WANASAYANSI mbalimbali
wanaoendesha tafiti mbalimbali za kutafuta tiba na chanjo ya Ukimwi,
wameitangazia dunia kuwa hatua waliyofikia sasa wanauona ugonjwa huo ‘siyo
hatari tena’ kwa sababu wanazo silaha zote za kuweza kukabiliana nao.
Ila wakasema, kinachowakwamisha ni
ukosefu wa fedha ambazo zinahitajika katika kuendeleza tafiti na kuweka sera
mpya za kukabili Virusi Vya Ukimwi (VVU) duniani.
Hayo yalibainika kwenye siku ya
pili ya Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika mjini Washington DC,
Marekani na unahudhuriwa na watu zaidi 22,000 miongoni mwao wakiwamo
wataalamu wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo
toka karibu kila kona ya dunia.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo
vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari cha Mkutano huo na gazeti
hili kufanikiwa kupata nakala yake, ilieleza kwamba jopo la wanasayansi nguli
duniani walikiri kuwa wamefanyia VVU utafiti wa kutosha ndiyo maana wanatamba
kuwa wamefanikiwa katika kuvidhibiti.
“Kwa sasa tunazo silaha zote
za kisayansi kumalizia mbali gonjwa hili la Ukimwi. Kilichobaki ni kutumia
kikamilifu utaalamu huu katika fursa hii tuliyo nayo,” alisema Rais wa
Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly
Katabira.
Kiongozi huyo ambaye pia ndiye
Mwenyekiti wa Mkutano huo akitokea nchini Uganda, aliongeza: “Kufanikisha
hilo ni lazima tukubali kubadili mfumo kwa maana kwamba kuweka sera mpya
zitakazowezesha kuokoa kundi linaloathirika zaidi na ugonjwa huu.”
Dk Katabira alifafanua:
“Kinachohitajika ni kuweka mfumo utakaowashirikisha wafadhili na watunga sera
katika kuweka mpango mzuri wa pamoja tuweza kulimaliza tatizo kwa silaha hizi
za kisayansi.”
Naye Mtaalamu wa Tiba katika Chuo
Kikuu cha California, Profesa Diane Havlir alisema: “Ujumbe wangu kwenu, hasa
kwa watunga sera ni kwamba: endeleeni kuwekeza katika mipango ya kisayansi.”
Kwenye mkutano huo walishiriki pia
wanasayansi wenye dawa na ushahidi unaoonyesha kuwa katika miaka ya karibuni
zimeonyesha dalili nzuri za kutibu Ukimwi na kifua kikuu (TB).
Wataalamu wengi wa afya waliunga
mkono kauli hiyo wakisema kwa sasa kuna uelewa mkubwa wa kitaalamu juu ya
muundo na tabia ya VVU hivyo ni rahisi kwao kutengeneza dawa kwa ajili ya
kuzuia, kutibu na chanjo.
Tafiti za awali
Kauli ya wanasayansi hao imekuja
baada ya miaka 30 ya kipindi kigumu cha kutafiti namna ya kupata chanjo au
tiba ya ugonjwa huo ambao umeua mamilioni ya watu duniani, hususan wataalamu
na nguvu kazi inayohitajika kuimarisha uchumi.
Waligundua VVU mwaka 1981 na
ilikuwa vigumu kupata dawa ya kuviua kwa sababu ya tabia zao na uwezo wa
kujigeuza kuwa sehemu ya mwili na kutumia selikinga kuzalisha virusi wengine.
Wanasayansi hao walitoa kauli hizo
za matumaini kukabili VVU mbele ya viongozi mashuhuri wa kisiasa, akiwemo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Rais wa Ufaransa,
François Hollande.
Mtaalamu anayesimamia mipango ya
afya Ikulu ya Marekani, Profesa Antony Fauci, ambaye piya ni Mkurugezi wa
taasisi ya nchi hiyo ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID),
alikuwa miongoni mwa waliohutubia na kusifu hatua iliyofikiwa na wanasayansi
duniani.
Ofisa Mkuu na Rais wa Taasisi ya
Mapambano ya Ukimwi nchini Marekani, Phill Wilson aliweka bayana kuwa
pamoja na ugonjwa huo kuonekana tishio hasa kwa nchi zinazoendelea, hakuna
nchi, hata zile tajiri, ambazo zinaweza kutamba haziathiriki na tatizo hilo.
Kwa hivyo akasema mikakati na sera
mpya za kisayansi zinahitajika dunia nzima, hivyo akawataka wanasayansi hao
‘kuanika hadharani silaha zao’ ili zianze kutumika ulimwenguni kote.
Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa
Mataifa wa Mapambano ya Ukimwi (UNAIDS), Sheila Tlou aliwataka wataalamu hao
kuweka mkakati mzuri utakaowezesha silaha hizo za kisayansi kuelekezwa katika
nchi maskini hasa barani Afrika.
Wanasayansi hao wamekuja na kauli
hizo za matumaini wakati ambapo tayari wamefanya tafiti mbalimbali na kugundua
tabia za VVU ikiwa ni pamoja na vitu ambavyo vinaviwezesha kushambulia seli
nyeupe za damu, maarufu kwa jina la CD4, ambazo ni sehemu ya kinga ya mwili
wa binadamu.
Licha ya tafiti mbalimbali
kuonyesha kuwa kuna kila dalili ya kupatikana kwa chanjo, miaka michache
iliyopita, waligundua moja ya dawa zinazotumika kupunguza makali ya VVU (ARV)
ijulikanayo kama Truvada, yenye uwezo wa kumkinga mwathirika kumwambukiza
mpenzi wanayeshiriki naye tendo la ndoa.
Wiki chache zilizopita, Mamlaka ya
Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) iliidhinisha Truvada, ambayo ilianza
kutumika sehemu mbalimbali duniani tangu mwaka 2004, kuwa ni tiba ya kuzuia
kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kwa mujibu wa maelezo ya FDA,
mwathirika anayetumia dawa hiyo anaweza kujamiiana na mwenza wake ambaye hana
VVU bila kutumia kondomu na hatomwambukiza.
Matokeo ya utafiti huo wa ARV
yaliwahi kuchapishwa kwenye gazeti hili toleo la Februari 12, mwaka huu. Kwa
mujibu wa FDA, Truvada inatarajia kuanza kutumika na kusambazwa duniani
katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
CHANZO:MWANANCHI PUBLICATION
|
No comments:
Post a Comment