya kupata magonjwa
ya homa za matumbo yanayotokana na unywaji wa maji yenye kemikali katika mto
Ndumbi au kula chakula ambacho kimeathirika na kemikali hizo.
Uchunguzi
uliofanywa katika kijiji hicho pamoja na vijiji jirani umebaini athari kubwa
zaidi katika kipindi cha kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba kila mwaka wakati
ambao kina cha maji katika mto huo kinakuwa kimepungua katika kiwango kikubwa.
Sumu
zinazomwagwa kwenye mto huo uchunguzi umebaini kuwa zinatokana na baadhi ya wananchi wanaofanya uvuvi haramu
kwa kutumikia kemikali zenye sumu katika mto Ndumbi ambao unamwaga maji yake
ziwa Nyasa.Wananchi hao wanategemea mto huo kwa maji ya
kunywa,kuoga,kupikia,kumwagilia bustani.
Wananchi
wanaoishi kwenye milima ya Livingstone ambako mto Ndumbi unaanzia wanadaiwa kufanya uharibifu wa kumwaga sumu
mbalimbali zikiwemo madawa ya kuulia wadudu kwenye kahawa ambazo ni
gramakson,DDT,Blue copper,mbolea ya urea pamoja na sumu za kienyeji aina ya
mtunyungu ambazo zinauwa samaki pamoja
na viumbe wengine kwenye mto huo.
Hata
hivyo uchunguzi umebaini kuwa wanaoathirika
sio wakazi wa kijiji cha Mkili pekee bali wakazi wa vijiji vingine vya
jirani mwambao mwa ziwa Nyasa wanaolazimika kunywa maji ya sumu za kemikali za
viwandani na mimea vikiwemo vijiji vya Ngumbo,Yola,Mbuli,Ndonga,Liwundi
na Ngumbo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wanakunywa maji ambao sio safi na
salama kutokana na kukosa maji ya bomba tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1961.
Tilia
Woka ni mkazi wa kijiji cha Mkili ambaye
anaishi eneo la milimani jirani na mto Ndumbi anasema wakazi wa kijiji cha
Mahande ndiyo wanaofanya vitendo vya kutia kemikali zenye sumu kwa lengo la
kuvua samaki waliopo kwenye mto Ndumbi kila mwaka bila kujali athari ambazo
zinajitokeza kila mwaka.
“Wavuvi
hao haramu kila mwaka kwa siri wanatia sumu katika eneo la chanzo cha mto kisha
dawa hiyo kadri maji yanavyoshuka kuelekea ziwani hujichanganya na kuwalewesha
samaki huku wengine wanakufa ,wavuvi hao hufuata mto huo huku wakiwakamata
samaki waliolewa na kuwafanya kitoweo”,anasema.
“Wavuvi
hawa haramu ni wajanja sana wanawahi asubuhi majira ya saa 12 wakiwa katika kikundi na kuweka dawa kwenye
mto Ndumbi ,dawa hiyo inafika ziwani majira ya
kumi jioni,wao hawafiki hadi ziwani wanakuwa wameshapata samaki kabla ya kufika ziwani,wengi wanaokula samaki
hao wanalalamika kuumwa matumbo na tunaomba serikali iongeze ulinzi ili
kuwakamata waharifu hawa wanaohatarisha maisha ya wananchi’,anasema Moses Hyera
mkazi wa kijiji cha Mkili.
Januari
Haule anayeishi kando kando mwa mto Ndumbi, anasema wakazi wa eneo hilo
wanaathirika kutokana na madawa yanayowekwa
kwenye mto huo hasa kuugua
matumbo,kupoteza maisha na mifugo mingi
inakufa na kusababisha umaskini mkubwa kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa
“Mwaka
2010 wavuvi hao haramu waliweka kwa awamu tano dawa hizo zenye kemikali kwenye
mto Ndumbi na kuleta athari kubwa hasa kwenye mazalia ya samaki aina ya magege
na mbelele ambao wanapenda kuzaliana mahali ambapo maji ya mto yanaingia ziwa
Nyasa hivyo wanauwa samaki wengi kwenye mto Ndumbi, samaki wanatoweka hasa
mwaka 2010 hali ilikuwa mbaya
zaidi”,anasema.
Utafiti ambao umefanywa katika mto Ndumbi
umebaini kuwa maji yake hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu pamoja na
viumbe wengine kwa kuwa yameonekana yana kemikali mbaya za sumu hasa kutokana
na kumwaga sumu mbalimbali zikiwemo zile zinazodaiwa kutoka katika mabomba ya
maji taka yaliotegwa katika hospitali ya misheni Litembo ambayo yanamwaga maji
kwenye mto huo na kuishia ziwa Nyasa.
Mganga
mkuu wa kituo cha afya Mkili Thomas
Magulilo anasema maji katika mto Ndumbi hayafai kabisa kwa matumizi ya binadamu
na kwamba wananchi wa kijiji hicho waliagizwa kuhakikisha kuwa wanachemsha maji
hayo kabla ya kunywa ambapo uchunguzi umebaini kuwa asilimia 99 ya wakazi wa
kijiji hicho wanakunywa maji kutoka kwenye mto Ndumbi au ziwa Nyasa bila
kuchemsha wala kuweka dawa za kuyatibu kama water guard.
“Asilimia
90 ya watu wanaofika kupima katika kituo hiki cha afya, wanagundulika kuwa na
vijidudu vya ugonjwa wa homa za matumbo hivyo hali ni mbaya,katika kijiji kizima
hakuna kisima cha maji wala bomba,wananchi tunawaelimisha kuchemsha maji wengi
wanadai hayana radha wanaendelea kunywa maji bila kuchemsha”,anasema mganga wa
kituo cha afya.
Bosko
Ndimbo mkazi wa kijiji cha Mahande anasema katika kijiji hicho watu wengi
wanatumia mbolea aina ya urea kuulia samaki kwenye mto huo hivyo mifugo mingi
inateketea iwapo inakunywa maji au kula vyakula vilivyochanganywa na mbolea ya
urea pamoja na dawa za asili aina ya utupa.
“Mwenyekiti
wa kijiji cha Mkili Kisika Mahoya anasema utiaji wa sumu sio tu kwamba
unafanyika kwenye mto Ndumbi pekee bali pia unafanyika kwenye mito mingine inayopita
katika kijiji hicho inayoitwa Mnywamaji na Chipindi inayomwaga maji yake ziwa
Nyasa na kusisitiza kuwa tatizo hilo ni kubwa na linaweza kuleta madhara mkubwa
ya kiafya na kimazingira.
Imanuel
Kipera ni kaimu afisa mtendaji wa kata ya Ngumbo anasema madawa ya kahawa
yalipigwa marufu kutumika hata hivyo baadhi ya wananchi ambao wamezificha dawa
hizo ndiyo wanaofanya uvuvi haramu kwenye mito
na kuhatarisha maisha ya viumbe hai.
“Mimi
kitaaluma ni afisa wa mifugo na kilimo,madhara ya madawa haya kwa samaki ni
kwamba kuanzia eneo ambalo unakuwa umemwaga sumu hadi mto unakoelekea viumbe
wote wanaathirika kuanzia samaki,mifugo na
watu ambao wanatumia maji hayo,mtu anayekula samaki wenye sumu anaweza
kupata magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo na kansa ambayo hutokea baada ya
muda mrefu”,anasema.
Hata
hivyo anasisitiza wananchi kupatiwa elimu ili kutambua afya ni jambo bora zaidi
kuliko kupata kitoweo na kwamba kuna baadhi ya madawa ya kahawa ya maji ambayo
wanayatumia yana athari na madhara
makubwa na kwamba serikali ya kata inachukua hatua za kukabiliana na wavuvi hao
haramu ambao wanafanya kazi hiyo kwa siri na hata wengine wanatia dawa hizo
usiku.
“Kwa
kweli tatizo hili la kuweka sumu kwenye maji ambayo yanategemewa na wakazi
zaidi ya 3000 katika kijiji cha Mkili ni zito ,wananchi wengi wanaugua ugonjwa
wa homa za matumbo ,baadhi yao wanafariki kila mwaka,kata yetu haina kisima
hata kimoja wala bomba tunagemea kupata maji ya mito na ziwa Nyasa,tunaomba
serikali yenye nguvu itusaidia”,anasisitiza.
Mganga
mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela ameahidi ofisi yake kuendelea
kuwaelimisha wananchi umhimu wa kuchemsha maji pamoja na kufuatilia athari ambazo wanazipata wananchi wa kijiji
cha Mkili ambao wanaugua homa za matumbo kutokana na kutumia maji yenye kemikali tena
bila kuchemshwa.
Afisa
mazingira mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la
hifadhi na usimamizi wa
mazingira(NEMC) Pendo Kundya anasema viuatilifu vyote hatari vinavyohatarisha
maisha ya binadamu na vilivyopigwa marufuku kama
DDT na BLUECOPER inatakiwa wananchi kutoa taarifa kote nchini badala ya
kuendelea kuyatumia madawa hayo kinyemela.
Utafiti umebaini kuwa madawa hayo yaliomalizika
muda wake wa matumizi au kuharibika yameonekana katika maeneo yasiopungua 325
nchini kote ambapo Kati ya kemikali hizo zipo jamii ya madawa hatari
yanayopigwa vita ulimwenguni kote kutokana na kuhatarisha afya za binadamu na
mazingira ya viumbe hai wote kwa ujumla.
Anavitaja
viuatilifu chakavu vya kilimo kuwa ni pamoja na vile vyote ambavyo vinatumika
kuuwa wadudu,wanyama na kuzuia magonjwa
ya mazao na mimea yaliyozidi miaka miwili tangu kutengenezwa na kusisitiza kuwa
viuatilifu chakavu ni sumu kali iliyopo katika mazingira na inayoathiri afya ya
viumbehai wakiwemo binadamu na kwamba wananchi kote nchini wanapaswa
kuorodhesha kitaalam na watalamu wenye ujuzi kwa kutumia vifaa maalum vya
kinga.
Mkuu
wa mkoa wa Ruvuma Dr.Christine Ishengoma amewaagiza wakuu wote wa wilaya katika
mkoa kusimamia na kuvilinda vyanzo vyote vya maji pamoja na kuwachukulia hatua kali wote ambao
wanabainika wanalima au kufanya uharibifu katika vyanzo hivyo ili kulinda
maisha ya viumbehai wote na hasa binadamu.
Hata
hivyo uchunguzi umebaini kuwa vyanzo vya maji katika maeneo mbalimbali nchini
vimekuwa vikiendelea kufanyiwa uharibifu mkubwa licha ya serikali kupiga
marufuku shughuli zozote ambazo zinaharibu vyanzo hivyo.
Serikali mnamo mwaka 2002 ilipitisha mwongozo
wa namna ya kutunza vyanzo vyote vya maji vilivyopo ili visipotee wala
kuchafuliwa.Sera hiyo ya maji inalenga kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji
vilivyopo vinatunzwa,kulindwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaozingatia uwiano
wa mahitaji ya viumbehai wote wakiwemo binadamu ,wanyama, mimea,wadudu pamoja
na viumbe hai wote ambao hawawezi kuishi bila maji.
Ili
kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinatunzwa na kuwa endelevu kwa manufaa ya
viumbehai vya sasa na vijavyo ni vema kutotupa wala kumwaga uchafu au kemikali
za sumu karibu na vyanzo hivyo,,kutochoma misitu ovyo,kupanda miti inayofaa au
miti rafiki kwa maji karibu na vyanzo vya maji,kutojenga vyoo karibu na vyanzo
vya maji,kutochimba mchanga au madini ndani
au karibu na vyanzo hivyo pamoja na kutosafishia madini au kitu kingine
katika vyanzo.
Mwandishi wa makala haya ni mwanafunzi
wa chuo kikuu huria cha Tanzania mwaka wa pili katika shahada ya uandishi wa
habari anapatikana kwa simu 0766463129, baruapepe albano.midelo@gmail.com
No comments:
Post a Comment